Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'STOP'! VAR kutoongezewa majukumu EPL

VAR Pict

Muktasari:

  • Kupitia mabadiliko ya sheria yaliyoidhinishwa na Bodi ya Kimataifa ya Sheria za Soka (Ifab), Februari, VAR itaruhusiwa kuingilia uamuzi wa kona pamoja na kadi za pili za njano kuanzia mwezi ujao, huku waamuzi wakitarajiwa kutumia mfumo huo katika Kombe la Dunia baada ya ombi kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

LIVERPOOL, ENGLAND: LIGI Kuu England (EPL), inatarajiwa kukataa kuongeza mamlaka ya teknolojia ya usaidizi wa mwamuzi (VAR) msimu ujao baada ya mazungumzo kati ya uongozi wa ligi na Bodi ya Waamuzi (PGMO).

Kupitia mabadiliko ya sheria yaliyoidhinishwa na Bodi ya Kimataifa ya Sheria za Soka (Ifab), Februari, VAR itaruhusiwa kuingilia uamuzi wa kona pamoja na kadi za pili za njano kuanzia mwezi ujao, huku waamuzi wakitarajiwa kutumia mfumo huo katika Kombe la Dunia baada ya ombi kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

V 01

Hata hivyo, Ifab imeacha uamuzi huo kuwa wa hiari kwa mashindano na ligi mbalimbali kuamua kama zitautumia au la. Uamuzi wa mwisho wa EPL utafanywa na klabu katika mkutano mkuu wa msimu ujao utakaofanyika mwezi ujao, lakini PGMO imeishauri ligi hiyo kutopanua matumizi ya VAR.

PGMO ina hofu kuwa VAR kuhusishwa katika uamuzi wa kona na kadi za njano kunaweza kuongeza muda wa mechi, jambo ambalo linaweza kuwakera wadhamini wa matangazo ya televisheni na kuongeza presha kwa waamuzi. Pia kuna wasiwasi kuwa kusimamishwa mara kwa mara kwa mchezo kutavuruga mtiririko wa mechi, huku vyanzo vikieleza kuwa klabu nyingi hazina nia ya kupinga ushauri wa PGMO na kuongeza majukumu ya VAR.

Kwa upande mwingine, Fifa ina mtazamo tofauti, ambapo mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya shirikisho hilo, Pierluigi Collina pamoja na rais wa chombo hicho, Gianni Infantino, wanaamini kuwa uamuzi mbaya wa kona unaweza kuathiri matokeo ya mchezo wa Kombe la Dunia, hasa katika hatua za mtoano. Vilevile kutokana na kuwepo kwa mapumziko ya kunywa maji ya dakika tatu kila kipindi katika Kombe la Dunia, ongezeko la muda wa mchezo halionekani kuwa tatizo kubwa.

Katika EPL uwezekano wa kona moja kuamua msimu mzima ni mdogo kutokana na kuwepo kwa mechi 38, lakini tukio la Jumapili iliyopita ambapo mwamuzi Chris Kavanagh alikataa bao la kusawazisha la dakika za mwisho la Callum Wilson dhidi ya Arsenal baada ya ushauri wa VAR, linaweza kuwa na athari katika mbio za ubingwa na vita vya kushuka daraja.

V 02

Mkuu wa waamuzi wa PGMO, Howard Webb, anatarajiwa kulizungumzia tukio hilo katika kipindi cha Sky Sports cha Match Officials Mic’d Up, huku PGMO ikisisitiza kuwa uamuzi uliofanywa ulikuwa sahihi na ulifuata taratibu zote.

West Ham inatarajiwa kuwasilisha malalamiko kuhusu uamuzi wa kuipa Arsenal faulo baada ya Pablo kugusana na kipa David Raya, ingawa ndani ya klabu hiyo kuna uelewa kuwa malalamiko hayo huenda yasibadilishe chochote.

Ifab pia inatarajiwa kujadili tatizo la wachezaji kuvutana na kushikana kwenye kona ambalo limekuwa kubwa zaidi katika Ligi Kuu England msimu huu, baada ya Kombe la Dunia kumalizika japokuwa hadi sasa hakuna mapendekezo rasmi ya namna ya kulitatua.

V 03

FIFA KUONGEZA NGUVU ZA VAR

Kuna sababu kadhaa zinazoeleza kwa nini Fifa imeongeza mamlaka ya VAR hadi kuhusika na matukio kama kona katika Kombe la Dunia 2026, hatua ambayo imezua mjadala mkubwa katika ulimwengu wa soka.

Kwanza ni kuongeza usahihi wa uamuzi wa waamuzi. Katika soka la kisasa, matukio ya kona yanaweza kubadilisha matokeo ya mechi kwa kiasi kikubwa. Kona moja inaweza kusababisha bao, na ikiwa imepatikana kimakosa kwa mfano mpira uliotoka au haukutoka inaweza kuathiri matokeo ya timu nzima, hasa katika hatua za mtoano ambapo hakuna nafasi ya kurekebisha makosa.

Pili, Fifa inaamini teknolojia inapaswa kuendelea kuboresha haki ya mchezo, na kwa mujibu wa Infantino na Collina, VAR imeonyesha mafanikio katika kupunguza makosa makubwa kama penalti zisizo sahihi, mabao ya kuotea (offside) na kadi nyekundu zisizo sahihi. Kwa hivyo, hatua inayofuata ni kuipanua zaidi ili kufunika maeneo ambayo yanaweza kuwa na makosa ya kibinadamu.

Tatu, Fifa inaamini Kombe la Dunia ni mashindano ya kiwango cha juu zaidi, hivyo kila uamuzi lazima uwe sahihi kadri inavyowezekana. Katika mazingira ya mechi za mtoano, kosa la kona linaweza kuwa tofauti kati ya kufuzu na kuondolewa. Hii ndiyo sababu Fifa inataka kuhakikisha hakuna timu inayoathirika kutokana na makosa ya wazi ya waamuzi.

Nne, tofauti na ligi za ndani kama EPL, Kombe la Dunia lina idadi ndogo ya mechi na kwamba kuongeza muda wa VAR kidogo kutokana na uchunguzi wa kona au kadi za njano hakutaleta athari kubwa ya muda wa jumla wa mashindano. Hata hivyo, hoja hizo zinakosolewa na baadhi ya mashirikisho na ligi ambazo zinaamini kuwa kupanua VAR kunaweza kupunguza kasi ya mechi. Pia kuna hofu kuwa waamuzi wanaweza kupoteza mamlaka ya moja kwa moja uwanjani.