West Ham yalia na VAR
Muktasari:
- West Ham walidhani wamepata bao muhimu la mshambuliaji Callum Wilson katika dakika za nyongeza, bao ambalo lingeweza kuipa timu hiyo pointi muhimu kwenye vita vya kubaki Ligi Kuu England sambamba na kuathiri mbio za ubingwa wa Arsenal.
LONDON, ENGLAND: UONGOZI wa West Ham United unatarajiwa kuwasiliana rasmi na bodi ya waamuzi England, PGMO, kuomba maelezo kutokana na uamuzi wa VAR kufuta bao lao la dakika za mwisho dhidi ya Arsenal, Jumapili iliyopita.
West Ham walidhani wamepata bao muhimu la mshambuliaji Callum Wilson katika dakika za nyongeza, bao ambalo lingeweza kuipa timu hiyo pointi muhimu kwenye vita vya kubaki Ligi Kuu England sambamba na kuathiri mbio za ubingwa wa Arsenal.
Hata hivyo, baada ya mapitio ya VAR, bao hilo lilifutwa kwa madai ya kuwapo faulo iliyofanywa na Pablo dhidi ya kipa wa Arsenal, David Raya, kabla ya mpira kuingia wavuni.
Taarifa kutoka England zinaeleza West Ham sasa wanataka kupata maelezo ya kina kutoka PGMO pamoja na kuomba sauti ya mawasiliano kati ya mwamuzi wa kati Chris Kavanagh na mwamuzi wa VAR Darren England wakati wa tukio hilo.
Baada ya bao hilo kufutwa, Arsenal walishinda mchezo huo kwa bao 1-0 na kujiongezea nafasi kwenye mbio za ubingwa kwa kufikisha tofauti ya pointi tano dhidi Manchester City huku West Ham wakiendelea kubaki kwenye hatari ya kushuka daraja.