Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makocha 12 wa Abramovich kwenye mechi 1000 Chelsea

Makocha 12 wa Abramovich kwenye mechi 1000 Chelsea

Muktasari:

CHELSEA usiku wa leo Jumapili itashuka uwanja wa ugenini kukipiga na Sevilla kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

LONDON, ENGLAND. CHELSEA usiku wa leo Jumapili itashuka uwanja wa ugenini kukipiga na Sevilla kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wakati mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona kitakachotokea kwenye mchezo huo, Jumapili iliyopita, miamba hiyo ya Stamford Bridge ilikipiga na Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England na huo ulikuwa mchezo wa 1000 tangu timu hiyo ilipoanza kuwa chini ya umiliki wa bilionea Roman Abramovich mwaka 2003.

Bilionea huyo wa Russia aliinunua Chelsea kutoka kwa Ken Bates, Juni 2003 na kuwekeza pesa nyingi kuifanya The Blues kuwa tishio Ulaye, ikibeba mataji 16 ndani ya kipindi hicho cha miaka 17, huku mataji hayo ikiwamo Ligi Kuu England mara tano na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja mwaka 2012.

Wakati Abramovich akiweka uwekezaji wa zaidi ya Pauni 2 bilioni kwenye kikosi hicho tangu alipoanza kukimiliki, katika mechi hizo 1000 ameshuhudia makocha 12 wakipita na kufanya kazi chini ya umiliki wake. Hiki ndicho walikifanya makocha wote waliopita Chelsea kwa wastani wao wa ushindi kwenye kikosi hicho tangu Abramovich achukue timu.


1. Jose Mourinho (Juni 2004-Septemba 2007 & Juni 2013 – Desemba 2015)

Wastani wa ushindi: 63.6%

Akiwa na mataji matatu ya Ligi Kuu England katika awamu zake mbili alizoinoa Chelsea, bila ya shaka Jose Mourinho ndiye kocha aliyefanikiwa zaidi Stamford Bridge. Mreno huyo ndiye aliyekuja kuifanya Chelsea kuwa timu tishio kwenye Ligi Kuu England, ambapo alibeba ubingwa wa ligi kwenye msimu wake wa kwanza tu, kisha akabeba msimu uliofuatia kabla ya kufutwa kazi mwaka 2007. Mourinho alirudi Chelsea baada ya miaka sita na kurudi aliongoza tena timu hiyo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England na bila ya shaka ndiye kocha aliyeleta mataji mengi kwenye kikosi hicho cha Chelsea chini ya utawala wa Abramovich.

2. Carlo Ancelotti (Julai 2009 – Mei 2011)

Wastani wa ushindi: 61.5%

Ancelotti alitua Chelsea akiwa kocha mwenye hadhi kubwa na mtaalamu wa mchezo huo. Alibeba mataji mawili katika msimu wake wa kwanza na kuliteka soka la England. Lakini, mambo yalikuja kutibuka kwenye msimu wake wa pili na alifutwa kazi saa chache tu baada ya mechi ya mwisho mwaka 2011. Kocha huyo alifutwa kazi akiwa kwenye korido za uwanja wa ugenini huko Goodison Park. Baada ya hapo alikwenda kuzinoa PSG, Real Madrid na Bayern Munich na kote huko alibeba mataji. Kwa sasa anainoa Everton.

3.Antonio Conte (Julai 2016 – Julai 2018)

Wastani wa ushindi: 65.1%

Kama ilivyokuwa kwa Mtaliano mwenzake, Ancelotti, Conte naye alibeba mataji mawili ya ligi za ndani katika msimu wake wa kwanza. Lakini, maisha hayakuwa marefu sana alifutwa kazi kwenye msimu uliofuatia tu, 2017/18. Hata hivyo, kocha huyo hakuwa na wastani mbaya wa ushindi katika mechi alizoiongoza timu hiyo na kuna kipindi alihusishwa na mpango wa kurudi kwenye Ligi Kuu England kabla ya kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Inter Milan huko kwenye Serie A.

4.Frank Lampard (Julai 2019 – hadi sasa)

Wastani wa ushindi: 54.3%

Baada ya kushudia muongo mmoja wa kumtazama Lampard akiwa uwanjani kuitumikia Chelsea, bilionea Abramovich aliamua kumpa Lampard kazi ya ukocha wa kukinoa kikosi hicho kwenye majira ya kiangazi ya mwaka 2019. Kocha huyo alianza kwa wakati mgumu baada ya kumpoteza staa wake Eden Hazard, huku timu ikizuia kusajili. Hata hivyo, aliifikisha timu fainali ya Kombe la FA na kumaliza msimu ndani ya Top Four. Baada ya msimu kumalizika, kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Abramovich alifungulia pochi kunasa mastaa kwa ajili ya Lampard na kwa sasa Chelsea ipo vizuri kwenye ligi.

5.Roberto Di Matteo (Machi 2012 – Novemba 2012)

Wastani wa ushindi: 57.1%

Kocha mwingine Mtaliano, ambaye aliipa Chelsea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Di Matteo alichukua mikoba ya kuinoa Chelsea kutoka kwa Andre Villas Boas katikati ya msimu na kocha huyo aliwapa ruhusa wachezaji wa Chelsea kucheza bila ya woga. Bilionea Abramovich ndoto zake za kubeba ubingwa wa Ulaya zilikuja baada ya kocha huyo akiwa na huduma moto kutoka kwa straika Didider Drogba - walifanikiwa kubeba taji hilo mwaka 2012. Baadaye alipewa mkataba wa jumla, lakini mambo hayakuwa mazuri, akashindwa kumaliza msimu, akafutwa kazi. Kitu pekee alifanikiwa kubeba ubingwa wa Ulaya.

6.Claudio Ranieri (Septemba 2000 – Mei 2004)

Wastani wa ushindi: 53.8%

Mtaliano huyo alikuwa kocha wa kwanza kufutwa kazi kwenye zama za Abramovich. Kibarua chake Ranieri kilikuwa kwenye mashaka makubwa muda mfupi tu baada ya bilionea huyo wa Russia kuinunua Chelsea. Wengi wanaamini kuingoza kwake vyema Chelsea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2003 kulimfanya Abramovich afungue pochi na kuwekeza kwenye timu hiyo. Alipewa pesa ya kusajili, lakini uvumi wa kocha Sven Goran Eriksson kuhusishwa na kibarua chake ulikuwa umeshamili muda wote. Katika msimu wake wa mwisho aliifikisha pazuri Chelsea kwenye michuano ya Ulaya kabla ya kibarua chake kuja kuchukuliwa na Jose Mourinho.

7. Guus Hiddink (Februari 2009 – Mei 2009 & Desemba 2015 – Mei 2016)

Wastani wa ushindi: 53.1%

Wakati Chelsea ilipohitaji kuwa kwenye mikono imara, bilionea Abramovich alimfuata Guus Hiddink. Mdachi huyo alitua Chelsea kuchukua mikoba ya Scolari mwaka 2009 na mikoba ya Mourinho mwaka 2015. Hiddink alipelekwa Chelsea kwenda kuweka mambo sawa baada ya mara zote kuonekana kuwa hali si nzuri. Alishinda ubingwa wa Kombe la FA katika awamu yake ya kwanza na wachezaji walimtaka abaki. Kwenye awamu yake ya pili, aliikuta timu kwenye nafasi ya 16 katika msimamo na kuisaidia kumaliza ligi kwenye nafasi ya 10.

8. Rafa Benitez (Novemba 2012 – Mei 2013)

Wastani wa ushindi: 57.1%

Mhispaniola, Rafa Benitez alikuwa kocha wa tatu wa muda kwenye kikosi cha Chelsea. Benitez alitibua uhusiano wake na mashabiki wa Chelsea kutokana na wakati wake aliokuwa akiinoa Liverpool. Hivyo, wakati anapewa mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Stamford Bridge kazi ya kwanza ilikuwa kurudisha kwenye hali nzuri uhusiano wake na mashabiki wa Chelsea. Kushindwa kuwavutia mashabiki kulimfanya akomee kwenye kikosi hicho cha Chelsea kwa miezi saba tu, lakini aliisaidia timu hiyo kushika nafasi ya tatu kwenye ligi na kubeba ubingwa wa Europa League.

9. Maurizio Sarri (Julai 2018 – Juni 2019)

Wastani wa ushindi: 61.9%

Mtaliano Sarri alitua Stamford Bridge na staili yake ya soka la kupiga pasi nyingi. Kwa namna fulani soka hilo lilileta matokeo mazuri. Aliifikisha timu kwenye fainali ya Kombe la Ligi, huku akiwahi kushindwa kukubaliana na kipa Kepa Arrizabalaga. Mashabiki wa Chelsea hawakuwa wapenzi wa staili yake ya uchezaji na hata uteuzi wake wa kikosi na bila ya shaka hicho ndicho kitu kilichosukuma kuondolewa kwake kwenye timu hiyo na kurudi zake Italia alikokwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Juventus. Lakini, aliipa The Blues ubingwa wa Europa League.

10. Avram Grant (Septemba 2007 – Mei 2008)

Wastani wa ushindi: 66.7%

Huyu alikuwa rafiki yake Abramovich. Mwanzoni Grant aliajiriwa kama mkurugenzi wa ufundi wakati Mourinho alipokuwa kocha. Baada ya Mreno huyo kufutwa kazi, Grant alipewa majukumu ya kuwa kocha wa mpito. Katika msimu wake mmoja ambao alikaribia kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England, mambo yalitibuka akizidiwa na Manchester United. Mambo yalikwenda kombo Chelsea na kuondoshwa kisha alikwenda pia kuzinoa Portsmouth na West Ham United.

11. Luiz Felipe Scolari (Julai 2008 – Februari 2009)

Wastani wa ushindi: 55.6%

Mbrazili, Scolari alikuwa kocha wa kwanza mshindi wa Kombe la Dunia kuchukua mikoba ya kuinoa timu ya Ligi Kuu England. Mambo hayakuwa mambo na kila kitu kilikwenda hovyo. Scolari alikosea wapi? Mambo yake kwenye Ligi Kuu England yaligoma kwenda sawa, ambapo kocha huyo alijikuta akifutwa kazi kabla hata hajamaliza msimu. Kwa mechi alizoisimamia Chelsea alikuwa na wastani wa ushindi wa asilimia 55.6. Kufumba na kufumbua akajikuta hana kazi Stamford Bridge.

12. Andre Villas-Boas (Juni 2011 – Machi 2012)

Wastani wa ushindi: 47.5%

Kocha huyo Mreno alitua Chelsea baada ya kupata mafanikio makubwa akiwa kwenye kikosi cha FC Porto. Bilionea mmiliki wa Chelsea, Abramovich alidhani kwamba Villas-Boas atakuwa Mourinho mpya kwenye kikosi cha, lakini kila kitu kilikuwa tofauti kabisa.

Chelsea walizidi uwezo kocha na kuanza kujadili mbinu zake za ufundishaji. Ndiye kocha aliyekuwa na wastani mdogo zaidi wa ushindi kuliko makocha wote walioajiriwa na Abramovich, huku akiwa ghali pia kwa sababu The Blues ililazimika kulipa Pauni 13 milioni kuvunja mkataba wake FC Porto.