Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Simba aitisha Yanga, ataja dakika 15

BARKER Pict


KOCHA wa Simba, Steve Barker amesema wamejiandaa kwa tahadhari kukutana na Yanga akidai kwamba kwa sasa ni vigumu kutabiri ubora halisi wa watani wao kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika ndani ya kikosi hicho, huku akitaka kutumia dakika 15 kupata mabao.


Simba itakutana na Yanga kesho Jumatano katika mchezo wa Ngao ya Jamii  mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar, Unguja. 


Akizungumza na Mwanaspoti jana, Barker alisema maandalizi yao yamejikita zaidi katika kuangalia ubora wa Yanga watakaokutana nao kwenye mchezo huo, badala ya kutegemea historia au mwenendo wa timu hiyo katika michezo iliyopita.

Alisema kuwa, Yanga ya sasa ni tofauti na ile waliyoizoea msimu uliopita kutokana na mabadiliko ya wachezaji yaliyofanyika, jambo linalowafanya kuwa makini kabla ya mchezo huo.

“Tunakwenda kukutana na Yanga tukizingatia ubora wao, lakini kwa sasa hatujui vizuri ubora wa timu yao kwa sababu ni kama wana timu mpya. Hilo linatufanya tujiandae kwa namna tofauti,” alisema Barker.

Barker alisema pamoja na kutokuwa na picha kamili ya ubora wa Yanga ya sasa, Simba haitaki kumpa nafasi mpinzani wake kuingia kwenye mchezo huo kwa uhuru, badala yake wanataka kutumia uwezo wao kuuweka mchezo kwenye udhibiti wao mapema.

Alisema moja ya mipango yao ni kuhakikisha wanatumia nafasi watakazopata na kujaribu kupata bao mapema ili kupunguza presha ya mchezo.

“Tutaingia tukiwa na mpango wa kucheza vizuri na kujaribu kumaliza mechi ndani ya dakika 15. Tunajua tunakutana na mpinzani mkubwa na hatutegemei mchezo mwepesi,” alisema.

Pamoja na changamoto hiyo, Barker bado anaamini Simba ina ubora wa kutosha katika kikosi chake na kwamba wachezaji wake wana uwezo wa kuamua mchezo huo endapo watatekeleza vizuri mipango yake.

“Bado ninaamini Simba ina kikosi bora, lakini hilo halimaanishi kwamba tutapata mechi rahisi. Ni mchezo ambao tutahitaji umakini mkubwa kutoka mwanzo hadi mwisho,” alisema Barker.

Katika historia ya Ngao ya Jamii nchini Tanzania tangu ilipoanzishwa mwaka 2001, Simba SC ndio vinara wa kubeba taji hilo mara nyingi zaidi wakiwa wametwaa mara 10.