Prime
Makocha Simba, Yanga ‘wawazuga’ mashabiki
PAMOJA na mashabiki wa Simba na Yanga kutoridhishwa na vikosi vya timu zao baada ya kupoteza michezo ya matamasha yao, bado inaonekana kuwa makocha wameficha ubora wao kwa wapinzani, wacheza Pool Table wanasema ‘wameficha white’.
Simba ilifunga tamasha lake la Simba Day Jumamosi ya wiki iliyopita na kuambulia kichapo cha bao 1-0 toka kwa Polisi Kenya, bao lilofungwa mwishoni kabisa mwa mchezo huo, hata hivyo, wakati mashabiki wa Yanga wakifurahia kilichowapata wenzao, kesho yake, yaani juzi Jumapili timu hiyo nayo iliingia uwanjani dhidi ya Les Aigles du Congo na kulala kwa mabao 2-1.
Tofauti na jinsi ilivyokuwa kwa upande wa Simba ambayo ilishacheza michuano ya Kagame Cup na kuondolewa kwenye hatua ya makundi, Yanga huu ndiyo ulikuwa mchezo wao wa kwanza msimu huu wanaonekana mbele ya mashabiki baada ya kufanya usajili wa zaidi ya wachezaji kumi wapya kwenye kikosi hicho.
Pamoja na vikosi vyote mashabiki wake kuonekana kuwa wanataka ushindi zaidi baada ya kuburudika na mambo mbalimbali, kwa upande wa makocha wa timu hizo mambo yalikuwa tofauti huku kila mmoja akiwa anawaza zaidi mchezo wa Ngao ya Jamii kesho kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Mchezo huu utakuwa na ushindani mkali kutokana na jinsi ambavyo timu hizo zimekuwa zikionyeshana umwamba kwenye michezo ya msimu uliopita.
Yanga ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara siku ya mwisho kabisa, ukiwa ni ubingwa wake wa tano mfululizo, huku Simba ikifanikiwa kuchukua ubingwa wa Shirikisho wa CRDB, lakini pia kumbuka kuwa Yanga ilianza kwa kutwaa Ngao na Simba wakachukua ubingwa wa Muungano kupokezana kwa kila mmoja kuchukua ubingwa ni jambo lingine ambalo linaleta presha kubwa kwenye mchezo huu.
Katika michezo yote miwili, kuanzia aina ya vikosi vilivyoanza kwenye mechi hizo bado picha halisi ilionekana kuwa makocha wote wanawaza zaidi kuhusu mchezo wa Dabi badala ya mechi hizo ambazo ni maalumu kwa ajili ya kujipima nguvu kutokana na kuwa na siku chache tu za kujiandaa.
Kitendo cha kocha wa Simba Steve Barker kuanza na kikosi ambacho hayumo Ibrahim Jabaar, Clatous Chama na Keletso Makgalwa ni ishara kuwa mawazo yake bado yalikuwa kwenye eneo la kutazama kikosi chake kinacheza, kimejipangaje badala ya kutafuta matokeo na ndiyo maana ukitazama jinsi mpangilio wa timu ulivyokuwa ulifika wakati akawa anataka kumuona kila mchezaji anacheza, badala ya kuongeza ubunifu kwenye timu ilikuhakikisha kuwa wanapata ushindi.
Mbali na wachezaji pia timu ilionekana kutengeneza mashabiki yake taratibu, huku wachezaji wakiepuka sana kugongana na wapinzani wao kwa kuwa tayari mawazo ya kesho Jumatano yalikuwa kichwani kwao.
“Tumemaliza mchezo huu, haya yalikuwa bado ni maandalizi ya msimu ni kweli tumepoteza lakini tunaamini kuwa kuna jambo ambalo tumelichukua kwenye mchezo huu na tutakkwenda kuyafanyia kazi kwenye mchezo wa Dabi, kila mchezaji amecheza vizuri,’’ amesema Barker baada ya mchezo huo kumalizika.
Kwa upande wa Yanga shida siyo kikosi kilichoanza, lakini kitendo cha kuanza bila kipa wake namba moja Djigui Diarra na mastaa wengine wa kikosi cha kwanza ni picha halisi kuwa kocha wa timu hiyo hakuwa anawaza zaidi ushindi kwenye mchezo huo kama mashabiki.
Kwa kocha aliyetaka kuonyesha silaha zake ilikuwa ngumu kwake kuwaondoa wachezaji asilimia 90 baada ya kipindi cha kwanza kumalizika, hii inaonyesha pia kwa Yanga benchi la ufundi lilikuwa linawaza kuhusu mchezo ujao wa Dabi, lakini pia walitaka kuendelea kuwaangalia mastaa wao kama wameshaingia kwenye mfumo wa jinsi timu inavyotakiwa kucheza.
“Nafikiri kesho tunakwenda Zanzibar kwa ajili ya mchezo wetu wa Ngao ya Jamii, tumepoteza mchezo huu lakini bado tuna mambo mengi ya kujifunza kabla ya mechi ya Dabi baadhi ya makosa tutarekebisha mazoezini kabla ya mechi ijayo ‘’, amesema kocha wa Yanga Manqoba Mngqithi.
HIZI NI MALI
Pamoja na mchezo kuwa wa kirafiki zaidi, lakini kuna wachezaji wapya wa timu zote mbili walionyesha ubora wa tofauti na wezao, mshambuliaji wa Simba, Keletso Makgalwa alionyesha uwezo wa juu wa kupokea mipira na kukimbia kuingia kwenye eneo la mpinzani.
Ni mmoja kati ya wachezaji hatari akiwa na mali mguuni kwa kuwa ni rahisi kwake kumfanya mpinzani amfanyie madhambi kutokana na kasi na ubunifu wake, lakini pia anaonekana kuwa fundi sana wa kupiga mipira ya faulo pamoja na kwamba mmoja aliopiga ulitoka nje.
Mchezaji mwingine kwa upande wa Simba ambaye hahitaji mechi ya pia kuuona ubora wake ni Ibraheem Olalekan Jabaar alionyesha uwezo wa juu wa kupiga pasi kukaa eneo sahihi, lakini ni aina ya wachezaji wanaocheza huku wanaburudisha muda wote wa mchezo, hata hivyo anaonekana tayari ameshazoeana na wenzake kikosini.
Kwa upande wa Yanga, pamoja na wengine kuonyesha ubora lakini Erick Mwijage alionekana kuwavutia mashabiki kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi, kupokonya mipira lakini ubora wa kuliendea lango la wapinzani bila kuwa na presha yoyote ni jambo lingine bora.
Kwa upande wa mshambuliaji Peter Shalulile, ameendeleza yale ambayo mashabiki wengi walikuwa wanayatarajia kutoka kwake, aina ya mkwaju wa penalti uliopatikana, ubora wake wa kuwapunguza mabeki na kucheza kwa ushirikiano na wenzake bila kujali jina lake ni jambo lingine linaloonyesha kuwa ni mchezaji mkubwa na yupo tayari kuingia uwanjani muda wowote.