Mo Salah aitwa mahakamani
Muktasari:
- Mahakama ya Kiraia ya Cairo imepanga Salah kufika mbele ya Mahakama ya Mwanzo ya New Cairo katika kesi namba 7826/2025, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kukusanya ushahidi katika kesi hiyo ya madai ya kiraia.
CAIRO, MISRI: Nyota wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya Misri, Mohamed Salah, ameagizwa kufika binafsi mahakamani mwezi Septemba kufuatia mzozo wa madai ya malipo kati yake na aliyekuwa wakili wake.
Mahakama ya Kiraia ya Cairo imepanga Salah kufika mbele ya Mahakama ya Mwanzo ya New Cairo katika kesi namba 7826/2025, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kukusanya ushahidi katika kesi hiyo ya madai ya kiraia.
Mahakama hiyo pia imewaagiza makarani wake kumjulisha rasmi Salah kuhusu wito huo, baada ya mchezaji huyo kutokuwepo wakati uamuzi wa awali ulipotolewa.
Katika hatua hiyo, Salah anatakiwa kutoa kiapo cha kukanusha madai kwamba wakili Amr Faragallah Morsi alifanya kazi za kisheria na kiutawala zinazodaiwa katika kesi hiyo.
Kwa mujibu wa taratibu za kiraia nchini Misri, kiapo hicho kinachojulikana kama decisive oath kinampa mmoja wa wahusika nafasi ya kumtaka mwingine kuapa kuhusu ukweli wa jambo linalobishaniwa.
Salah anatakiwa kutoa kiapo hicho mwenyewe na hawezi kumtuma mwakilishi wake wa kisheria kufanya hivyo kwa niaba yake.
Chama cha Wanasheria nchini Misri kimeeleza kuwa kuchukua au kukataa kiapo hicho kunaweza kuamua suala linalobishaniwa.
Iwapo Salah ataapa kwamba wakili huyo hakufanya kazi zinazodaiwa, madai hayo yanaweza kuamuliwa kwa upande wake. Aidha, kutofika mahakamani au kukataa kuapa bila sababu inayokubalika kisheria kunaweza kutafsiriwa kama kukataa kiapo na huenda ikaathiri uamuzi wa kesi.
Hata hivyo, kwa sasa hakuna hukumu ya mwisho iliyotolewa kwamba Salah anadaiwa fedha hizo, wala suala hilo si kesi ya jinai.
Mahakama pia imeahirisha uamuzi kuhusu gharama za kesi na ada za mashauri hadi itakapotoa hukumu ya mwisho.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Morsi Septemba 11, 2025, akidai malipo kwa huduma za kisheria, taratibu za kiutawala na ushauri aliodai kumfanyia Salah mwaka 2012.