Fernandes akubali mavitu ya Van de Beek

Fernandes akubali mavitu ya Van de Beek

Muktasari:

KIUNGO fundi wa mpira, Bruno Fernandes amesema tena kwa kusisitiza anaendana kimchezo na Donny van de Beek baada ya kuisaidia Manchester United kupindua meza dhidi ya Southampton kwenye Ligi Kuu England uwanjani St. Mary’s.

MANCHESTER, ENGLAND. KIUNGO fundi wa mpira, Bruno Fernandes amesema tena kwa kusisitiza anaendana kimchezo na Donny van de Beek baada ya kuisaidia Manchester United kupindua meza dhidi ya Southampton kwenye Ligi Kuu England uwanjani St. Mary’s.

Staa huyo mpya wa Man United, Van de Beek alikuwa kwenye kiwango bora kabisa wakati alipoanzishwa kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Fernandes alichukua nafasi ya kumsifu Mdachi huyo baada ya mechi hiyo, akijaribu kujibu hoja zilizokuwa zikiibuka wawili hao wahawezi kucheza pamoja Paul Pogba asipokuwapo. Hivyo akizungumza baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Saints, Fernandes alisema: “Kila kiungo kweye timu yetu ana kiwango. Donny ana kiwango kikubwa sana. Tunaweza kucheza pamoja kama ilivyo kwa wachezaji wengine.

“Kila mtu ana kiwango cha kucheza pamoja na tunafahamiana vyema. Tunaweza kucheza tukiwa watatu ya kucheza tukiwa wanne. Donny alicheza vizuri sana, lakini Fred na Nemanja (Matic) walikuwa muhimu sana kwenye timu.”

Katika mchezo huo, Man United ilitanguliwa mabao 2-0 hadi kufikia mapumziko, lakini Man United ilichomoa kipindi cha pili, ikifunga mara tatu, Fernandes mara moja na Edinson Cavani alifunga mara mbili kukifanya kikosi hicho cha Ole Gunnar Solskjaer kushinda kibabe.