Chawinga waipeleka Malawi fainali WAFCON
Muktasari:
- Malawi ambayo ni mara ya kwanza kushiriki mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 1991, hadi sasa inaendelea kuandika rekodi.
TIMU ya Taifa ya Malawi, imetinga hatua ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) baada ya kuitandika Algeria mabao 3-1 kwenye nusu fainali iliyochezwa leo usiku Agosti 12, 2026 jijini Rabat, Morocco.
Malawi ambayo ni mara ya kwanza kushiriki mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 1991, hadi sasa inaendelea kuandika rekodi.
Kama ilivyo kawaida yao dada wawili wa Malawi, Tabitha Chawinga na Temwa Chawinga, wameendelea kuwa nyota wa WAFCON 2026 baada ya kuisaidia timu hiyo kutinga fainali kwa kuhusika na mabao yote ya ushindi.
Mchezo huo ulikuwa wa kasi na wenye matukio mengi, huku timu zote zikishambuliana kwa zamu. Hata hivyo, Malawi ilipata faida baada ya beki wa Algeria, Morgane Belkhiter, kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumzuia Tabitha Chawinga akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, baada ya mwamuzi kupitia VAR.
Dakika ya 33, Tabitha aliiandikia bao la kuongoza Malawi kwa kufunga mpira wa juu akiwa hewani uliogonga mwamba kabla ya kudunda chini na kuvuka mstari wa goli. Bao hilo liliipa Malawi uongozi na kuifanya Algeria kuanza kuongeza presha.
Malawi iliendelea kuwashangaza wapinzani wao na kuongeza bao la pili dakika za nyongeza mwa kipindi cha kwanza kupitia Temwa Chawinga, lakini furaha hiyo ilifuatiwa na pigo baada ya Rose Kadzere kuonyeshwa kadi nyekundu kabla ya mapumziko.
Algeria ilirejea kipindi cha pili ikiwa na matumaini ya kubadilisha matokeo na juhudi zao zilizaa matunda baada ya Ikram Adjabi kufunga na kupunguza tofauti. Hata hivyo, Tabitha Chawinga alizima matumaini hayo kwa kufunga bao lake la pili na la tatu kwa Malawi, na kuweka matokeo kuwa 3-1.
Ushindi huo umeifanya Malawi maarufu The Scorchers ifikie fainali ya WAFCON kwa mara ya kwanza katika historia, ikiwa ni sehemu ya safari ambayo imekuwa gumzo tangu mashindano yalipoanza.
The Scorchers imekuwa ikionyesha uwezo mkubwa licha ya kutokuwa miongoni mwa timu zilizotajwa kupewa nafasi kubwa kabla ya mashindano.
Sasa Malawi itakutana na mshindi kati ya wenyeji Morocco na Cameroon katika fainali itakayochezwa Jumapili, huku ikiwa na nafasi ya kuandika historia nyingine kwa kuwa taifa la nne kutwaa ubingwa wa WAFCON ikiwa itashinda mchezo huo.
Mafanikio ya Malawi katika mashindano hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na dada hao wawili, Tabitha na Temwa, ambao wamekuwa na kiwango bora na kuwa hatari kwa wapinzani.