Napoli yaichokonoa Chelsea ikimtaka Benoit Badiashile
Muktasari:
- Chelsea imefanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi msimu huu wa kiangazi, ambapo Trevoh Chalobah amejiunga na Como, huku Maxence Lacroix akijiunga na Chelsea akitokea Crystal Palace.
NAPOLI imeanza mazungumzo ya kumsajili beki wa kati wa Chelsea, Benoit Badiashile, ambapo mazungumzo yanaendelea kati ya klabu hizo pamoja na wawakilishi wa mchezaji huyo, huku pande zote zikijaribu kufikia makubaliano ya mwisho.
Chelsea imefanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi msimu huu wa kiangazi, ambapo Trevoh Chalobah amejiunga na Como, huku Maxence Lacroix akijiunga na Chelsea akitokea Crystal Palace.
Levi Colwill, Tosin, Wesley Fofana na Lacroix wanatarajiwa kuwa mabeki wa kwanza wa kati wa Chelsea msimu huu. Hata hivyo, bado haijafahamika iwapo Axel Disasi, Mamadou Sarr na Aaron Anselmino wataondoka Stamford Bridge.
Kinachoelezwa ni kwamba kuwapo kwa mastaa wengi katika kikosi hicho kumewaibua baadhi kutaka kuondoka.
Tijjani Reijnders
MACHESTER City inafahamu kuhusu lengo la Nottingham Forest kumsajili kiungo wake wa kimataifa wa Uholanzi, Tijjani Reijnders, mwenye umri wa miaka 28. Reijnders alisajiliwa na City kutoka AC Milan msimu uliopita kwa ada ya Pauni 46 milioni. Hata hivyo timu hiyo bado haijafikia uamuazi wa nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi
Harry Kane
BARCELONA na Tottenham Hotspur zote zimefanya mawasiliano hivi karibuni na Bayern Munich kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa England, Harry Kane, mwenye umri wa miaka 33, katika dirisha hili la uhamisho wa kiangazi. Hata hivyo, Bayern imeshaeleza kwamba haitamuachia straika huyo msimu huu.
Ayyoub Bouaddi
MANCHESTER City iko mbioni kumsajili Ayyoub Bouaddi mwenye umri wa miaka 18 kutoka Lille ambayo inamthamini kiungo huyo wa kimataifa wa Morocco kwa Pauni 85 milioni. Mchezaji huyo tayari ameshakubaliana na Man City katika ofa binafsi na yupo tayari kutua jijini Manchester.
Bradley Barcola
BRADLEY Barcola, mwenye umri wa miaka 23, ametoa ishara ya kukubali kujiunga na Liverpool, licha ya Arsenal kufanya jaribio la dakika za mwisho kumsajili mshambuliaji huyo wa PSG na Ufaransa, ambaye thamani yake inakadiriwa kuwa karibu Pauni 130 milioni.
Gabriel Martinelli
AS Roma imefanya mazungumzo ya awali na wawakilishi wa Gabriel Martinelli, huku ikichunguza uwezekano wa kumsajili winga huyo wa Arsenal na timu ya taifa ya Brazil mwenye umri wa miaka 25. Martinelli bado anapenda kuitumikia Arsenal msimu ujao, lakini lolote linaweza kutokea.
Romelu Lukaku
FENERBAHCE inadaiwa kufikia makubaliano na Napoli ya kumsajili mshambuliaji Romelu Lukaku. Mkataba wake una thamani ya Pauni 5.12 milioni pamoja na nyongeza kulingana na mafanikio, huku Lukaku akiwa tayari kusaini dili na klabu hiyo ya Uturuki. Kuondoka kwa Lukaku kunaweza kuipa Napoli nafasi ya kumsajili mshambuliaji wa Arsenal, Gabriel Jesus.
Alessandro Bastoni
BEKI wa Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, Alessandro Bastoni, mwenye umri wa miaka 27, pamoja na kiungo wa Crystal Palace na England, Adam Wharton, mwenye umri wa miaka 22, bado wanavutiwa na Real Madrid ambayo inalenga kufanya usajili mwingine katika dirisha hili la kiangazi.
Martin Zubimendi
REAL Madrid inavutiwa kumsajili kiungo wa kimataiafa wa Hispania aliyeshinda Kombe la Dunia 2026, Martin Zubimendi, mwenye umri wa miaka 25, kutoka Arsenal. Kwa sasa pande hizo zinaendelea na mazungumzo ili kufikia muafaka.
Joao Palhinha
JOAO Palhinha yupo tayari kuhamia Aston Villa kwa mkopo kutoka Bayern Munich, kwa mujibu wa The Sun, ambapo kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 alicheza kwa mkopo Tottenham Hotspur msimu uliopita, huku Newcastle United pia ikiripotiwa kuwa inamtaka.