Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gor Mahia yatuma salamu nzito Kagame Cup ikiifumua APR mabao 5-0

GOR MAHIA Pict

Muktasari:

  • Mabao ya nahodha Michael Kibwage, Patrick Esombe, Paul Okoth, Lesley Otieno na Ebenezer Assifuah yaliihakikishia timu hiyo inayofundishwa na kocha Charles Akonnor ushindi mkubwa ulioiwezesha kuongoza Kundi A na kuongeza matumaini ya kutinga moja kwa moja hatua ya nusu fainali.

MABINGWA wa Kenya, Gor Mahia, wameanza kwa kishindo kampeni ya Kombe la CECAFA Kagame 2026 baada ya kuwachapa mabingwa wa Rwanda, APR FC, mabao 5-0 katika mchezo wa Kundi A ulioonekana kuwa wa upande mmoja.

Mabao ya nahodha Michael Kibwage, Patrick Esombe, Paul Okoth, Lesley Otieno na Ebenezer Assifuah yaliihakikishia timu hiyo inayofundishwa na kocha Charles Akonnor ushindi mkubwa ulioiwezesha kuongoza Kundi A na kuongeza matumaini ya kutinga moja kwa moja hatua ya nusu fainali.

Ikiwa inawania kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa Kombe la Kagame baada ya miaka 41, Gor Mahia iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na dhamira ya kuanza vizuri.

Kwa upande wa APR, ambayo ilimaliza nafasi ya pili katika toleo lililopita, nayo ilikuwa na nia ya kuweka alama mapema katika harakati zake za kutwaa ubingwa wa nne wa mashindano hayo ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku timu zote zikionyesha nia ya kushambulia tangu kipyenga cha kwanza.

APR ilipata nafasi ya kwanza ya maana dakika ya 10 pale Raouf Memel Dao alipounganisha pasi ya Cheick Djibril Ouattara, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango.

Dakika tano baadaye, Gor Mahia ilijibu kupitia mchezaji wake mpya Paul Okoth, aliyekimbilia pasi nzuri ya David Odhiambo, lakini alishindwa kulenga lango.

Baadaye Patrick Esombe aliisumbua safu ya ulinzi ya APR baada ya kuupata mpira uliotoka nje kidogo ya eneo la hatari, lakini kipa Ernan Siluane aliokoa kwa ustadi na kuizuia Gor Mahia kufunga.

APR  ilikaribia kufunga dakika ya 30 wakati William Togui Mel alipopiga kichwa kufuatia krosi ya Kouadiokan Amani, lakini mpira ulipita juu ya lango.

Hatimaye Gor Mahia ilivunja ukimya dakika ya 33. Mohamed Siraj alipiga kona iliyomkuta nahodha Michael Kibwage, ambaye aliruka juu ya mabeki na kupiga kichwa cha nguvu na kuandika bao la kwanza.

Dakika tatu baadaye, Gor Mahia iliongeza bao la pili kupitia Patrick Esombe, aliyepiga shuti kali kutoka nje ya eneo la hatari lililomshinda kipa Siluane.

Kabla ya mapumziko, Alpha Onyango alikaribia kuifungia Gor Mahia bao la tatu baada ya kutengenezewa nafasi na Odhiambo, lakini shuti lake lilipita kidogo pembeni mwa lango.

Kipindi cha pili, Gor Mahia iliendelea ilipoishia na kuongeza bao la tatu dakika ya 63. Enock Machaka alitoa pasi nzuri iliyomkuta Paul Okoth, ambaye alitulia na kuupitisha mpira pembeni mwa kipa aliyekuwa ametoka golini, akifunga bao lake la kwanza akiwa na jezi ya Gor Mahia.

APR ilijaribu kurejea mchezoni, huku Yunusu Nshimiyimana akipiga kichwa kilichotoka nje kufuatia krosi ya Amadou Zon dakika 20 kabla ya mchezo kumalizika, lakini ilishindwa kabisa kuuvunja ukuta wa safu ya ulinzi ya Gor Mahia.

Dakika ya 80, Gor Mahia ilipata bao la nne baada ya Shariff Musa kufanya kazi nzuri ya kuwapita mabeki kabla ya kutoa pasi ya mwisho iliyomkuta Lesley Otieno, ambaye hakufanya makosa na kuuweka mpira wavuni akiwa karibu na lango.

Mshambuliaji aliyeingia kipindi cha pili, Ebenezer Assifuah, alihitimisha karamu ya mabao mwishoni mwa mchezo baada ya kuuwahi mpira uliokuwa ndani ya eneo la penalti na kuutumbukiza wavuni, akiifungia Gor Mahia bao la tano na kuhitimisha ushindi wa kishindo katika mchezo wao wa ufunguzi.

Ushindi huo mkubwa umeifanya Gor Mahia kukwea kileleni mwa Kundi A, mbele ya Vipers SC, ambayo iliifunga Garde Républicaine mabao 3-0 katika mchezo mwingine wa mapema wa kundi hilo.

Koch wa Gor Mahia, Charles Akonnor ameanza vizuri na vijana wake katika harakati za kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame 2026.