Simba, Singida Black Stars zishindwe zenyewe
Muktasari:
- Michuano hiyo itafanyika kuanzia Julai 24 hadi Agosti 7 mwaka huu katika viwanja vya Amahoro na Kigali Pele jijini Kigali nchini Rwanda.
SIMBA na Singida Black Stars zitakuwa na kazi moja tu ya kufanya katika michuano ya Kombe la CECAFA Kagame Cup 2026 baada ya Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) kutangaza kila kitu kipo tayari kwa ajili ya kuandaa mashindano hayo makubwa ya klabu za Afrika Mashariki na Kati.
Michuano hiyo itafanyika kuanzia Julai 24 hadi Agosti 7 mwaka huu katika viwanja vya Amahoro na Kigali Pele jijini Kigali nchini Rwanda.
Makundi yameshapangwa ambapo kundi A lina APR ya Rwanda, Vipers SC (Uganda), Gor Mahia FC (Kenya) na Garde Republicaine (Djibouti).
Kundi B, lina Simba na Singinda Black Stars zote za Tanzania, Jamus (Sudan Kusini) na Mogadishu City Club (Somalia). Kundi C lina Rayon Sports ya Rwanda, Tusker (Kenya) na KVZ (Zanzibar).
Katibu Mkuu wa FERWAFA, Bonnie Mugabe, amesemamaandalizi yote yamekamilika na Rwanda iko tayari kuandaa moja ya mashindano bora zaidi ya Kagame Cup kuwahi kushuhudiwa.
Mugabe amesemauzoefu walioupata baada ya kufanikiwa kuandaa michuano ya FIFA Series mapema mwaka huu umewapa imani kuwa wana uwezo wa kutoa mashindano yenye viwango vya kimataifa, kuanzia viwanja, usalama, huduma kwa timu hadi mazingira kwa mashabiki.
“Tunatarajia wadau wengi kujitokeza kuunga mkono mashindano haya kwa sababu tunataka yawe na mafanikio makubwa,” amesemaMugabe.
Alifafanua kuwa kulikuwa na mpango wa kushirikisha baadhi ya klabu kutoka Tunisia na Libya kama wageni maalumu, lakini baadaye zilijiondoa kutokana na changamoto mbalimbali zilizozikabili kabla ya kuanza kwa mashindano.
Hata hivyo, Mugabe amesemaFERWAFA ina matumaini ya kuendelea kuwa mwenyeji wa Kagame Cup kwa miaka mitatu mfululizo, jambo litakaloifanya Rwanda kuendelea kuwa kitovu cha soka la klabu katika ukanda wa CECAFA.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, Jean Sseninde, aliipongeza FERWAFA kwa kujitolea kuandaa mashindano hayo, akisema hatua hiyo itaongeza hadhi na ushindani wa michuano hiyo.
Sseninde amesemaCECAFA ina mpango wa kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki katika matoleo yajayo, ikiwemo kuendelea kualika klabu kutoka maeneo mengine ya Afrika ili kuongeza ubora na ushindani.
Mbali na heshima ya kutwaa ubingwa, timu zitakazofanya vizuri pia zitajizolea fedha taslimu. Bingwa wa Kagame Cup 2026 ataondoka na Dola 30,000 (zaidi ya Sh78 milioni), mshindi wa pili Dola 20,000 (zaidi ya Sh52 milioni), huku ya tatu ikipewa Dola 10,000 (zaidi ya Sh26 milioni).
Fedha hizo zimeendelea kutolewa kupitia udhamini wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye amekuwa mdhamini mkuu wa mashindano hayo tangu mwaka 2002 kwa lengo la kuendeleza maendeleo ya soka la klabu katika ukanda wa CECAFA.
Kwa Simba na Singida Black Stars, mashindano hayo yatakuwa fursa ya kupima ubora wao dhidi ya baadhi ya klabu bora za ukanda huo, huku wakisaka kuirejesha Tanzania kwenye kilele cha soka la CECAFA baada ya ushindani mkubwa unaotarajiwa mwaka huu.