Prime
Rushine aionya Simba CAFCL
LICHA ya Simba kuondoka Malawi ikiwa na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mighty Wanderers FC, nahodha wa kikosi hicho, Rushine De Reuck, amewaonya wachezaji wenzake kutobweteka na matokeo hayo, huku rekodi bora ya uwanja ikiwabeba.
Simba ilipata ushindi huo kufuatia bao la Anicent Oura katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, matokeo ambayo sasa yanaipa faida kabla ya mchezo wa marudiano utakaofanyika wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba inahitaji kulinda faida yake ya bao moja katika mchezo wa nyumbani, lakini Rushine amesisitiza kuwa hilo halipaswi kuwafanya waanze kufikiria kwamba tayari wamefuzu.
Akizungumza na Mwanaspoti beki huyo raia wa Afrika Kusini amesema kikosi hicho kinapaswa kuingia kwenye mchezo wa pili kikiwa na kiu ileile ya ushindi na kuhakikisha kinamaliza kazi mbele ya mashabiki wake.
“Tumepata ushindi mzuri ugenini, lakini bado kuna dakika 90 nyingine za kucheza. Hatupaswi kufikiria kwamba kazi imekwisha kwa sababu tu tumeshinda bao 1-0,” amesema Rushine na kuongeza;
“Wapinzani wetu walionyesha ushindani mkubwa. Walipambana vizuri na walifanya mchezo kuwa mgumu kwetu. Tunapaswa kuwaheshimu na kujiandaa vizuri kwa mchezo wa pili, hatupaswi kufanya makosa ya kizembe, tunatakiwa kutumia nafasi chache tutakazopata, uzembe kidogo tu unaweza kumaliza ndoto zetu.”
Ushindi wa Malawi pia umeipa Simba nafasi ya kuingia kwenye mchezo wa pili ikiwa na utulivu, kwani kwa sasa presha kubwa ya kutafuta matokeo itakuwa kwa Mighty Wanderers ambao wanahitaji kubadili matokeo ili kusonga mbele.
Hata hivyo, Simba inapaswa kuwa makini na hilo, kwani timu hiyo ya Malawi inaweza kutumia presha hiyo kama silaha ya kushambulia tangu mwanzo wa mchezo huku ikitafuta bao litakalorejesha mzani kuwa sawa. Kwa upande wa Simba, safu ya ulinzi ikiongozwa na Rushine itakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha hairuhusu bao la mapema, wakati safu ya ushambuliaji ikitakiwa kutumia nafasi zitakazopatikana ili kuondoa kabisa presha ya mchezo.
“Tunawaheshimu Mighty Wanderers, lakini tunajiamini pia. Tunahitaji kuwa makini, kucheza kama timu na kupambana kwa dakika zote 90. Hatuwezi kubweteka kwa sababu tumeshinda mchezo wa kwanza,” amesema.
REKODI ZA UHURU
Uwanja wa Uhuru maarufu kama shamba la bibi una kumbukumbu nzuri za Simba katika michuano ya kimataifa huku moja ya ushindi unaokumbukwa ikiwa ni ule wa mwaka 1979 dhidi ya Mufulira Wanderers ya Zambia katika mashindano ya African Champions Cup.
Simba iliichapa Mufulira mabao 4-0, ushindi ulioweka alama kubwa katika historia ya klabu hiyo kwenye michuano ya kimataifa.
Miaka kadhaa baadaye, Simba iliendeleza rekodi yake nzuri kwenye uwanja huo ilipowakaribisha Awassa Kenema ya Ethiopia katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2008. Wekundu wa Msimbazi walitawala mchezo huo na kushinda 3-0, kabla ya kwenda Ethiopia na kutoka sare ya 1-1, hivyo kusonga mbele katika michuano hiyo. Mwaka 2011, Simba ilirejea Uhuru katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kukutana na Élan Club ya Comoros, ambapo ilionyesha tena nguvu yake mbele ya mashabiki wake kwa kushinda kwa mabao 4-2.
Kwa maana hiyo, kabla ya mchezo wa marudiano dhidi ya Wanderers, historia ya Simba kwenye Uhuru inatoa kumbukumbu nzuri.