Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Singida Black Stars, Simba mzigoni Kombe la Kagame

KAGAME Pict

Muktasari:

  • Kwa upande wa Simba, wataanza kampeni zao dhidi ya Mogadishu City ya Somalia kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 12 jioni, huku wakisaka ushindi utakaowaongezea morali katika harakati za kurejesha ubingwa walioutwaa mara ya mwisho mwaka 2002.

WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika Kombe la Kagame 2026, Singida Black Stars na Simba, leo Jumamosi Julai 25, 2026 wanashuka dimbani kuanza kampeni zao katika kuwania ubingwa wa michuano hiyo iliyoanza kuchezwa Ijumaa ya Julai 24, 2026 mjini Kigali nchini Rwanda, huku kila mmoja akiwa na malengo makubwa ya kuanza kwa ushindi.

Singida Black Stars, ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, watafungua ratiba yao kwa kuivaa Jamus FC ya Sudan Kusini wakilenga kuanza vyema safari ya kutetea taji walilolitwaa mwaka jana. Mechi hiyo imepangwa kuchezwa saa 9 alasiri kwenye Uwanja wa Kigali Pele.

Kwa upande wa Simba, wataanza kampeni zao dhidi ya Mogadishu City ya Somalia kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 12 jioni, huku wakisaka ushindi utakaowaongezea morali katika harakati za kurejesha ubingwa walioutwaa mara ya mwisho mwaka 2002.

Simba inaingia kwenye michuano hiyo ikiwa na rekodi ya kuwa klabu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya CECAFA Kagame Cup, ikitwaa ubingwa mara sita (1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002). Ushindi wa mwaka huu utaifanya ifikishe mataji saba na kuendelea kuimarisha rekodi yake katika mashindano hayo.

KAGA 01

Mbali na kuwania matokeo mazuri kwa heshima ya klabu zao, Simba na Singida ambao ni mabingwa watetezi pia wanabeba matumaini ya kuiwakilisha vyema Tanzania Bara katika mashindano hayo yanayoshirikisha timu 12 kutoka nchi tisa za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku fainali ikitarajiwa kuchezwa Agosti 7.

Wakati huohuo, Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Paulos Weldehaimanot Andemariam, amesema Kombe la CECAFA Kagame 2026 litakuwa bora zaidi kuwahi kuandaliwa katika ukanda huo kutokana na maandalizi makubwa yaliyofanywa na Rwanda.

KAGA 02

Akizungumza katika mkutano rasmi na waandishi wa habari uliofanyika Uwanja wa Amahoro, Kigali, kuelekea uzinduzi wa michuano hiyo uliofanyika Julai 24, 2026, Andemariam aliipongeza Serikali ya Rwanda chini ya Rais Paul Kagame pamoja na Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) kwa maandalizi yake na kukubali tena kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

"Ninaishukuru Serikali ya Rwanda chini ya Rais Paul Kagame pamoja na uongozi wa FERWAFA kwa kuhakikisha mashindano haya yanarejea nchini Rwanda kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019. Tuna imani haya yatakuwa mashindano bora zaidi ya CECAFA Kagame Cup," amesema Andemariam.

KAGA 03

Kiongozi huyo pia alifichua kuwa Rwanda tayari imeonyesha nia ya kuandaa michuano mingine mitatu ya mashindano ya CECAFA, akieleza kuwa nchi hiyo imeendelea kuthibitisha uwezo wake kupitia miundombinu bora ya michezo na uzoefu wa kuandaa matukio makubwa ya kimataifa.

Amesema mbali na CECAFA Kagame Cup, Rwanda pia itakuwa mwenyeji wa mashindano mengine matatu ya kanda yaliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwaka huu, jambo linaloonyesha imani kubwa ambayo imejengwa kwa taifa hilo.

Aidha, Andemariam amesema CECAFA inaendelea kuweka mikakati ya kuboresha thamani ya mashindano hayo ili yavutie wadhamini zaidi na hata kushirikisha timu kutoka kanda nyingine za Afrika katika siku zijazo.

Michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026 imeanza Julai 24, 2026 kwa mechi za Kundi A ambapo Vipers SC ya Uganda ilicheza dhidi ya Garde Republicaine FC ya Djibouti huku wenyeji APR FC wakikabiliana na Gor Mahia FC ya Kenya katika Uwanja wa Amahoro.

KAGA 04

Mashindano ya mwaka huu yanashirikisha timu 12 kutoka nchi tisa za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na yanatarajiwa kumalizika Agosti 7 kwa mchezo wa fainali.

Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa dola 30,000 za Marekani (zaidi ya Sh 81 milioni), mshindi wa pili dola 20,000 (zaidi ya Sh54 milioni), huku timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu ikiondoka na dola 10,000 (zaidi ya Sh27 milioni).

Tangu mwaka 2002, Rais wa Rwanda Paul Kagame amekuwa akichangia fedha za zawadi za mashindano hayo, hatua iliyochangia kuyapa hadhi na kuendelea kuvutia ushindani mkubwa ndani ya ukanda wa CECAFA.

Kundi A la michuano hiyo linaundwa na timu za APR (Rwanda), Vipers (Uganda), Gor Mahia (Kenya) na Garde Republicaine (Djibouti).

Kundi B ni Singida Black Stars (Tanzania), Simba (Tanzania), Jamus (Sudan Kusini) na Mogadishu City (Somalia), huku Kundi C ni Al Hilal (Sudan), Rayon Sports (Rwanda), Tusker (Kenya) na KVZ (Zanzibar).