Straika Gor Mahia aigawa Yanga

Muktasari:

Lakini buana kwa sasa utata mzito ukaibuka juu ya kipi kifanyike kwa mshambuliaji huyo mrefu kutokana na kuelezwa kuwa aliletwa kwa ushawishi wa bosi mmoja wa juu wa Yanga - tena kwa barua ambayo Mwanaspoti limeiona akiandikiwa kutoka ofisi kuu ya sekretarieti ya klabu hiyo akitakiwa kufika nchini kwa lengo la kusajiliwa.

JUZI kati buana, Yanga si ilishusha straika mmoja mwenye mwili jumba akitokea Gor Mahia ya Kenya ili kumsainisha mkataba kupitia dirisha dogo la usajili linaloendelea. Umbo na wasifu wake uliotajwa wa kutupia nyavuni kwa mipira ya vichwa na ile ya miguuni, viliwafanya mashabiki wa Yanga kupagawa kinoma walipomuona Uwanja wa Uhuru walipokuwa wakiicharaza Iringa United kwenye mechi ya Kombe la FA na kuwatambia wenzao wa Simba wakisema, “Subirini Januari 4, mtamkoma.”

Hata hivyo unaambiwa kuna filamu moja nzito inaendelea juu ya straika huyo, Yikpe Gnamain, raia wa Ivory Coast ikiwa haijulikani hatima yake kama atasajili au la kutokana na kuwagawa vigogo klabuni.

Gnamian alitua nchini asubuhi ya Ijumaa iliyopita akipokewa na Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro na mashabiki wengi waliamini jamaa anakuja kusaini na kuanza mambo kuziba mashimo yaliyoachwa na kina Juma Balinya, Issa Bigirimana na Sadney Urikhob.

Lakini buana kwa sasa utata mzito ukaibuka juu ya kipi kifanyike kwa mshambuliaji huyo mrefu kutokana na kuelezwa kuwa aliletwa kwa ushawishi wa bosi mmoja wa juu wa Yanga - tena kwa barua ambayo Mwanaspoti limeiona akiandikiwa kutoka ofisi kuu ya sekretarieti ya klabu hiyo akitakiwa kufika nchini kwa lengo la kusajiliwa.

TATIZO NINI?

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa Kamati ya Ufundi ambayo ndio imekuwa ikipendekeza majina ya wachezaji wa kusajiliwa kwa bilionea wa klabu hiyo, GSM, imegoma kumpitisha kwa vile hakuwa kwenye rada yao.

Baada ya kutua nchini Gnamian alikutana na kizuizi ambapo badala ya kusajiliwa moja kwa moja jopo la wajumbe wa Kamati ya Usajili walitaka kwanza afanyiwe majaribio.

Lengo hilo inadaiwa lilitokana na kamati hiyo kutomjua mshambuliaji huyo aliyeitumikia Gor Mahia ya Kenya wala ujio wake ambapo walitaka kujiridhisha kwanza juu ya ubora wake.

“Hatukuwa tunamjua kwani tulikuwa na makubaliano kama kamati na hata mwenyekiti wa kamati yetu analijua hilo kwamba wachezaji wengi tulihangaika kuwatafuta kabla ya kuwapeleka kwao ili wawalete,” alisema bosi mmoja kutoka Kamati ya Ufundi aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

“Lengo lilikuwa hatukutaka kuleta mchezaji ambaye badala ya kuipa faida klabu akageuka mzigo, ndio maana tulifanya mchakato huu wa kutafuta wachezaji kwa muda mrefu.”

AGOMEA MAJARIBIO

Mara baada ya Gnamian ambaye mpaka anaondoka Gor Mahia katika mechi 10 akifunga mabao mawili pekee tena katika mchezo mmoja, aligomea hatua ya kutakiwa kujaribiwa badala ya kusajiliwa kama ambavyo barua yake inavyoeleza.

Yanga ilitaka kusafiri na mshambuliaji huyo mpaka Mbeya ili ajifue na wenzake na benchi la ufundi la timu hiyo liweze kutoa majibu sahihi kama anafaa kupewa fomu, lakini jamaa alisema sio makubaliano yao na hivyo kuuchuna.

Hata hivyo, imefichuka kwamba msimamo huo mkali wa kamati hiyo ya ufundi ni kwamba tayari ilishawasiliana na baadhi ya wachezaji wao wa zamani kutoka Kenya kujua ubora wa mshambuliaji huyo na kuambiwa si mchezaji mbovu, lakini shida ipo katika rekodi yake ya majeruhi na nidhamu.

“Kule Kenya tumeshapata taarifa zake, tumeambiwa wakati wowote anaweza kugoma anakaa nyumbani endapo anaona kuna mambo hayapo sawa, pia tuliambiwa tuangalie sana afya yake, ana rekodi ya kuwa majeruhi kila mara, sasa mtu asione tunakurupuka kuweka mashaka,” alisema mjumbe mwingine.