Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

400 kushiriki mbio za baiskeli

BASKELI Pict

Muktasari:

  • Mbio hizo zitakazoshirikisha waendesha baiskeli zaidi ya 400 kutoka Tanzania na nje ya nchi, zitakuwa za kilomita 109 ambapo zitaanzia Dar es Salaam, kupitia Makurunge na kumalizikia Old Boma, Bagamoyo.

TANZANIA imefungua ukurasa mpya katika mchezo wa baiskeli baada ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA), kuzindua mashindano mapya ya Vodacom Coastal Classic yatakayofanyika Oktoba 4, 2026.

Mbio hizo zitakazoshirikisha waendesha baiskeli zaidi ya 400 kutoka Tanzania na nje ya nchi, zitakuwa za kilomita 109 ambapo zitaanzia Dar es Salaam, kupitia Makurunge na kumalizikia Old Boma, Bagamoyo.

Lengo la mbio hizo ni kutafuta vipaji vya ndani kushindana na waendesha baiskeli kutoka mataifa mbalimbali.

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, amesema kampuni hiyo inalenga kutumia mashindano hayo kutoa fursa kwa vipaji vya Watanzania na kuhamasisha watu wengi zaidi kushiriki katika mchezo wa baiskeli.

“Tunataka kuona Watanzania wakipata nafasi ya kushindana katika viwango vya juu. Tuna vipaji vingi vinavyohitaji kupewa fursa, mafunzo na mazingira bora ya kushindana,” amesema Kamando.

Amesema ushirikiano huo una lengo la kuhakikisha mchezo wa baiskeli unapata mazingira bora ya kukua na kutoa fursa zaidi kwa vijana wenye vipaji.

Uzinduzi wa Coastal Classic umefanyika sambamba na kutambulishwa kwa Nyerere Cycling Tour, ambayo inachukua nafasi ya msafara wa Twende Butiama ulioanzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuenzi falsafa na urithi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kupitia miradi ya elimu na maendeleo ya jamii.

Kwa mujibu wa waandaaji, Nyerere Cycling Tour imekuja na dira mpya ya kuendeleza msafara huo na kuugeuza kuwa jukwaa la kimataifa la mchezo wa baiskeli.

Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa, amesema uzinduzi huo ni mwanzo wa safari mpya ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mashindano ya baiskeli katika Afrika Mashariki.

“Nyerere Cycling Tour si msafara wa baiskeli pekee, bali ni mwendelezo wa maono ya Mwalimu Nyerere ya kutoa fursa sawa kwa Watanzania. Tunataka pia kuvutia waendesha baiskeli kutoka duniani kote kuja kushindana hapa nchini,” amesema Landa.

Nyerere Cycling Tour ya mwaka huu zitafanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 14, 2026 zikianzia Bagamoyo na kumalizikia Butiama.

Waandaaji wanatarajia mashindano hayo kuvutia waendesha baiskeli wa ndani na nje ya Tanzania, huku yakilenga kuongeza ushindani, kuibua vipaji na kukuza utalii wa michezo nchini.

Kwa kuanzishwa kwa Vodacom Coastal Classic na kuendelezwa kwa Nyerere Cycling Tour, Tanzania inalenga kutumia mchezo wa baiskeli kama sehemu ya kukuza vipaji, kuimarisha ushindani wa kimataifa na kuongeza fursa za utalii wa michezo.