Mkude, Maseke waibukia Mashujaa
Muktasari:
- Mkude amejiunga na Mashujaa baada ya kukaa nje ya soka msimu uliopita, kufuatia kuachana na Yanga ambayo aliitumikia kuanzia mwaka 2023 hadi 2025.
KIUNGO wa zamani wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Jonas Mkude, amejiunga na Mashujaa kwa mkataba wa mwaka mmoja, akitarajiwa kuongeza nguvu katika kikosi hicho kuelekea msimu mpya.
Mkude amejiunga na Mashujaa baada ya kukaa nje ya soka msimu uliopita, kufuatia kuachana na Yanga ambayo aliitumikia kuanzia mwaka 2023 hadi 2025.
Chanzo cha ndani ya Mashujaa kimesema klabu hiyo imeamua kumsajili Mkude kutokana na uzoefu wake mkubwa, huku ikiendelea kuamini kuwa bado ana uwezo wa kuisaidia timu hiyo.
“Ni kweli, Mkude baada ya kuachana na Yanga alikuwa nje ya uwanja, lakini hilo haliwezi kuondoa ubora na uwezo wake kama mchezaji. Lazima anatambua wajibu wake wa kufanya mazoezi binafsi, hivyo akijiunga na timu atajengwa na kurejeshwa katika utimamu wa mwili,” kilisema chanzo hicho.
Kabla ya kujiunga na Yanga, Mkude aliitumikia Simba kwa muda mrefu, kuanzia mwaka 2012 alipandishwa kutoka kikosi cha pili hadi mwaka 2022.
Uzoefu huo wa kufanya kazi chini ya makocha mbalimbali ni miongoni mwa mambo ambayo viongozi wa Mashujaa wanaamini yatakuwa na mchango mkubwa katika kikosi chao.
MASEKE NAYE MASHUJAA
Mbali na Mkude, Mashujaa pia imemsajili kipa Wilbol Maseke, aliyekuwa akiichezea Coastal Union ya Tanga msimu uliopita.
Ujio wa Maseke unaacha nafasi ya Erick Johola kuondoka baada ya kuhitimisha msimu uliopita akiwa na cleansheet saba, kabla ya kujiunga na Pamba Jiji.
“Maseke ni miongoni mwa makipa wazawa wazuri. Ujio wake utakuwa wa kusaidiana na Patrick Munthali, ambaye msimu uliopita alimaliza akiwa na cleansheet sita.
“Katika msimu wa 2024/25, Munthali alikuwa kinara kwa makipa wazawa akiwa na cleansheet 12, akifuatwa na Moussa Camara aliyekuwa Simba akiwa na 19 na Djigui Diarra akiwa na 17,” kilisema chanzo hicho.