Zeynep Mestan kuinoa Turgutluspor
Muktasari:
- Mestan, ambaye aliwahi kucheza soka la wanawake, amepewa jukumu la kuiongoza Turgutluspor katika hatua mpya ya ujenzi wa timu hiyo, huku uteuzi wake ukithibitishwa na klabu kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumanne.
ISTANBUL, UTURUKI: KLABU ya Turgutluspor imeandika historia katika soka la Uturuki baada ya kumteua mrembo Zeynep Mestan (22), kuwa kocha mpya wa kikosi chake cha wakubwa cha wanaume, hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kupewa jukumu hilo katika klabu hiyo.
Mestan, ambaye aliwahi kucheza soka la wanawake, amepewa jukumu la kuiongoza Turgutluspor katika hatua mpya ya ujenzi wa timu hiyo, huku uteuzi wake ukithibitishwa na klabu kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumanne.
Katika taarifa yake, Turgutluspor ilisema imefikia makubaliano na Mestan kuwa kocha kwa kuzingatia muundo na malengo ya msimu mpya, huku ikimtakia mafanikio katika kazi hiyo mpya.
Mestan ana wafuasi zaidi ya 21,000 kwenye Instagram kutokana na umaarufu alioupata wakati wa kucheza soka, ambapo aliwahi kuichezea klabu mbalimbali za wanawake katika maeneo ya Izmir na Manisa.
Alianza kucheza soka mwaka 2019 akiwa na Karsiyaka BES Spor, kabla ya kuendelea na klabu nyingine na baadaye kumalizia uchezaji wake mwaka 2025 akiwa Bornova Genc Yildizlar Spor.
Hatua yake ya kuingia kwenye ukocha imekuja wiki sita tu baada ya kutimiza umri wa miaka 22, jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa makocha vijana zaidi katika soka la wanaume.
Turgutluspor inatarajia kurejea kwenye ushindani baada ya kushushwa daraja hadi ngazi ya sita ya soka la Uturuki, kufuatia kumaliza nafasi ya 10 katika Ligi ya Bolgesel Amator msimu uliopita.
Hilo lilikuwa kushuka daraja kwa mara ya pili mfululizo kwa klabu hiyo, baada ya kumaliza nafasi ya 16 katika TFF 3. Ligi msimu wa 2024/25.
Msimu ujao pia utakuwa wa kwanza kwa Turgutluspor kushiriki Ligi ya Manisa Super Amateur, licha ya klabu hiyo kuwahi kucheza katika daraja la pili la soka la Uturuki hadi mwaka 2001.
Mestan anatarajiwa kuanza rasmi safari yake ya ukocha na Turgutluspor mwezi Oktoba, huku akipewa jukumu la kuiongoza klabu hiyo katika jitihada za kurejea kwenye ngazi za juu za soka nchini Uturuki.