Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wamegeuza umaarufu dili la kupiga mkwanja

Muktasari:

  • Katika miaka ya karibuni, tumeshuhudia mabadiliko makubwa ambapo wachezaji nyota wa Ligi Kuu Bara hawaishii tu kulipwa mishahara na klabu zao, bali wanatumia majina yao makubwa (brand names) na ushawishi wao kama mtaji wa kuingiza pesa nje ya uwanja ili kulinda mustakabali wao wa kifedha.

MCHEZO wa mpira wa miguu nchini Tanzania kwa sasa sio burudani tu, bali ni sekta kubwa ya kiuchumi.

Katika miaka ya karibuni, tumeshuhudia mabadiliko makubwa ambapo wachezaji nyota wa Ligi Kuu Bara hawaishii tu kulipwa mishahara na klabu zao, bali wanatumia majina yao makubwa (brand names) na ushawishi wao kama mtaji wa kuingiza pesa nje ya uwanja ili kulinda mustakabali wao wa kifedha.


Mohamed Hussein (Manukato)

Beki wa kushoto wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwa nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ameingia kwenye biashara ya bidhaa za manukato.

Nyota huyo anayeichezea Yanga kwa sasa akishirikiana kwa karibu na mkewe amewekeza kwenye biashara ya kuuza manukato kupitia duka lao maarufu lililopo Kinondoni Studio, Dar es Salaam.

Hii ni hatua ya kipekee kwani sekta ya manukato ina faida kubwa na inamfanya Shabalala kugusa soko la mashabiki wanaopenda kunukia vizuri hata wachezaji wenzake pia.

Clatous Chama (Bidhaa na viatu)

Mwamba wa Lusaka anayekipiga Simba kwa sasa ni balozi wa bidhaa na viatu (brand endorsement), lakini pia kiungo huyo fundi anamiliki mamilioni ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram.

Chama anatumia mtindo tofauti wa kibiashara badala ya kufungua duka lake binafsi, yeye anafanya matangazo makubwa ya biashara za viatu vya mtindo (sneakers) na mavazi.

Maduka makubwa ya nguo nchini yanamtumia kama nembo ya masoko (brand ambassador) ili kuvuta wateja, jambo linalomuingizia mkwanja wa maana kupitia matangazo anayoyafanya kupitia kurasa zake za kijamii.


Maxi Nzengeli (Jezi na mavazi)

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, raia wa DR Congo, Maxi Nzengeli, amekuwa kipenzi cha mashabiki kwa kasi na uwezo wake wa kufunga mabao.

Lakini, nje ya uwanja Max ameamua kutumia upendo huo kwa vitendo kwa kufungua duka la jezi na mavazi ya michezo. Hatua hii inamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wa kigeni wenye maono ya mbali akitumia jina lake lenye chapa inayoweza kuuza bidhaa kwa mashabiki.


Clement Mzize (Uwekezaji wa hisa)

Mshambuliaji wa Yanga na timu ya taifa (Taifa Stars), Clement Mzize, ni mfano bora wa vijana wa kisasa wenye nidhamu ya kifedha.

Mzize ameshatambulisha biashara zake mpya pamoja na kuwekeza kwenye hisa. Kuna wakati nyota huyo alionekana akishiriki kama mmoja wa vijana wanahisa katika mkutano mkuu wa benki moja kubwa ya kibiashara.

Hii inatuma ujumbe mzito kuwa mchezaji anaweza kutumia jina lake kufungua milango ya uwekezaji mkubwa wa kifedha. Lakini, nje na hilo pia ni mfanyabiashara wa duka la nguo za michezo na kawaida akitumia fursa ya jina lake kujiingizia kipato na kuvutia wateja au mashabiki.


Aishi Manula (Vifaa vya michezo)

Kipa mkongwe wa zamani wa Simba anayekipiga Azam FC kwa sasa, Aishi Manula, amekuwa mfano wa kuigwa kwa miaka mingi ambapo alipiga hatua kubwa ya kibiashara kwa kufungua duka kubwa la vifaa vya michezo.

Kama kipa mwenye ushawishi mkubwa, duka lake limekuwa likivutia wateja wengi wakiwemo wachezaji wenzake na makipa chipukizi wanaofuata vifaa vya kisasa kama glovu na viatu vya soka.

Lakini, ukiachana na mastaa hao watano kama mifano kuna nyota kibao wa soka na michezo mingine hapa nchini ambao wana harakati nyingi za kusaka mkwanja nje ya uwanja.


MSIKIE MKONGWE

Mchezaji wa zamani Simba, Duwa Said anasema kuwa: “Uamuzi wa mastaa hao unaonyesha kuwa fursa za kibiashara kwenye soka la Bongo hazina mipaka.

Iwe ni kuuza manukato (kama Tshabalala), nguo, vifaa vya michezo, uwekezaji wa hisa, au matangazo, jambo la msingi ni kuwa na nidhamu ya fedha mapema.

“Maisha ya soka uwanjani ni mafupi, lakini nguvu ya jina la mchezaji inaweza kuishi na kuzalisha pesa milele ikitumiwa kwa akili, hivyo wachezaji waliopo sasa wanakitu cha kujifunza kwa hawa na wale wa zamani ili wasije wakaishi maisha ya aibu baadaye.”