Ambulance viwanjani, kinga dhidi ya majanga ya soka
Muktasari:
- Gari hilo hutumika kutoa huduma za dharura kwa wachezaji na watazamaji, ikiwamo uokoaji wa maisha kama vile huduma ya utomasaji moyo (CPR), majeraha ya uti wa mgongo, majeraha ya kichwa na majeraha ya mivunjiko yenye jeraha la wazi.
KWA mujibu wa kanuni za soka zilizopokewa kutoka Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), katika kila mchezo wa soka ni lazima kuwepo na gari la wagonjwa, yaani Ambulance.
Gari hilo hutumika kutoa huduma za dharura kwa wachezaji na watazamaji, ikiwamo uokoaji wa maisha kama vile huduma ya utomasaji moyo (CPR), majeraha ya uti wa mgongo, majeraha ya kichwa na majeraha ya mivunjiko yenye jeraha la wazi.
Majeraha kama haya yasipopatiwa huduma za dharura kwa wakati, mgonjwa anaweza kupoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu.
Magari haya huwa na wataalamu wa afya wenye ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kiafya yanayohitaji huduma za dharura, ambao huweza kutoa huduma eneo lilipotokea tukio na njiani wakati mgonjwa akisafirishwa kwenda katika kituo cha kutolea huduma kilicho jirani.
Hata dereva wa magari hayo ana ujuzi wa mambo ya huduma za dharura, hivyo kuifanya timu nzima iliyopo katika gari hilo kuwa timamu katika kutoa huduma za dharura.
Mtakumbuka matukio makubwa ya dharura yaliyowahi kutokea katika viwanja vya soka, ikiwamo lile la Juni 2021 la mchezaji wa soka wa Denmark, Christian Eriksen, kuanguka na kupoteza fahamu.
Timu ya wataalamu wa afya waliokuwepo katika Ambulance ndiyo iliyobeba jukumu la kumbeba mchezaji huyo, huku pia akiendelea kupewa huduma mbalimbali akiwa anasafirishwa kwenda katika kituo maalum cha kukabiliana na matatizo ya dharura.
Miongozo ya Fifa inaelekeza kuwepo kwa gari la wagonjwa katika kila mechi kubwa, hasa zinazohusisha ushindani mkubwa pamoja na idadi kubwa ya mashabiki. Mtakumbuka ndani ya uwanja wa soka kunatokea faulo za kimichezo, ikiwamo zinazohusisha majeraha ya kichwa ambayo yanahitaji huduma za dharura zinazotolewa na gari la wagonjwa.
KUHUSU GARI LA WAGONJWA IKO HIVI
Magari ya kubebea wagonjwa, Ambulance, yalianzishwa mwaka 1487 kwa ajili ya usafiri wa dharura kwa wagonjwa na majeshi ya Hispania katika mji wa Malaga. Miaka hiyo, farasi na punda ndiyo walikuwa wakivuta tela maalum lenye huduma mbalimbali, ikiwamo za dharura. Kazi ya magari haya si tu kwa ajili ya kumtoa mgonjwa kutoka pointi moja kwenda nyingine kwa ajili ya kupata huduma, bali pia huwa na vifaa tiba, dawa na wataalamu wa afya wenye ujuzi. Ndiyo maana mgonjwa huweza kupewa huduma akiwa ndani ya ambulance.
Suala la ambulance kuwepo katika mechi za soka haliepukiki, kwani soka ni aina ya mchezo unaohusisha kugusana kimwili huku ukiwa na nguvu na kasi, hivyo kuweza kusababisha majeraha, ikiwamo majeraha ya kichwa, shambulio la moyo na mivunjiko mikubwa.
Vilevile, magari haya katika viwanja vya soka yapo pia kwa ajili ya kutoa huduma za dharura kwa watazamaji wanaopata matatizo ya kiafya, ikiwamo kuzimia au kudondoka. Kutokana na kukua kwa teknolojia katika karne ya 19 na 20, Ambulance zilipiga hatua na hivi sasa kuna ambulance ya anga, yaani ndege, pamoja na Ambulance ya majini, yaani meli au boti. Lakini, kutokana na matumizi ya ambulance ya ardhini kuwa makubwa, ilisababisha kuwa na aina tatu za ambulance ambazo ni daraja I, II na III.
Ambulance ya daraja la III huwa na tela linalovutwa na gari, likiwa na chumba na vifaa vya upasuaji.
Yana vifaa tiba muhimu, ikiwamo mitungi ya oksijeni na vifaa vyake saidizi, mashine ya kustua moyo, mashine ya kupima mwenendo wa viashiria nyeti vya uhai kama vile mapigo ya moyo, unyepesi wa mishipa ya damu, upumuaji, joto na kiwango cha oksijeni.
Vilevile huwa na dawa zote muhimu kwa ajili ya kukabiliana na matatizo ya dharura, ikiwamo dawa ya adrenaline, dawa za kukabiliana na sumu za madawa ya kuulia wadudu, dawa za kukabiliana na pumu na dawa za kushusha shinikizo la juu la moyo.
Huwa na begi kubwa la kuhifadhia dawa na vifaa tiba, begi la vifaa vya kukabiliana na majeraha, mashine ya kunyonya ute na maji maji ya mwilini, barakoa maalum kwa ajili ya upumuaji, kitanda, mashine ya kusaidia upumuaji na mashine ya kusoma mwenendo wa moyo.
Vilevile huwa na kifaa tiba maalum cha shingoni, pamoja na kifaa tiba cha kubebea na kutuliza mwili kwa majeruhi wa shingo na uti wa mgongo.
Gari ya wagonjwa ijulikanayo kama Emergency Ambulance ndiyo inayotumika sana kukabiliana na magonjwa na majeraha ikiwa katika mfumo wa magari ya barabarani, ndege, helikopta, meli na boti.
Kwa ambulance ya kawaida, huwa na uwezo wa kubeba mgonjwa mmoja aliyelazwa kitandani na wawili wenye kukaa, huku ikiwa na dereva, tabibu na muuguzi.
Kwa kawaida, magari haya huhitajika kumpeleka mgonjwa katika kituo cha kutolea huduma za afya na kisha kurudi katika eneo lake la uwajibikaji. Kwa kawaida, magari haya hayatumiki kubebea maiti bali wagonjwa tu.
Neno 'ambulance' katika magari hayo huandikwa kinyume nyuma kwa lengo la kuwezesha magari mengine kuliona katika vioo vyao vya pembeni na katikati na kulisoma neno Ambulance sawa sawa.
USHAURI
Uwepo wa gari la wagonjwa katika viwanja vya soka kwa wakati haukwepeki, kwani matatizo ya kiafya ya dharura hayana hodi. Katika mechi zote ni muhimu kuwepo kwa magari haya viwanjani.
Ligi kubwa kama NBC zinahitaji gari lililo na vifaa kamili, madaktari waliohitimu pamoja na daktari atakayekuwepo uwanjani wakati wa mechi na mazoezi.