Serge Aurier aibukia timu ya daraja la saba
Muktasari:
- Aurier (33), ambaye aliisaidia Tottenham kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuachana na klabu ya Persepolis ya Iran mapema mwaka huu.
PARIS, UFARANSA: BEKI wa zamani wa Tottenham, Serge Aurier yuko mbioni kufanya uamuzi wa kushangaza katika kipindi hiki cha mwisho wa soka lake, akitarajiwa kujiunga na klabu ya daraja la saba nchini Ufaransa.
Aurier (33), ambaye aliisaidia Tottenham kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuachana na klabu ya Persepolis ya Iran mapema mwaka huu.
Beki huyo wa kulia anafanya mazungumzo na Montigny-en-Gohelle, klabu inayoshiriki Ligi ya Mkoa ya Hauts-de-France, daraja la pili la mashindano ya eneo hilo.
Montigny-en-Gohelle, inayopatikana takribani kilomita 13 mashariki mwa Lens, ilipokea kipigo cha aibu mwishoni mwa wiki baada ya kufungwa mabao 10 dhidi ya wapinzani wao Biache-Saint-Vaast.
Kwa mujibu wa taarifa, mpango wa Aurier kujiunga na klabu hiyo umechelewa kukamilika kutokana na kusubiri nyaraka kutoka Shirikisho la Soka la Iran (FA).
Hata hivyo, vyanzo vilivyo karibu na mchezaji huyo viliambia gazeti la ndani la La Voix du Nord kuwa vinatarajia Aurier kupewa ruhusa ya kusaini mkataba huo muda wowote.
Aurier alianza safari yake ya soka katika akademi ya Lens na baadaye akapandishwa kikosi cha kwanza, ambako alicheza mechi yake ya kwanza ya kulipwa.
Kwa sasa amerejea katika klabu hiyo akiwa kocha wa kikosi cha vijana wenye umri wa chini ya miaka 15, lakini inaonekana bado hana mpango wa kuachana kabisa na soka la ushindani.
Akiwa Tottenham, Aurier alicheza mechi 110 na kufunga mabao nane baada ya klabu hiyo kumsajili kutoka Paris Saint-Germain (PSG) kwa ada ya pauni 23milioni mwaka 2017. Aliondoka Spurs mwaka 2021 na baadaye akatumia misimu miwili Nottingham Forest.
Aurier pia amewahi kuzitumikia Toulouse, Villarreal na Galatasaray, ambapo aliisaidia klabu hiyo ya Uturuki kutwaa ubingwa wa Super Lig mwaka 2024.
Katika kipindi chake PSG, Aurier alitwaa mataji 11, huku akiwa sehemu ya kikosi cha Ivory Coast kilichotwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mara mbili.
Sasa, baada ya kucheza katika baadhi ya klabu kubwa barani Ulaya, Aurier yuko mbioni kuendelea na safari yake ya soka katika ngazi ya chini kabisa nchini Ufaransa.