Yamal hataki kuwa Messi wala Ronaldo
Muktasari:
- Kinachomfanya Lamine Yamal kuwa mchezaji wa kipekee si sifa anazopewa pekee, bali ni utulivu anaouonyesha anapozipokea na namna alivyoanza kujenga utambulisho wake kama mwanasoka bora.
LONDON ENGLAND: Mkongwe na mshindi mara nane wa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka Lionel Messi hana shaka hata kidogo.
Alipoulizwa katika hafla ya uzinduzi wa tangazo la Kombe la Dunia amtaje mchezaji bora wa kizazi kipya, alijibu: “Ni Lamine. Bila shaka yoyote; kwangu mimi ndiye bora zaidi.”
Wiki hiyo hiyo, kituo cha televisheni cha Marekani, CBS, kilimuuliza Lamine Yamal mbele ya kamera kama Hispania itashinda Kombe la Dunia. Alitabasamu na kujibu kwa ufupi: “Ndiyo.”
Kinachomfanya Lamine Yamal kuwa mchezaji wa kipekee si sifa anazopewa pekee, bali ni utulivu anaouonyesha anapozipokea na namna alivyoanza kujenga utambulisho wake kama mwanasoka bora.
Akiwa na umri wa miaka 18 tu. Tayari amecheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, ameshinda ubingwa wa Ulaya na Hispania. Kiwango chake kimewafanya Barcelona kumpa jezi namba 10 iliyokuwa inavaliwa na Messi jambo linalovutia zaidi si mafanikio yake akiwa na umri mdogo, bali ni utulivu wake wa kiakili.
Ulinganisho na Messi hauwezi kuepukika
Ulinganisho kati ya Yamal na Messi hujitokeza bila kujali kama Yamal anautaka au la.
Kwanza, wote wanatumia zaidi mguu wa kushoto. Aidha, Yamal ana akili ya hali ya juu ya kupiga chenga na uwezo wa kufanya mambo magumu yaonekane rahisi, sifa ambazo pia zilimtambulisha Messi.
Kwa kweli, akiwa katika umri huo, Yamal ameonyesha ushawishi zaidi kuliko Messi. Hata hivyo, bado ni mapema kusema atafikia kiwango kilekile alichokifikia nyota huyo wa Argentina.
Licha ya ugumu wa kuwalinganisha moja kwa moja, takwimu moja inaonyesha kuwa Yamal anaelekea kuwa mrithi halali wa Messi. Akiwa na miaka 18 pekee, tayari ameichezea Barcelona mechi 151. Kufikia siku ya kuzaliwa ya Messi ya miaka 19 tarehe 24 Juni 2006, alikuwa amecheza mechi 41 tu za timu ya kwanza ya Barcelona.
Ronaldinho, ambaye alicheza pamoja na Messi mwanzoni mwa enzi ya mafanikio ya Barcelona na kushinda Ligi ya Mabingwa pamoja naye, anaona mfululizo huo ukiendelea kufikiwa na Yamal.
“Mimi na Messi tuliandika historia, na sasa ni zamu ya Lamine Yamal. Kile alichokwisha kuonyesha akiwa na umri mdogo ni cha ajabu sana,” amesema Ronaldinho katika mahojiano na FIFA mwezi Machi.
Aliyekuwa beki wa Manchester United, Rio Ferdinand, alienda mbali zaidi alipoulizwa kama Yamal tayari ni bora kuliko Messi na Cristiano Ronaldo walivyokuwa katika umri kama wake.
“Ndiyo,” alijibu Ferdinand kwenye ESPN. “Uwezo wake wa kufikia kiwango cha juu unaweza kuwa mkubwa zaidi kuliko wao. Kile alichokifanya akiwa na miaka 17 hakuna aliyewahi kukifanya. Labda Pele, lakini mimi sikumuona Pele akicheza.”
“Presha haipo, ni kisingizio”
Historia ya soka imejaa wachezaji waliotajwa kuwa warithi wa Messi lakini baadaye wakakutana na changamoto mbalimbali.
Majina kama Giovani dos Santos, Gerard Deulofeu, Ansu Fati, Munir El Haddadi na hasa Bojan Krkic yaliwahi kutajwa kama nyota wakubwa wa baadaye.
Lakini Yamal amechagua kuacha vyombo vya habari viendelee na mijadala hiyo huku yeye akijikita zaidi uwanjani. Hata mazungumzo ya kuwania tuzo ya Ballon d’Or yamekuwa yakimfuata tangu akiwa na miaka 16.
Anasema anacheza soka ili watu wafurahie. Anataka watoto watamani kuwa kama yeye, si lazima wawe kama Messi au Ronaldo.
“Sifikirii Ballon d’Or. Ninataka kufurahia soka na kushinda na Barcelona pamoja na timu ya taifa,” amesema.
“Presha haipo, ni kisingizio tu. Ukiwaza kufurahia na kujiburudisha, hakuna presha.”
Kocha wake wa zamani katika akademi ya Barcelona, Inocente Diaz, alikuwa akisema jambo kama hilo miaka kadhaa iliyopita.
“Yeye ni bora hata kuliko Messi,” aliiambia gazeti la Sport mwaka 2025. “Ana mchanganyiko wa kipekee wa sifa za kimwili zinazomkumbusha Messi na Cristiano Ronaldo. Ndani ya miaka sita atashinda Ballon d’Or.”
Ndoto ya Kombe la Dunia
Kwa upande wake, Lamine Yamal ameweka macho yake kwenye Kombe la Dunia.
Tayari ameeleza anavyoiamini nafasi ya Hispania katika mashindano hayo. Jibu lake lilikuwa neno moja tu kwa Kiingereza: “Yes”.
Lakini nyuma ya tabasamu hilo kuna mchezaji ambaye ameota kushiriki Kombe la Dunia maisha yake yote.
“Siku zote nimekuwa nikijiwazia nikicheza Kombe la Dunia, nikimuona mama yangu akiwa jukwaani. Natumaini nitaweza kushinda,” amesema Yamal.