Luis Díaz kuiongoza Colombia Kombe la Dunia 2026, James Rodríguez naye ndani
Muktasari:
- Kocha mkuu wa timu hiyo, Néstor Lorenzo, ametangaza kikosi hicho usiku wa kuamkia leo Jumanne, Mei 26, 2026, huku kikiwa na mchanganyiko wa damu changa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa.
Mshambuliaji Luis Díaz, amejumuishwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 26 watakaoliwakilisha taifa la Colombia kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2026, itakayounguruma nchini Marekani, Mexico na Canada.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Néstor Lorenzo, ametangaza kikosi hicho usiku wa kuamkia leo Jumanne, Mei 26, 2026, huku kikiwa na mchanganyiko wa damu changa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa.
Katika uteuzi huo, nyota wa zamani wa Real Madrid na Bayern Munich, James Rodríguez, anatarajiwa kuongeza ubunifu na uzoefu mkubwa katika safu ya kiungo.
Aidha, aliyekuwa kiungo wa Bayer Leverkusen, Gustavo Puerta, naye amefanikiwa kupata nafasi katika kikosi hicho kitakachopambana kuwania taji hilo kubwa zaidi duniani.
Safu ya ulinzi na makipa itakuwa chini ya ‘makomando wa zamani’ kama David Ospina, Davinson Sánchez, na Yerry Mina, ambao watashirikiana na mabeki chipukizi kuhakikisha lango linakuwa salama.
Kwenye safu ya ushambuliaji, Díaz atasaidiwa na nyota wengine hatari kama Jhon Córdoba na Luis Suárez ili kuhakikisha Colombia inapata mabao ya kutosha.
Kikosi kamili cha Colombia kilichotangazwa kipo hivi; Makipa: Camilo Vargas, Alvaro Montero, David Ospina.
Mabeki: Daniel Munoz, Davinson Sanchez, Jhon Lucumi, Johan Mojica, Willer Ditta, Santiago Arias, Deiver Machado, Yerry Mina.
Viungo: Jefferson Lerma, Jhon Arias, Jorge Carrascal, Juan Camilo Portilla, Richard Rios, Juan Fernando Quintero, Gustavo Puerta, Kevin Castano, James Rodriguez, Jaminton Campaz.
Washambuliaji: Luis Diaz, Jhon Cordoba, Luis Suarez, Juan Camilo Hernandez, Carlos Andres Gomez.