Yale ya Pogba yamkuta Mudryk wa Chelsea
Muktasari:
- Winga huyo, ambaye aliigharimu Chelsea Pauni 88.5 milioni wakati inamsajili, vipimo vyake vilionyesha ‘positive’ baada ya kupimwa mkojo kutambua kama kuna matumizi ya virutubisho vinavyopigwa marufuku michezoni mwishoni mwa mwezi Oktoba.
LONDON, ENGLAND: STAA wa Chelsea, Mykhailo Mudryk amepigwa marufuku kucheza soka na ripoti zinafichua huenda akakabiliana na adhabu ya kufungiwa miaka minne baada ya kufeli kwenye vipimo vya matumizi ya dawa zinazokatazwa michezoni.
Winga huyo, ambaye aliigharimu Chelsea Pauni 88.5 milioni wakati inamsajili, vipimo vyake vilionyesha ‘positive’ baada ya kupimwa mkojo kutambua kama kuna matumizi ya virutubisho vinavyopigwa marufuku michezoni mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Mudryk na Chelsea kwa sasa wanasubiri majibu ya vipimo vya pili baada ya vile vya kwanza kuonyesha staa huyo ametumia dawa sizizoruhusiwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Tribuna la Ukraine linadai Mudryk amepimwa na kutoa majibu ya positive kwenye matumizi ya Meldonium, virutubisho vinavyokatazwa michezoni kwa sababu vinasisimua misuli kama ilivyo kwa insulini.
Kirutubisho hicho kinaufanya mwili kupata oksijeni ya wingi na kuupa mwili nguvu iliyokuwa imepotea ili kuufanya mwili kuwa vizuri.
Meldonium imekuwa ikitumika sana Ulaya Mashariki, lakini imewekwa kwenye orodha ya dawa zisizoruhusiwa kwenye michezo na Wakala wa Kupiga Matumizi ya Dawa michezoni (WADA) tangu mwaka 2016.
Staa wa mchezo wa tenisi, mrembo Maria Sharapova alifungiwa miezi 15 baada ya kupimwa na kukuta ametumia meldonium katika mashindano ya Australian Open mwaka 2016.
Kama vipimo vya pili vikitoa majibu vya kwanza, Mudryk atakuwa kwenye hatari ya kufungiwa soka miaka minne.
Kwa sasa winga huyo mwenye umri wa miaka 23 amezuiliwa na FA kama adhabu ya awali baada ya majibu ya vipimo vya kwanza.
Mudryk kwenye taarifa yake ya jana Jumanne asubuhi alisema akisisitiza hakufahamu kama anatumia virutubisho vyovyote vinavyopigwa marufuku michezoni.
Alisema: “Naweza kuthibitisha sampo ya kwanza niliyowapa FA kwa ajili ya kupimwa imekutwa na viturubisho visivyoruhusiwa. Hii kitu ilinishtua kwa sababu sikuwahi kufahamu kama natumia virutubisho vyovyote vinavyokatazwa na navunja sheria na nitashirikiana kwa karibu na timu yangu kwenye uchunguzi kuona hiki kitu kimetokeaje.”
Mudryk aliongeza: “Nafahamu sijafanya kosa na ninaamini nitarejea uwanjani muda si mrefu. Sitaki kusema zaidi kutokana na usiri wa tukio lenyewe, lakini nafahamu nitarudi uwanjani kwa haraka kadri inavyowezekana.”
Chelsea ilitoa taarifa yake iliyosomeka: “Chelsea Football Club inathibitisha Chama Cha Soka England kuwasiliana na mchezaji wetu Mykhailo Mudryk kutokana na majibu yaliyopatikana kwenye vipimo vya mkojo ilivyomfanyia. Klabu na Mykhailo tutasapoti shughuli hiyo ya upimaji inayofanywa na FA kwa wachezaji wetu, akiwamo Mykhailo. Mykhailo amesema hajawahi kufanya kwa kujua kama anatumia virutubisho vinavyokatazwa. Chelsea na Mykhailo sasa itafanya kazi bega kwa bega na mamlaka juu ya majibu yaliyopatikana. Klabu haina cha kuongeza.”
Mudryk haijachezea Chelsea tangu alipofunga bao kwenye ushindi wa 2-0 kwenye michuano ya Conference League dhidi ya Heindenheim, Novemba 28. Hajawahi kujumuishwa kwenye kikosi tangu kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Aston Villa katika mikikimikiki ya Ligi Kuu England, Desemba 1. Miongo miwili iliyopita, Chelsea ilishuhudia straika wao wa kutoka Romania, Adrian Mutu alifungiwa kucheza soka kwa miezi saba, Septemba 2004 baada ya kupimwa na kukutwa anatumia cocaine. Baada ya hapo, Chelsea ilisitisha mkataba wa Mutu kutokana na mshambuliaji huyo kukiuka vipengele na The Blues ililipwa fidia ya Pauni 14 milioni. Mwaka 2003, beki wa zamani wa Manchester United na England, Rio Ferdinand alifungiwa kucheza soka miezi minane baada ya kufeli vipimo vya matumizi ya dawa zinazopigwa marufuku michezoni.
Kiungo wa zamani wa Man United na Juventus, Paul Pogba naye alifungiwa miezi 18, Agosti 2023 baada ya kupimwa na kukutwa ametumia viturubisho vya kusisimua misuli vya DHEA, jambo lililosababisha mkataba wake kusitishwa huko Juventus. Mudryk alijiunga na Chelsea kwa pesa nyingi akitokea Shakhtar Donetsk, Januari 2023. Alishindwa kuonyesha makali kwenye miezi yake sita ya kwanza, akiwa hajafunga bao lolote katika mechi 17.
Msimu uliopita, alifunga mabao saba katika mechi 41. Msimu huu amefunga mabao matatu katika mechi 15, huku mabao yote hayo akifunga kwenye michuano ya Ulaya.