Prime
Hamisa Mobetto afunguka tetesi za Aziz Ki kusajiliwa Yanga
GUMZO la kurejea kwa kiungo mshambuliaji wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki, ndani ya kikosi cha Yanga, limeendelea kutawala mijadala ya mashabiki wa soka nchini, huku wengi wakisubiri kwa hamu kujua kama nyota huyo atavaa tena jezi za kijani na njano katika dirisha hili la usajili.
Tetesi hizo zilianza kusambaa kwa kasi mwishoni mwa wiki uliopita baada ya baadhi ya kurasa za michezo na wadau wa soka kudai kuwa Yanga inafanya mipango ya kumrejesha kiungo huyo aliyewahi kuwa tegemeo la timu hiyo kabla ya kuhamia Morocco mwaka 2025.
Kutokana na gumzo hilo, mashabiki wengi wamekuwa wakimiminika kwenye mitandao ya kijamii ya Hamisa Mobetto, ambaye ni mke wa Aziz Ki, wakitaka kujua ukweli wa taarifa hizo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hamisa alisema amepokea ujumbe mwingi kutoka kwa mashabiki wanaouliza kuhusu hatma ya mume wake, lakini akaweka wazi kuwa hana taarifa zozote za kuwajibu.
"Ninapata meseji nyingi sana za watu na kwenye komenti ninapoposti kitu kwa akaunti yangu Instagram wakiniuliza kama Aziz anarudi Yanga kucheza. Ukweli ni kwamba hata mimi naona hizo taarifa kama zinavyosambaa mitandaoni, lakini kwenye hilo sina jibu la kuwapa kwa sababu sina taarifa rasmi za kuthibitisha kama ni kweli au si kweli."
Kauli hiyo ya Hamisa imezidi kuongeza hamu ya mashabiki wa Yanga ambao wameendelea kuamini huenda klabu hiyo ikafanya usajili mkubwa wa kumrudisha mmoja wa wachezaji waliowahi kuipa mafanikio makubwa katika miaka ya karibuni.
Aziz Ki alijiunga na Yanga mwaka 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast na ndani ya misimu miwili aliyocheza Jangwani alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa kikosi hicho.
Mbali na kuchangia ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), aliisaidia Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/23, mafanikio yaliyomfanya kuwa kipenzi cha mashabiki wa Wananchi.
Baada ya kumalizika kwa msimu wa 2024/25, Aziz Ki aliondoka Yanga na kujiunga na Wydad Athletic Club ya Morocco, hatua iliyozua hisia tofauti kwa mashabiki waliokuwa wakitamani aendelee kusalia Jangwani.
Hadi sasa hakuna tamko rasmi kutoka Yanga wala kutoka kwa kambi ya Aziz Ki linalothibitisha taarifa za kurejea kwake.
Hata hivyo, gumzo hilo limeendelea kuteka hisia za mashabiki, wengi wakiamini kuwa kama usajili huo utakamilika utakuwa miongoni mwa dili kubwa zaidi za dirisha hili la usajili nchini.