Liverpool njia nyeupe kwa Barcola
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ufaransa, mazungumzo kati ya Barcola na vigogo hao wa England yamezaa matunda, huku kocha mpya wa Liverpool, Andoni Iraola akitajwa kuwa mtu muhimu aliyemshawishi mchezaji huyo kuichagua Anfield.
LONDON, ENGLAND: LIVERPOOL imepiga hatua muhimu katika harakati za kumsajili winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, baada ya kufikia makubaliano ya awali na nyota huyo wa Ufaransa kuhusu uhamisho wake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ufaransa, mazungumzo kati ya Barcola na vigogo hao wa England yamezaa matunda, huku kocha mpya wa Liverpool, Andoni Iraola akitajwa kuwa mtu muhimu aliyemshawishi mchezaji huyo kuichagua Anfield.
Hata hivyo, kazi bado haijaisha. Liverpool sasa italazimika kuafikiana na PSG kuhusu ada ya usajili, ambapo mabingwa hao wa Ligue 1 wanadaiwa kutaka kiasi cha pauni 140milioni ili kumruhusu winga huyo kuondoka.
Licha ya Arsenal na vigogo wengine wa Ulaya kuonyesha nia ya kumsajili Barcola, Liverpool inaonekana kuwa mbele kwenye mbio hizo baada ya kufikia mwafaka binafsi na mchezaji huyo.
Barcola, ambaye amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake, ameripotiwa kukataa kuongeza mkataba mpya na PSG, jambo lililofungua mlango wa kuondoka kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Liverpool imekuwa ikimfuatilia kwa muda mrefu ikisaka mrithi wa Mohamed Salah pamoja na kuboresha safu yake ya ushambuliaji kuelekea msimu mpya.
Nyota huyo wa zamani wa Lyon amekuwa akipata nafasi chache ndani ya kikosi cha kocha Luis Enrique, baada ya kushushwa kwenye mpangilio wa uchaguzi na Khvicha Kvaratskhelia pamoja na Desire Doue.
Hata akiwa anakabiliwa na ushindani mkali PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Barcola bado alitoa mchango mkubwa msimu uliopita. Alifunga mabao 13 na kutoa pasi saba za mabao katika mashindano yote, akifanya hivyo ndani ya mechi 35 alizoanza kikosi cha kwanza na kucheza takribani dakika 3,000.
Kiwango hicho kinamaanisha alihusika moja kwa moja kwenye bao karibu kila baada ya mechi mbili, rekodi inayomfanya kuwa mmoja wa mawinga wenye tija barani Ulaya.
Katika timu ya taifa ya Ufaransa, Barcola tayari ameichezea mechi 28 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki Kombe la Dunia lililomalizika hivi karibuni. Alicheza mechi nane kwenye michuano hiyo na kufunga mabao matatu, likiwemo moja dhidi ya England kwenye mchezo wa kusaka mshindi wa nafasi ya tatu.
Ingawa alianza mechi nne kama mchezaji wa kikosi cha kwanza, safari yake ilikatizwa kwenye nusu fainali dhidi ya Hispania baada ya kutolewa dakika ya 60 kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa.
Sasa macho yote yanaelekezwa kwenye mazungumzo kati ya Liverpool na PSG, huku vigogo hao wa Anfield wakiamini wanaweza kukamilisha moja ya usajili mkubwa zaidi wa dirisha hili na kumpata mchezaji wanayemuona kuwa sehemu muhimu ya enzi mpya chini ya Iraola.