Xavi atimuliwa Barca, Milan yamtema Pioli

Muktasari:
- Katikati mwa msimu Xavi aliwahi kusema kuwa ataondoka kwenye kikosi cha Barcelona mwishoni mwa msimu huu, lakini wakati msimu ukikaribia kumalizika ilitoka taarifa kuwa Barcelona inazungumza na kocha huyo ili abaki.
Barcelona, Hispania. Klabu ya Barcelona imemtimua kocha wake Xavi Hernandez baada ya kudumu klabu hapo kwa miaka mitatu.
Katikati mwa msimu Xavi aliwahi kusema kuwa ataondoka kwenye kikosi cha Barcelona mwishoni mwa msimu huu, lakini wakati msimu ukikaribia kumalizika ilitoka taarifa kuwa Barcelona inazungumza na kocha huyo ili abaki.
Taarifa iliyotolewa muda mfupi uliopita, imesema kuwa klabu hiyo imeachana na kocha huyo na inatarajia kumtangaza mbadala wake muda mchache ujao.
Kwa mujibu wa mwandishi mahiri Fabrizio Romano, Xavi ametakiwa kumalizia mchezo wa mwisho wa Jumapili dhidi ya Sevilla na kuondoka klabu hapo.
Wakati mwandishi huyo akiandika hivyo, vyombo vingine vimesema kuwa kocha mzoefu Hansi Flick, anatarajiwa kuchukua nafasi ya Xavi kwenye kikosi hicho ambacho msimu huu kimemaliza mikono mitupu.
Inaelezwa kuwa Xavi alipewa taarifa ya kutimuliwa leo asubuhi baada ya rais wa timu hiyo Joan Laporta, kwenda kwenye mazoezi ya Barcelona huku timu yake ikiwa pointi kumi nyuma ya Real Madrid ambayo imeshatwaa ubingwa.
Pamoja na kuwa kocha hapo na kutwaa ubingwa mmoja wa La Liga, Xavi alikaa kwenye kikosi cha Barcelona kwa miaka 24 akiwa mchezaji mahiri wa timu hiyo akicheza michezo 767 na kutwaa makombe makubwa 25.
Wakati huohuo, AC Milan nayo imetangaza kuachana na kocha wake Stefano Pioli ambaye amedumu kwenye timu hiyo kwa miaka mitano.
Taarifa rasmi ya klabu hiyo imesema:"AC Milan na kocha Stefano Pioli zimkubaliana kuwa meneja huyo ataondoka kwenye timu baada ya mchezo wa mwisho wa msimu huu baada ya kuwa hapa tangu Oktoba mwaka 2019.
"AC Milan inawatakia kila la kheri Stefano Pioli na wasaidizi wake na ina mshukuru kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwenye timu hii tunaamini anapokwenda atafanya kazi bora zaidi," ilisema taarifa hiyo.
Milan ikiwa imebakiza mchezo mmoja ipo nafasi ya pili kwenye ligi ya Italia na pointi 74, Inter Milan ikiwa kileleni na pointi 93.