X-Mass, Mwaka Mpya kwa Arsenal kicheko
Muktasari:
- Lakini, kwenye soka hasa katika Ligi Kuu England, kipindi hicho kinakuwa na purukushani nyingi kwa timu kutokana na kukabiliwa na ratiba ya mechi nyingi katika msako wao wa kusaka ubingwa wa mataji mbalimbali.
LONDON, ENGLAND: KRISMASI na Mwaka Mpya ni kipindi cha harakati nyingi na ubize wa kutosha kwa watu kusafiri kwa sababu ni kipindi cha likizo.
Lakini, kwenye soka hasa katika Ligi Kuu England, kipindi hicho kinakuwa na purukushani nyingi kwa timu kutokana na kukabiliwa na ratiba ya mechi nyingi katika msako wao wa kusaka ubingwa wa mataji mbalimbali.
Bahati nzuri kwa mwaka huu ipo Arsenal na ratiba iliyopangwa kwenye mechi za kipindi hiki, kuwafanya kusafiri umbali mdogo kulinganisha na wapinzani wake wengine kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
Kocha Mikel Arteta na chama lake la Arsenal amekuwa na zali la mentali kwenye ratiba ya mechi zake za mwezi huu za kuelekea Krismasi na Mwaka mpya, na mechi 13 ambazo itacheza timu yake, nyingi zitachezwa kwenye jiji la London.
Ratiba ya mechi zao zinavyosoma, Arsenal itasafiri kutoka nje ya London mara moja tu kabla ya Januari 22, huku mechi zao tatu za ugenini zote zitakuwa kwenye Jiji la London.
Mechi yao dhidi ya Brighton itakayopigwa Januari 4, 2025 ndiyo pekee kwenye Ligi Kuu England, ambayo itachezwa nje ya London.
Kitu kizuri kwa Arteta kipindi hiki ni timu yake itacheza mechi tisa kwenye Uwanja wa Emirates, wakianza na Manchester United katika kipute kitakachopigwa usiku wa leo Jumatano kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, huku ratiba yao ya mechi 13 itakamilishwa na kipute dhidi ya Dinamo Zagreb, Januari 22.
Katika mechi zake za ugenini katika orodha ya mechi 13 itakayocheza kipindi hiki, Arsenal itasafiri kwa umbali usiozidi maili 250, wastani wa kilomita 400 tu. Mechi yao na Brighton peke yake ndiyo watakayosafiri umbali mrefu, maili 177.4.
Wakati huo mechi za Fulham, Crystal Palace na Brentford itasafiri maili 21.2, 26, na 24 mtawalia.
Hofu ya Arteta na chama lake la Arsenal ilikuwa kwenye safari ya juzi Jumatatu kwenda kwenye upangaji wa droo ya Kombe la FA huko Manchester. Kwenye droo hiyo iliyofanyika Old Trafford, Arsenal ilipangwa kukabiliana na Man United, kipute ambacho kitafanyika Emirates, Januari mwakani. Kwa ratiba hiyo, ina maana Arsenal itakabiliana na Crystal Palace na Man Utd mara mbili kila moja kwenye ratiba ya kipindi hiki.
Baada ya ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya West Ham United, Jumamosi iliyopita na Arsenal ilisafiri kwa maili 11.8 tu kwenye mechi hiyo ya ugenini, yenyewe inafahamu wazi inahitaji kumaliza pengo la pointi tisa katika kuwakimbizia vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool ili kuweka hai matumaini yao ya kuwapo mwenye mbio za ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Kwa ratiba yao ilivyo, Arsenal ina nafasi kubwa ya kupunguza pengo hilo la pointi kwenye mbio za ubingwa.
Katika kipindi hiki, vinara Liverpool wanaonolewa na Arne Slot kitasafiri kucheza na Newcastle, Girona, Southampton, West Ham, Nottingham Forest na Brentford - huku mechi zote hizo zikiipa miamba hiyo ya Anfield maili za kutosha kwenye kusafiri.