Tchouameni anaondoka, macho kwa Rodri
Muktasari:
- Real Madrid wanataka kumuuza mchezaji huyo ili kufanikiwa kupata fedha kwa ajili ya kufanya usajili mwingine mkubwa kwenye kikosi hicho kilichopo chini ya kocha mkuu Jose Mourinho ambaye anataka kuisuka timu hiyo upya ili iweze kuwania makombe makubwa duniani.
KLABU ya Real Madrid imesema ipo tayari kwa ajili ya kumuuza kiungo wake Aurelien Tchouameni kwenye kikosi cha Manchester United, ambacho kimeshaonyesha nia ya kumtaka.
Real Madrid wanataka kumuuza mchezaji huyo ili kufanikiwa kupata fedha kwa ajili ya kufanya usajili mwingine mkubwa kwenye kikosi hicho kilichopo chini ya kocha mkuu Jose Mourinho ambaye anataka kuisuka timu hiyo upya ili iweze kuwania makombe makubwa duniani.
Mourinho ameshasema kuwa mchezaji yoyote anayetaka kuondoka kwenye timu hiyo milango iko wazi na anachotakiwa kufanya ni kwenda ofisini kwake. Mmoja kati ya wachezaji ambao wanawindwa vikali na timu hiyo ni Rodri kutoka kwenye kikosi cha Manchester City akiwa alishafanya kazi kubwa akiwa na Manchester City.
Rodri ni mmoja kati ya wachezaji ambao walifanya vizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizopita ambapo Hispania ilifanikiwa kutwaa ubingwa mbele ya Argentina.
Rodri
REAL Madrid wanafanyia kazi mpango wa kumsajili kiungo wa Manchester City, Rodri. Klabu hiyo ya Hispania ina imani kuwa inaweza kufikia makubaliano ya kumnasa nahodha huyo wa timu ya taifa ya Hispania mwenye umri wa miaka 30.
Julian Alvarez
ARSENAL wanafikiria kufanya dili la kubadilishana mchezaji pamoja na fedha ili kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid na Argentina, Julian Alvarez (26).
Oscar Bobb
ROMA wanavutiwa kumsajili winga wa Norway, Oscar Bobb (23), kutoka Fulham, licha ya kwamba alijiunga na klabu hiyo kutoka Manchester City miezi sita tu iliyopita.
Yan Diomande
PARIS Saint-Germain (PSG) bado hawajawasilisha ofa rasmi ya pauni milioni 102 (euro milioni 120) kwa ajili ya kumsajili winga wa RB Leipzig kutoka Ivory Coast, Yan Diomande (19).
Bruno Guimaraes
OFA ya pauni milioni 70 ambayo Arsenal wamewasilisha kwa ajili ya Bruno Guimaraes inatarajiwa kukataliwa na Newcastle United, ingawa mchezaji huyo anaripotiwa kuwa na hamu ya kujiunga na The Gunners.
Bruno Fernandes
MANCHESTER United hawana mpango wa kumuuza nahodha wao Bruno Fernandes (31), licha ya tetesi zinazomhusisha kiungo huyo wa Ureno na kuondoka Old Trafford.
Trevoh Chalobah
COMO wanatarajiwa kukutana na Chelsea siku ya Jumamosi katika jitihada za kumsajili beki wa England, Trevoh Chalobah (27).
Kerim Alajbegovic
CHELESEA wamewasilisha ofa yao ya kwanza kwa ajili ya winga wa Bayer Leverkusen na Bosnia na Herzegovina, Kerim Alajbegovic (18).
Fabio Vieira
ARSENAL na Hamburg wanaendelea na mazungumzo kuhusu kiungo wa Ureno Fabio Vieira (26), ambaye anataka kujiunga na klabu hiyo ya Bundesliga baada ya kucheza kwa mkopo huko msimu uliopita.
Marcus Rashford
MSHAMBULIAJI wa England, Marcus Rashford (28), amealikwa kushiriki katika makala maalumu ya Amazon kuhusu maisha ya ndani ya Manchester United, jambo linaloashiria kuwa viongozi wa juu wa klabu hiyo bado wana nia ya kumbakisha Old Trafford.