Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ufaransa yaifuata Morocco robo fainali, Mbappe amkamata Messi

Muktasari:

  • Bao pekee la mchezo huo limefungwa na nahodha Kylian Mbappé kwa njia ya penalti dakika ya 66, ushindi uliowafanya mabingwa hao wa dunia mwaka 2018 kuifuata Morocco katika robo fainali.

Ufaransa imetinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Paraguay katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa usiku wa kuamkia leo Jumapili kwenye Uwanja wa Lincoln Financial Field.

Bao pekee la mchezo huo limefungwa na nahodha Kylian Mbappé kwa njia ya penalti dakika ya 66, ushindi uliowafanya mabingwa hao wa dunia mwaka 2018 kuifuata Morocco katika robo fainali.

Licha ya Ufaransa kumiliki mpira kwa zaidi ya asilimia 80 katika kipindi cha kwanza, lakini ilishindwa kabisa kupiga shuti lililolenga lango kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Paraguay iliyoongozwa na Julio Enciso na wenzake waliokuwa wakifanya kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji wa Les Bleus.

Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa na uliogubikwa na faulo nyingi pamoja na mvutano. Dakika za katikati ya kipindi cha kwanza Mbappé alionekana kukasirishwa baada ya kuchezewa faulo na Andrés Cubas, hali iliyosababisha mzozo uliowahusisha karibu wachezaji wote wa timu hizo mbili.

Baada ya mapumziko, kocha Didier Deschamps alifanya mabadiliko yaliyobadili kabisa sura ya mchezo huku Ufaransa ikianza kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga.

Kiungo Manu Koné alikuwa wa kwanza kujaribu bahati yake kwa shuti la mbali lililomlazimisha kipa Orlando Gill kufanya kazi ya ziada kuokoa hatari hiyo.

Dakika ya 60, Deschamps alimwingiza mshambuliaji Désiré Doué ambaye alikuja kuwa mchezaji muhimu katika ushindi huo.

Dakika sita baada ya kuingia, aliwapita mabeki watatu wa Paraguay kabla ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Diego Gómez.

Mwamuzi hakusita kuamuru penalti huku Mbappé akibeba jukumu la kuipiga. Nyota huyo wa Real Madrid aliupiga mpira kwa utulivu na kumshinda kipa Gill, akiifungia Ufaransa bao pekee.

Baada ya kupata bao hilo, Ufaransa ilibadili mbinu na kucheza kwa tahadhari zaidi, ikidhibiti mchezo huku Paraguay ikisukuma idadi kubwa ya wachezaji mbele kutafuta bao la kusawazisha.

Katika dakika za nyongeza, Mbappé alikaribia kufunga bao la pili lakini Orlando Gill aliokoa kwa ustadi mara mbili mfululizo na kuzuia ushindi huo usiwe mkubwa zaidi.

Matokeo hayo yanaifanya Ufaransa kutinga robo fainali, ambako itakutana na Morocco katika moja ya mechi zinazosubiriwa kwa hamu kubwa.

Kwa upande wa Paraguay, safari yao ya kuvutia katika Kombe la Dunia imefikia tamati, licha ya kuonyesha kiwango bora na kuipa wakati mgumu moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.

Beki wa Ufaransa William Saliba alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi baada ya kuiongoza safu ya ulinzi kwa umahiri na kusaidia timu yake kutunza ushindi muhimu wa bao 1-0.

Wakati huohuo, Mbappe bao lake hilo limemfanya kufikisha saba sawa na nyota wa Argentina, Lionel Messi katika orodha ya vinara wa ufungaji wa michuano hiyo kwa mwaka huu. Chini yao kuna Erling Haaland wa Norway na Harry Kane wa England wenye matano kila mmoja.

Bado Mbappe ana kazi ya ziada ya kufukuzana na Messi kwani wawili hao tofauti yao ni bao moja katika ile orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa mashindano hayo.

Messi ndiye kinara wa jumla kwani tangu aanze kucheza Kombe la Dunia mwaka 2006, amefikisha mabao 20 katika mechi 30, akifuatiwa na Mbappe aliyeanza kushiriki mwaka 2018 akifikisha mabao 19 katika mechi 19.

Awali kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia 2026, Miroslav Klose wa Ujerumani alikuwa akishikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote akiwa na mabao 16 katika mechi 24, lakini sasa anakamata nafasi ya tatu.