Namba zimemhukumu Julio Mashujaa
Muktasari:
- Baadhi ya watu wanaweza kushangaa uamuzi huo wa Mashujaa FC kuachana na Julio hasa ukizingatia ndiye ameiongoza timu hiyo kukwepa kushuka daraja.
TETESI ambazo kijiwe hiki kimezipata ni kwamba Mashujaa FC imeamua kutoendelea na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye ni kocha wake mkuu na sasa inasaka kocha mpya.
Hilo linatokea wiki mbili tangu Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-2026 ulipomalizika na Mashujaa FC ilikwepa janga la kushuka daraja baada ya kumaliza ikiwa katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Baadhi ya watu wanaweza kushangaa uamuzi huo wa Mashujaa FC kuachana na Julio hasa ukizingatia ndiye ameiongoza timu hiyo kukwepa kushuka daraja.
Hata hivyo, kwa tathimini tuliyoifanya hapa kijiweni, tumejiridhisha uongozi wa Mashujaa haujakosea kuchukua uamuzi huo kwani takwimu za kocha huyo kwenye ligi msimu uliomalizika hazivutii.
Katika pointi 33 ambazo Mashujaa FC imemaliza msimu ikiwa nazo, Julio ameiongoza kupata pointi 19 huku nyingine 14 zikiwa zimevunwa na mtangulizi wake Salum Mayanga.
Hata hivyo, tofauti na Mayanga ambaye pointi 14 alizivuna katika mechi 12, Julio yeye aliiongoza Mashujaa FC kukusanya pointi 19 katika idadi ya michezo 18.
Kwa hesabu za haraka haraka, Mayanga alikuwa na wastani wa kupata pointi 1.2 kwa mchezo na Julio alikuwa akipata wastani wa pointi 1.1 kwa mchezo.
Hiyo inamaanisha kwamba hakuna kitu cha kipekee au kikubwa ambacho Mashujaa FC ilikifanya ikiwa chini ya Julio kwani namba hazidanganyi na zinapingwa kwa namba au utafiti.