Wenye vita ya ubingwa England ni Liverpool, Arsenal
Muktasari:
- Na utamu unazidi baada ya sare ya Liverpool kwa Everton kuweka milango wazi kwa Arsenal.
LONDON, ENGLAND: MBIO za ubingwa kwenye Ligi Kuu England ni za farasi wawili, Liverpool na Arsenal.
Na utamu unazidi baada ya sare ya Liverpool kwa Everton kuweka milango wazi kwa Arsenal.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema: “Tutapambania hadi mwisho.”
Vita itakuwa ya vuta nikuvute kwenye mechi zao zijazo kabla ya kukutana wenyewe Mei.
Liverpool kwa sasa inaonekana kuwa bosi kwenye mbio hizo za ubingwa, lakini kuna sababu nyingi za kuamini kwamba vita yao na Arsenal itakwenda hadi mwisho wa msimu baada ya kikosi hicho cha kocha Arne Slot kuwa na siku nane muhimu za kuamua hatima ya msimu wao kwenye Ligi Kuu England.
Liverpool imeanza mchakamchaka wa mechi zake tatu ngumu kabisa kuanzia kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Aston Villa, Jumatano iliyopita.
Kisha itacheza na Manchester City na Newcastle United, kama itapoteza mechi zote hizo mbili na kisha Arsenal ikashinda mechi zake mbili zijazo na itacheza na West Ham United na Nottingham Forest - hiyo ina maana Arteta na chama lake atamaliza wiki ijayo akiwa nyuma ya Liverpool kwa pointi mbili na mechi moja mkononi.
Mechi hizo itakazocheza Liverpool ndani ya siku nane, zitaamua.
Arsenal inafahamu kilichowatokea nyuma, hivyo wanaamini chochote kinaweza kutokea, jambo wanalofanya ni kuhakikisha wanaendelea kuwapo kwenye eneo hilo la kuwabana wapinzani wao.
Huu ni msimu wa tatu mfululizo, Arsenal ipo kwenye mbio za ubingwa.
Hilo limewapa uzoefu wa kutosha namna ya kupambana licha ya kikosi chao kuwa la majeruhi ya wachezaji muhimu, Bukayo Saka, Kai Havertz na Gabriel Jesus.
Viwango vyao vipoje?
Liverpool imeangusha pointi katika mechi mbili kati ya tatu zilizopita, ilitoka sare na Everton na Aston Villa na ilishinda 2-1 dhidi ya Wolves.
Kwa kutolewa kwenye Kombe la FA na timu ya Championship, Plymouth Argyle, hiyo ina maana Liverpool imeshinda mechi moja tu kati ya nne za mwisho katika michuano yote.
Hiyo ni ishara kasi yao ya kushinda imeanza kushuka. Kwa kifupi tu, Liverpool imevuna pointi 11 kutoka kwenye mechi zao tano za Ligi Kuu England, wakati Arsenal imevuna pointi 13.
Arsenal imeshinda mechi tano kati ya sita zilizopita katika michuano yote, ilishindwa moja tu kwenye kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Newcastle kwenye Kombe la Ligi.
Ushindi huo kwenye mechi nyingi unashawishi kwa Arsenal kuwa vizuri kwenye mbio za ubingwa kuzidi Liverpool.
Arsenal imeruhusu bao moja tu katika mechi tatu za mwisho ilizocheza kwenye Ligi Kuu England na katika mechi tano zilizopita, imezichapa Tottenham, ambao ni mahasimu wao na Man City 5-1.
Ratiba zao zipoje?
Liverpool itakapomalizana na mechi ngumu za kuwakabili Man City na Newcastle, mambo yanaonekana kuwa mepesi kwenye karatasi. Kwanza watakuwa na muda wa kupumzika na Liverpool itacheza mechi moja tu ya Ligi Kuu England kwenye mwezi Machi.
Mechi tano kati ya sita itakazocheza kati ya Machi na Aprili dhidi ya timu zilizopo kwenye 10 la chini kwenye msimamo wa ligi, isipokuwa ile ya ugenini kwa Fulham, Aprili 5.
Lakini, watakuwa na kasheshe la Ligi ya Mabingwa Ulaya na fainali ya Kombe la Ligi, lakini baada ya hapo, itakuwa na shughuli mbele ya Chelsea, Arsenal na Brighton kabla ya kumalizana na Crystal Palace.
Arsenal ratiba yao inahitaji ujanja sana kushinda ili kuendelea kuchuana kwenye mchakamchaka wa ubingwa.
Wikiendi hii itakabiliana na West Ham - timu ambayo iliwatibulia kwenye mbio za msim uliopita na baada ya hapo itakabiliana na Nottingham Forest.
Kisha itakuwa na mechi ya ugenini kukabiliana na Manchester United, kabla ya kuwa na vipute viwili vya London derby mfululizo dhidi ya Chelsea na Fulham na baadaye kukabiliana na Everton iliyopamba moto kwa sasa tangu ilipomrudisha David Moyes kwenye benchi lao la ufundi.
Arsenal itakuwa na mechi 10 kabla ya safari yao ya kuifuata Liverpool uwanjani Anfield.