Watkins ajitoa sadaka dili la Sesko likikwama Man United
Muktasari:
- Man United ipo kwenye vita kali na Newcastle United juu ya mchezaji Sesko na miamba ya St James’ Park imeweka mezani Pauni 78 milioni ili kumnasa straika huyo kutoka RB Leipzig.
STRAIKA Ollie Watkins yupo tayari kwenda kuziba pengo endapo kama Manchester United itashindwa kumsajili Benjamin Sesko.
Man United ipo kwenye vita kali na Newcastle United juu ya mchezaji Sesko na miamba ya St James’ Park imeweka mezani Pauni 78 milioni ili kumnasa straika huyo kutoka RB Leipzig.
Taarifa za Ujerumani zinafichua Newcastle inaweza kushinda kwenye vita hiyo ya kumsajili Sesko, ikimwandaa akachukue mikoba ya Alexander Isak, ambaye anaweza kuondoka kwa pesa ndefu dirisha hili.
Lakini, jambo hilo linamwibua Watkins, ambaye sasa anadhani umefika wakati wa kuachana na Aston Villa na kuwa tayari kwenda kukipiga Old Trafford kama mbadala wa Sesko endapo kama kocha Ruben Amorim atashindwa kumsajili.
Aston Villa ipo tayari kuuza ili kuweka sawa vitabu vyake vya hesabu. Miamba hiyo inayonolewa na kocha Unai Emery, mapema dirisha hili ilikumbana na faini ya Uefa kutokana na kukiuka kanuni za matumizi.
Villa ilifungua milango ya kupokea ofa za mastaa kama Jacob Ramsey na Leon Bailey ili kwenda sambamba na mahitaji ya Ligi Kuu England kwenye matumizi, lakini sasa hadi hakuna ofa yoyote ya kuwahusu mastaa hao.
Badala yake, inaweza kuvuna Pauni 40 milioni au Pauni 50 milioni kwenye mauzo ya Watkins, ambaye amekuwa kwenye rada za Man United dirisha hili.
Kiwango hicho cha pesa kitakuwa bonasi pia kwa Man United kwa sababu itakuwa na pesa nyingine zimebaki kusajili maeneo mengine, ikiwamo kiungo mkabaji kuliko kulipa zaidi ya Pauni 70 milioni kwa straika Sesko.
Yves Bissouma
TOTTENHAM inataka kumuuza kiungo wao wa kimataifa wa Mali, Yves Bissouma, 28, ili kuachia nafasi kwa kiungo wa zamani wa Chelsea, Conor Gallagher, 25, ambaye kwa sasa yupo Atletico Madrid. Gallagher aling’ara akiwa Chelsea msimu wa 2022/23 kabla hajanunuliwa na Atletico kwa Euro 42 milioni. Spurs ipo tayari kulipa Pauni 30 milioni ili kukamilisha uhamisho wa fundi huyu lakini mabosi wa Atletico wamegoma na wanahitaji Pauni 40 milioni.
Nathan Collins
LIVERPOOL inamfuatilia kwa karibu beki wa kati wa Brentford na timu ya taifa ya Ireland, Nathan Collins, 24, ili kumsajili dirisha hili la majira ya kiangazi. Collins aliyecheza mechi 30 za Ligi Kuu England msimu uliopita ni mmoja wa mabeki waliowekwa kwenye rada za Liverpool tangu kuanza dirisha hili kuimarisha safu yao ya ulinzi. Nathan mwenyewe ameshawasilisha maombi ya kutaka kuondoka baada ya kuona Liverpool inamhitaji.
John Victor
WEST Ham imewasilisha ofa mpya ya Pauni 10 milioni kwenda Botafogo ili kumsajili kipa wa timu hiyo, Mbrazili, John Victor, 29, dirisha hili. Kipa huyo ambaye msimu huu unaoendelea amecheza mechi 33 ligi ya Brazil (Brasileirao), amemaliza 11 kati ya hizo bila ya kuruhusu bao. Pia aliivutia sana West Ham kutokana na kiwango alichoonyesha katika michuano ya Kombe la Dunia la klabu.
Rasmus Hojlund
BAYER Leverkusen imeingia katika hatakati za kumsajili mshambuliaji wa Manchester United, Rasmus Hojlund, 22, lakini inakutana na ushindani kutoka AC Milan, Inter Milan na Juventus. Hojlund alifunga mabao 10 EPL msimu uliopita lakini haonekani kuaminika sana na Kocha Ruben Amorim ambaye ameshatoa ombi kwa mabosi wa mashetani hao wekundu anahitaji mshambuliaji mwingine.
Jean Philippe Mateta
ATALANTA inaweza kumgeukia mshambuliaji wa Crystal Palace, Jean-Philippe Mateta, 28, ikiwa itashindwa kufikia makubaliano na Fulham kuhusu mshambuliaji Rodrigo Muniz, 24. Mabosi wa Atalanta wanatafuta mshambuliaji ili kuziba pengo la Ademola Lookman ambaye ipo tayari kumuuza katika dirisha hili. Mateta alifunga mabao 12 Ligi Kuu England msimu uliopita, na amekuwa akivutia klabu nyingi.
Ruben Dias
BEKI wa kati wa Manchester City, Ruben Dias, 28, yuko mbioni kuongeza mkataba wa kuendelea kusalia Manchester licha ya kuwa bado na miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa. Tangu atue Man City mwaka 2020, Dias amecheza mechi 169 za michuano yote na amekuwa nguzo muhimu kwenye safu ya ulinzi ya Pep Guardiola.
Julian Ryerson
KUNA vita kali inaendelea kati ya Sunderland na Wolves juu ya kuiwania saini ya beki wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Norway, Julian Ryerson 27, katika dirisha hili. Ryerson ambaye msimu uliopita alicheza mechi 22 za Bundesliga inadaiwa anauzwa kwa Pauni 10 milioni. Wolves na Sunderland zimekuwa zikijaribu kuishawishi Dortmund ikubali kupunguza bei.