Marekani kuwania uenyeji wa Kombe la Dunia 2038
Muktasari:
- Huku Hispania ikitwaa ubingwa kwa kuifunga Argentina katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa MetLife, New York, macho sasa yamehamia kwenye mustakabali wa mashindano hayo.
MIAMI, MAREKANI: MAREKANI inaweza kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2038, licha ya kuwa imehitimisha hivi karibuni kuandaa mashindano ya mwaka 2026 kwa ushirikiano na Canada na Mexico.
Huku Hispania ikitwaa ubingwa kwa kuifunga Argentina katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa MetLife, New York, macho sasa yamehamia kwenye mustakabali wa mashindano hayo.
Tayari FIFA imeshatangaza waandaaji wa Kombe la Dunia la 2030 na 2034, lakini dalili zinaonyesha Marekani imeibuka kama mgombea mwenye nguvu wa kuandaa toleo la mwaka 2038.
Iwapo itafanikiwa, itakuwa mara ya kwanza kwa taifa kuandaa Kombe la Dunia mara mbili ndani ya kipindi cha miaka 12.
MFUMO WA MZUNGUKO WA FIFA WAIFUNGULIA NJIA MAREKANI
Kwa mujibu wa sera ya mzunguko wa FIFA, shirikisho la bara ambalo limeandaa mashindano katika matoleo mawili yaliyopita kwa kawaida halipewi nafasi ya kuandaa tena, ingawa si sheria ya lazima.
Kombe la Dunia la 2030 litaandaliwa kwa pamoja na Hispania, Ureno na Morocco, huku Argentina, Uruguay na Paraguay zikipokea mechi moja moja maalumu kuadhimisha miaka 100 tangu kufanyika kwa Kombe la Dunia la kwanza mwaka 1930.
Kutokana na mpangilio huo, mabara ya Ulaya (UEFA), Afrika (CAF) na Amerika Kusini (CONMEBOL) yanaweza kukosa nafasi ya kuandaa matoleo mawili yanayofuata.
Kwa upande wa Kombe la Dunia la 2034, ushindani ulihusisha mataifa ya Asia na Oceania pekee kabla ya Australia kujiondoa na kuiachia Saudi Arabia kupewa uenyeji bila mpinzani.
Hali hiyo inaacha CONCACAF (Marekani, Canada, Mexico na mataifa ya Amerika ya Kati na Karibiani) pamoja na AFC kama washindani wakuu wa kuandaa Kombe la Dunia la 2038.
MAREKANI YAIVUTIA FIFA
Baada ya FIFA kuvunja rekodi ya mapato kupitia mauzo ya tiketi na huduma za ukarimu katika Kombe la Dunia la 2026, Marekani inaonekana kuwa chaguo linaloweza kuiletea faida kubwa zaidi.
Rais wa Marekani, Donald Trump, tayari ameonyesha nia ya kuona mashindano hayo yakirejea nchini humo haraka iwezekanavyo.
"Kutokana na mafanikio ya mwaka huu, tutawasilisha ombi mara moja. Tunapaswa kuandaa tena mashindano haya, na nataka yafanyike wakati bado nipo hapa, unasikia Gianni (Infantino)?" alisema Trump kabla ya fainali ya 2026.
Uhusiano wa karibu kati ya Trump na Rais wa FIFA, Gianni Infantino umeendelea kuzua mjadala, jambo linalowafanya wengi kuamini kuwa Marekani inaweza kuwa na nafasi nzuri katika mbio hizo.
ENGLAND BADO YASUBIRI
Wakati Marekani ikitajwa kuwa mbele kwenye mbio za 2038, England bado haijaandaa Kombe la Dunia tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 1966.
Iwapo Marekani itapewa uenyeji wa 2038, itakuwa imeandaa Kombe la Dunia mara tatu ndani ya kipindi cha miaka 44, jambo ambalo litakuwa rekodi nyingine katika historia ya mashindano hayo.