Warriors wanahitaji nini ili kumjengea Curry timu ya ubingwa?
Muktasari:
- Suala hilo limezidi kuwa wazi baada ya Curry mwenye umri wa miaka 38, kupewa mkataba mpya wa miaka miwili wenye thamani ya hadi dola milioni 136.7, ambao unaweza kumfanya abaki Warriors hadi majira ya kiangazi ya mwaka 2029.
SAN FRANCISCO, MAREKANI: SWALI kubwa linaloikabili Golden State Warriors kwa sasa ni kama klabu hiyo bado inaweza kujenga kikosi chenye uwezo wa kutwaa ubingwa wa NBA kikimzunguka nyota wake, Steph Curry au muda wa kufanya hivyo umeanza kuisha.
Suala hilo limezidi kuwa wazi baada ya Curry mwenye umri wa miaka 38, kupewa mkataba mpya wa miaka miwili wenye thamani ya hadi dola milioni 136.7, ambao unaweza kumfanya abaki Warriors hadi majira ya kiangazi ya mwaka 2029.
Lakini licha ya fursa hiyo, Curry hajaonyesha haraka ya kuweka saini kwenye mkataba huo.
Kwa mtazamo wa kwanza, hatua hiyo inaweza kuonekana kama mbinu ya mazungumzo ya kimkataba. Lakini kwa undani zaidi, inaonekana kuna jambo kubwa zaidi nyuma yake.
Curry anataka kuona mpango wa Warriors wa kurejea kileleni.
Msimu uliopita, Golden State ilikosa nafasi ya kucheza Playoffs kwa mara ya pili katika misimu mitatu baada ya kufungwa na Phoenix Suns katika hatua ya Play-In.
Timu iliyokuwa ikitawala NBA kwa miaka kadhaa sasa imegeuka kuwa klabu inayotafuta majibu, huku muda ukiwa rasilimali muhimu zaidi waliyonayo.
Curry, ambaye ni bingwa mara nne wa NBA, alicheza mechi 41 pekee msimu uliopita kutokana na majeraha. Hilo ni ukumbusho kwamba hata mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga kwa mipira ya mbali katika historia ya NBA hawezi kukwepa athari za umri.
Akiwa fiti, Curry bado ni miongoni mwa wachezaji bora kabisa wa ligi. Lakini Warriors hawawezi tena kuendelea kufanya kazi kana kwamba wana nafasi zisizo na mwisho za kujaribu kutwaa ubingwa mwingine.
WARRIORS WASIMUUZE CURRY
Jibu la kwanza ni rahisi: Warriors hawapaswi kumuuza Curry.
Kumuuza hakutatua tatizo lolote la msingi linaloikabili klabu hiyo.
Hata kama Golden State ingepokea idadi kubwa ya chaguo za Draft na wachezaji vijana wenye vipaji, hatua hiyo ingekuwa ishara ya mwisho wa enzi iliyokuwa na mafanikio makubwa zaidi katika historia ya klabu.
Curry si tu sura ya Warriors; bado ndiye mchezaji wao muhimu zaidi.
Akiwa fiti, bado ana uwezo wa kuibeba safu ya ushambuliaji, kuvuta ulinzi wa wapinzani kwa kiwango ambacho ni wachezaji wachache sana katika historia ya NBA wamewahi kufanya na kubadili kabisa mwelekeo wa mfululizo wa Playoffs kwa uwezo wake wa kufunga.
Zaidi ya yote, Curry amefanya vya kutosha kupewa nafasi ya kuamua namna sura hii ya mwisho ya safari yake itakavyokuwa.
Kwa hiyo, isipokuwa yeye mwenyewe aombe kuondoka, Warriors wanapaswa kuendelea kujenga timu inayomzunguka.
TATIZO SI CURRY, NI WANAOMZUNGUKA
Tatizo si kwamba Curry hawezi tena kuwa mhimili wa timu inayowania ubingwa.
Tatizo ni kwamba wachezaji wanaomzunguka hawajawa na ubora unaohitajika.
Warriors wanahitaji nyota mwingine mkubwa na hapa ndipo changamoto inapoanzia.
TIMU ZA UBINGWA ZA WARRIORS
Historia inaonyesha wazi. Kulikuwa na Klay Thompson akiwa katika ubora wake. Kulikuwa na Draymond Green aliyeiongoza safu ya ulinzi.
Kulikuwa pia na Kevin Durant, aliyekuwa sehemu ya timu iliyotwaa mataji mawili.
Katika ubingwa wa 2022, kulikuwa na Andrew Wiggins, ambaye alicheza moja ya vipindi bora zaidi vya maisha yake ya kikapu.
Warriors ya sasa haina mchezaji wa kiwango hicho cha pili.
Kikosi kina wachezaji wenye vipaji, lakini hakina nyota mwingine mwenye uwezo wa kudumu katika kiwango cha All-NBA na kuchukua sehemu kubwa ya mzigo wa Curry.
Hilo ndilo linapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza cha uongozi wa Warriors.
Iwe kupitia biashara ya wachezaji au kumsajili nyota mkubwa kupitia soko la wachezaji huru, Golden State inahitaji mchezaji anayeweza kuunda nafasi na mashambulizi, kufunga kwa ufanisi na kuibeba timu pale Curry anapokuwa benchi au akikosa mechi.
MUDA WA WARRIORS UNAYOYOMA
Warriors bado wana Curry mwenye uwezo wa kubadili mchezo, lakini umri wake unafanya kila msimu kuwa muhimu zaidi.
Hawahitaji kuanza upya.Hawahitaji kumuuza Curry.Wanahitaji kumpa mshirika mwingine wa kiwango cha juu.
Ikiwa Golden State itafanikiwa kupata nyota huyo na kujenga kikosi kinachoweza kumlinda Curry dhidi ya mzigo mkubwa wa msimu mzima, bado inaweza kuwa tishio katika NBA.
Lakini bila kufanya hivyo, swali la kama Curry anaweza kuiongoza Warriors tena kwenye ubingwa litaendelea kuwa kubwa na huenda muda wa kulijibu ukawa mfupi kuliko wanavyofikiria.