Prime
Manqoba ashusha mkwara mzito
YANGA imeanza msimu wa Ligi Kuu Bara kwa kiwango bora baada ya kushinda mechi zake tano za kwanza na kuvuna pointi zote 15. Sasa hesabu zao zimehamia kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, huku kocha wa mabingwa hao wa Tanzania, Manqoba Mngqithi, akitoa kauli inayoweza kuwapa presha wapinzani wao.
Yanga imeondoka jana kuelekea Botswana kwa ajili ya mchezo huo, safari ambayo itapitia Afrika Kusini kabla ya kutua jijini Gaborone, tayari kwa mchezo wa hatua ya awali ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Septemba 5, 2026.
Hapa nchini, Yanga imeonyesha ubabe mkubwa baada ya kushinda mechi zote tano za mwanzo, huku ikionyesha kiwango bora chini ya kocha huyo aliyeanza msimu kwa kasi na kuiongoza timu hiyo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 15.
Akizungumzia mchezo huo dhidi ya Gaborone United, Manqoba amesema kikosi chake kipo tayari kwa mtihani huo na tayari wamefanya maandalizi ya kutosha, ikiwamo kuifahamu aina ya timu watakayokutana nayo na kila kitu kipo mikononi mwao sasa.
Manqoba amesema wanafahamu kuwa wanakwenda kukutana na timu nzuri ambayo ilifanya vizuri msimu uliopita nchini Botswana, lakini akasisitiza kuwa kikosi chake hakiendi kucheza kwa kujilinda.
Kocha huyo amesema kikosi chake kitaenda kutafuta ushindi katika mchezo huo badala ya kukaa nyuma na kuwaruhusu wapinzani wao kuwashambulia, akieleza kuwa wanataka kupata matokeo yatakayowarahisishia mchezo wa marudiano.
“Nadhani kazi ya kuijua timu tunayokwenda kukutana nayo imeshafanyika. Tunajua ni aina gani ya hesabu tunazotakiwa kuzifanya ili tuweze kuanza vizuri kampeni ya mashindano haya makubwa Afrika. Kumbuka kila timu unayokutana nayo huku imefanya vizuri,” amesema Manqoba.
“Mimi si kocha ambaye nahusudu soka la kujilinda. Lengo letu la kwanza ni kutafuta ushindi bila kujali tunacheza nyumbani au ugenini. Tutakwenda na akili hiyo, lakini tutakuwa imara kuhakikisha hatuwapi nafasi wapinzani kutupa shida.
“Nilisema awali kwamba huwa nachukia timu inaporuhusu bao. Napenda sana umakini katika eneo letu la ulinzi. Nimefurahi katika mechi zetu tatu zilizopita tumekuwa na mabadiliko katika eneo la ulinzi na hatujaruhusu bao.”
Aidha, Manqoba ameongeza anaondoka na wachezaji wote waliofiti kucheza, huku akithibitisha kwa sasa hawana mchezaji mpya mgonjwa.
“Tutaondoka na timu kamili ambayo kila mchezaji akipewa nafasi ataweza kucheza. Ninachofurahi na kushukuru ni mpaka sasa hatuna mchezaji ambaye unaweza kusema ameumia hivi karibuni na anaweza kuwa nje, tunakwenda kutafuta ushindi na siyo vinginevyo na uwezo huo naamini tunao,” amesema.