Usajili huu: wapinzani wa Arsenal wataweza kuwapoka Taji?
Muktasari:
- The Gunners walikuwa watulivu katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili, baada ya kukamilisha shughuli zao mapema. Kinyume chake, wapinzani wao wakuu walitumia fedha nyingi kuimarisha vikosi vyao kwa lengo la kuizuia Arsenal kutwaa tena taji hilo.
LONDON, ENGLAND; ARSENAL imeanza msimu mpya wa Ligi Kuu England kwa ushindi katika mechi zake mbili za kwanza, huku dirisha la usajili likifungwa ikiwaacha wakiwa katika hali nzuri ya kuendeleza ubabe wao na kutetea ubingwa walioutwaa msimu uliopita.
The Gunners walikuwa watulivu katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili, baada ya kukamilisha shughuli zao mapema. Kinyume chake, wapinzani wao wakuu walitumia fedha nyingi kuimarisha vikosi vyao kwa lengo la kuizuia Arsenal kutwaa tena taji hilo.
Swali kubwa sasa ni moja: Je, Arsenal bado ndiyo timu yenye nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa, au wapinzani wake wamefanya usajili wa kutosha kuwang'oa kileleni?
ARSENAL: BADO TIMU YA KUIANGALIA
Arsenal ilijaribu kumsajili mshambuliaji wa Argentina, Julian Alvarez kutoka Atletico Madrid, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.
The Gunners walitaka kumshawishi Alvarez kuachana na mpango wake wa kujiunga na Barcelona, lakini Atletico ilizuia kwa nguvu zote mpango huo. Arsenal iliendelea kuwa na matumaini kwamba mchezaji huyo angeamua kuondoka, hasa ikiwa Barcelona isingeweza kukamilisha dili.
Hata hivyo, hakuna makubaliano yaliyofikiwa.
Na huenda hilo likawa eneo pekee linaloleta maswali kuhusu ubora wa kikosi cha Arsenal, je, wana mshambuliaji wa uhakika wa kuendeleza kiwango cha kufunga mabao kwa msimu mzima?
Katika maeneo mengine, Arsenal inaonekana imara. Baada ya kuifunga Coventry City na kupata ushindi ugenini dhidi ya Aston Villa katika mechi zake mbili za mwanzo, kikosi cha Mikel Arteta bado kinaonekana kuwa timu ya kuishinda.
Bruno Guimaraes, aliyesajiliwa kutoka Newcastle United kwa pauni milioni 75, alionyesha ishara za kile atakachokiongeza baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Aston Villa.
Uwezo wake wa kutoa pasi zinazopenya safu ya ulinzi pamoja na ushindani wake mkubwa uwanjani ni nyongeza muhimu kwa Arsenal.
Beki wa England, Ezri Konsa naye ameongeza ubora mkubwa kwenye safu ya ulinzi baada ya kuwasili akitokea Aston Villa. Christos Tzolis, licha ya kuwa na usiku mgumu dhidi ya Villa na kutolewa mapema kipindi cha pili, tayari ameonyesha anaweza kuwa chaguo muhimu upande wa kushoto.
Kwa sasa, Arsenal bado inaonekana kuwa timu iliyojiandaa vizuri zaidi kutwaa tena ubingwa.
MANCHESTER CITY: WAMEFANYA USAJILI WA KUTOSHA?
Manchester City pia imeanza kwa kasi, huku ikiifunga na Arsenal katika Ngao ya Jamii na kisha kufanya moja ya madirisha makubwa zaidi ya usajili katika historia yake.
Klabu hiyo imepitia mabadiliko makubwa baada ya Pep Guardiola kuondoka baada ya miaka 10 na nafasi yake kuchukuliwa na Enzo Maresca.
Pia, imewapoteza baadhi ya mastaa waliokuwa sehemu ya mafanikio yake makubwa, akiwamo Rodri, Bernardo Silva, John Stones na Jack Grealish, pamoja na Savio, Omar Marmoush, Nico Gonzalez, James Trafford, Nathan Ake na Tijjani Reijnders.
Lakini kiu ya kurejea kileleni bado ipo.
City imetumia nguvu kubwa sokoni, ikilipa pauni milioni 125 kumsajili Enzo Fernandez na kumrejesha chini ya uongozi wa Maresca. Kabla ya hapo, ilitumia pauni milioni 116 kumnunua kiungo wa England, Elliot Anderson, kutoka Nottingham Forest.
Pia ilimsajili Iliman Ndiaye kutoka Everton kwa pauni milioni 65, kinda wa Morocco mwenye miaka 18, Ayyoub Bouaddi, kutoka Lille kwa pauni milioni 85.6, pamoja na Allan Elias kutoka Palmeiras ya Brazil.
Kwa ujumla, ni ujenzi upya mkubwa wa kikosi.
Usajili wa Fernandez umeifanya City kufikisha matumizi ya pauni milioni 458 katika dirisha hili pekee ni rekodi mpya ya matumizi ya klabu ya Ligi Kuu England katika dirisha moja, ikivunja rekodi ya Liverpool ya pauni415 milioni iliyowekwa msimu uliopita.
Hata hivyo, City pia imeuza wachezaji wenye thamani ya takribani pauni milioni 300, jambo linaloonyesha ukubwa wa mabadiliko yanayoendelea katika mwanzo wa enzi ya baada ya Guardiola.
Ni dirisha lililojaa matukio, lakini kwa kuzingatia ubora ambao bado upo kikosini, Manchester City inaonekana kuwa tishio kubwa kwa Arsenal katika mbio za ubingwa.
CHELSEA: KIKOSI KINACHOWAPA MATUMAINI
Chelsea inaweza kuwa imempoteza Enzo Fernandez kwa Manchester City kwa pauni milioni 125 katika saa za mwisho za dirisha, lakini kazi kubwa iliyofanyika kipindi hiki cha usajili bado inampa matumaini kocha mpya Xabi Alonso.
Alonso ameanza kwa ushindi katika mechi mbili za Ligi Kuu, huku kiwango cha kipa Robert Sanchez katika ushindi wa kwanza dhidi ya Fulham kikimshawishi kocha huyo kutatua tatizo la muda mrefu kwa kumsajili Emiliano Martinez kutoka Aston Villa.
Kama ilivyo kawaida kwa Chelsea, orodha ya wachezaji waliosajiliwa na walioondoka ni ndefu.
Morgan Rogers, aliyesajiliwa kutoka Aston Villa kwa pauni milioni 117, tayari ameunda safu hatari ya ushambuliaji pamoja na Cole Palmer na Joao Pedro.
Maxence Lacroix naye ameongeza ubora katika safu ya ulinzi.
Chelsea pia imebadili mkakati kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu, Jordan Henderson na Danny Welbeck, ambao wameongezwa ili kuleta uzoefu, nidhamu na weledi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Katika saa za mwisho, Chelsea ilijaribu pia kumsajili kiungo wa Monaco, Lamine Camara, lakini klabu hiyo ya Ufaransa ilisitisha mpango huo.
Chelsea haina michuano ya Ulaya msimu huu, hivyo itakuwa na muda mwingi wa kujiandaa kwa mechi za ligi.
Kikosi chake kina ubora wa kutosha kuwasumbua wapinzani, ingawa kwa sasa bado haipewi nafasi kubwa kama Arsenal na Manchester City katika mbio za ubingwa.
LIVERPOOL: TATIZO LA KIUNGO BADO LIPO
Baada ya kumteua Andoni Iraola kuchukua nafasi ya Arne Slot, Liverpool iliingia sokoni ikiwa na jukumu kubwa la kutafuta namna ya kufidia pengo la Mohamed Salah, aliyeondoka Anfield mwishoni mwa msimu uliopita.
Bradley Barcola alikuwa mmoja wa walengwa wakuu na hatimaye Liverpool ilimsajili kutoka Paris Saint-Germain kwa pauni milioni 123.
Ana kasi, ubunifu na uwezo wa kufunga mabao, lakini si mbadala wa moja kwa moja wa Salah kwa sababu anapendelea kucheza upande wa kushoto.
Victor Munoz, ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Hispania kilichoshinda Kombe la Dunia, pia amewahi kuonyesha uwezo wake baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa ustadi katika sare ya 2-2 dhidi ya Nottingham Forest.
Badala ya kutafuta mchezaji mmoja wa kuchukua nafasi ya Salah, Liverpool imeonekana kuchagua mkakati wa kusambaza jukumu la kufunga mabao kwa wachezaji wa pembeni na maeneo mengine.
Lakini sare dhidi ya Newcastle United na Forest imeibua tatizo ambalo liliigharimu Liverpool msimu uliopita.
Ukosefu wa kiungo wa asili wa namba sita bado umeacha pengo kubwa katikati ya uwanja, jambo linaloifanya timu kuwa rahisi kushambuliwa kwa mipira ya kushtukiza.
Timu pinzani bado zinaweza kupenya moja kwa moja katikati ya Liverpool, lakini Iraola hakuonyesha nia ya kusajili mchezaji wa aina hiyo katika dirisha hili.
Iwapo Liverpool haitatatua udhaifu huo, hilo linaweza kuwa tatizo litakalowazuia kurejesha ubingwa baada ya msimu uliopita wa kusikitisha katika utetezi wa taji.
MANCHESTER UNITED: BADO SI TISHIO LA UBINGWA
Baada ya kuimarisha safu ya ushambuliaji msimu uliopita kwa kumsajili Benjamin Sesko, Bryan Mbeumo na Matheus Cunha, Manchester United ililenga zaidi kuimarisha kiungo katika dirisha hili.
Youri Tielemans, Andrey Santos na Carlos Baleba wamewasili Old Trafford kwa lengo la kuongeza ubora katikati ya uwanja.
Lakini je, hiyo inatosha kuifanya United kuwa mshindani wa kweli wa ubingwa?
Inaonekana bado haitoshi.
Michael Carrick aliiongoza United kumaliza katika nafasi ya tatu na kurejea Ligi ya Mabingwa msimu uliopita baada ya kuchukua nafasi ya Ruben Amorim kwa muda, na sasa amepewa jukumu hilo kwa kudumu.
Hata hivyo, mwanzo wa msimu umechanganyika.
United ilipoteza dhidi ya Hull City iliyopanda daraja kabla ya kupata ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Ipswich Town.
Klabu hiyo iliamua kutofanya usajili mwingine wa dakika za mwisho, hivyo kikosi cha Carrick kinaonekana zaidi kuwa na uwezo wa kupigania nafasi nne za juu kuliko kupambana moja kwa moja na Arsenal katika mbio za ubingwa.
TOTTENHAM: FEDHA ZIMETUMIKA, LAKINI MATOKEO?
Tottenham Hotspur imekuwa miongoni mwa timu zilizotumia fedha nyingi zaidi katika dirisha hili, ikitumia zaidi ya pauni milioni 300.
Lakini matokeo ya mwanzo hayajaendana na ukubwa wa uwekezaji huo.
Spurs imepoteza mechi mbili za ligi, dhidi ya Brentford ugenini na Newcastle United nyumbani.
Kocha Roberto De Zerbi amepewa sapoti kubwa na uongozi wa klabu, hadi katika siku ya mwisho ya dirisha alipata mchezaji aliyekuwa akimhitaji ya Mykhailo Mudryk, ambaye aliwahi kufanya kazi chini yake Shakhtar Donetsk.
Mudryk alimaliza suala lake la kesi ya dawa za kusisimua misuli na Chama cha Soka England mwezi Julai, lakini hajacheza mechi ya ushindani tangu Novemba 2024.
Sasa jukumu kubwa la De Zerbi ni kuwaunganisha wachezaji hao wapya, wakiwemo 10 waliowasili hadi Tosin Adarabioyo kutoka Chelsea, na kuunda timu yenye mfumo mmoja.
Kikosi kina vipaji na matumaini makubwa, lakini changamoto kubwa zaidi kwa De Zerbi ni kuiondoa Tottenham katika hali ya kushindwa iliyowafanya kumaliza nafasi ya 17 katika misimu miwili iliyopita.
ASTON VILLA: MWANZO WA ENZI MPYA
Aston Villa ilimaliza nafasi ya nne na kutwaa Europa Ligi katika msimu uliopita uliokuwa wa mafanikio makubwa chini ya Unai Emery.
Lakini msimu huu unaonekana kuwa mwanzo wa enzi mpya Villa Park.
Villa imewapoteza baadhi ya wachezaji wake muhimu, akiwemo kipa Emiliano Martinez, mabeki Lucas Digne na Ezri Konsa, viungo Morgan Rogers na Youri Tielemans, pamoja na mshambuliaji Ollie Watkins.
Kipa wa Japan, Zion Suzuki, amechukua nafasi ya Martinez, huku Villa pia ikimsajili beki Taylor Harwood-Bellis kutoka Southampton, Aaron Wan-Bissaka kwa mkopo kutoka West Ham United na Matteo Ruggeri kutoka Atletico Madrid.
Kiungo wa Freiburg na timu ya taifa ya Uswisi, Johan Manzambi, pia amewasili, pamoja na winga Ibrahim Mbaye kutoka Paris Saint-Germain, mshambuliaji Nicolas Jackson kutoka Chelsea na kiungo mkongwe wa Ujerumani, Leon Goretzka.
Ujenzi huo uliendelea kwa kuwasili kwa kiungo Joao Gomes kutoka Wolverhampton Wanderers na winga Alejandro Garnacho kwa mkopo kutoka Chelsea.
Hata kocha mwenye uwezo mkubwa wa kubadilisha timu kama Emery atahitaji muda kuunganisha vipande hivyo vipya.
Hata hivyo, amepewa vifaa vya kutosha vya kuunda timu nyingine yenye ushindani.
Lengo la Villa msimu huu linaonekana kuwa kurejea katika nne bora na si lazima kuingia moja kwa moja kwenye vita ya ubingwa.