Wakifunga hawa, timu haipotezi
Muktasari:
- Lakini, kuna wachezaji hao, wamekuwa na zali la mentali kwenye Ligi Kuu England, kwamba hawajawahi kupoteza mechi yoyote ya ligi hiyo, ambayo wao walitikisa nyavu. Wapo wengi, lakini makala haya yanakuletea watano waliocheza mechi nyingi bila ya kupoteza katika michezo ambayo wao walitikisa nyavu kwenye Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: KWA kawaida, mchezaji kufunga mabao kunasaidia timu yake kushinda mechi.
Lakini, kuna wachezaji hao, wamekuwa na zali la mentali kwenye Ligi Kuu England, kwamba hawajawahi kupoteza mechi yoyote ya ligi hiyo, ambayo wao walitikisa nyavu. Wapo wengi, lakini makala haya yanakuletea watano waliocheza mechi nyingi bila ya kupoteza katika michezo ambayo wao walitikisa nyavu kwenye Ligi Kuu England.
5. Salomon Kalou
Amefunga: Mechi 32
Matokeo: Ushindi 29, sare 3
Salomon Kalou ni mchezaji mwingine aliyekuwa na rekodi tamu kabisa inayokuja michuano ya Ligi Kuu England. Alipokuwa kwenye kikosi cha Chelsea kwa miaka sita, mkali huyo wa kimataifa wa zamani wa Ivory Coast alishinda taji moja la Ligi Kuu England. Lakini, rekodi tamu kuhusu yeye ni kwamba kwenye mechi ambazo alifunga, Chelsea haijapoteza na alifanya hivyo kwenye mechi 32, Chelsea ilishinda 29 na sare ni tatu.
4. Gabriel Martinelli
Amefunga: Mechi 35
Matokeo: Ushindi 29, sare5
Unaweza kuona namna Gabriel Martinelli asivyokubalika sana na mashabiki wa Arsenal, lakini ukweli ni kwamba Mbrazili huyo amekuwa na rekodi tamu kabisa linapokuja suala la matokeo ya miamba hiyo ya Emirates. Utamu wa Martinelli kwenye kikosi cha Arsenal ni kwamba kwenye mechi zote za Ligi Kuu England, ambazo winga huyo alifunga, kikosi hicho cha Emirates hakijawahi kupoteza, imeshinda 29 na sare tano.
3. Diogo Jota
Amefunga: Mechi 50
Matokeo: Ushindi 42, sare 8
Staa wa Liverpool, Diogo Jota amefunga kwenye mechi 50 tofauti kwenye Ligi Kuu England, ambazo hakupoteza mchezo hata mmoja katika mechi hizo.
Alipokuwa chini ya kocha Jurgen Klopp kwenye kikosi cha Liverpool, Jota alifunga kwenye mechi 34 tofauti na hakupoteza hata moja, wakati chini ya Arne Slot amefunga kwenye mechi nne, ambazo hakupoteza. Jota alifunga kwenye mechi 12 tofauti alipokuwa Wolves.
2. James Milner
Amefunga: Mechi 54
Matokeo: Ushindi 43, sare 11
James Milner amekuwa na rekodi mbalimbali linapokuja suala la ushiriki wake kwenye Ligi Kuu England. Kwa sasa staa huyo yupo kwenye kikosi cha Brighton. Lakini, rekodi zake zinaonyesha kwenye Ligi Kuu England, amefunga kwenye mechi 54 tofauti, akifanya hivyo kwenye vikosi vya Leeds United, Newcastle, Aston Villa, Manchester City na Liverpool. Na Milner hajawahi kupoteza mechi ambayo alifunga, ameshinda 54, sare 11.
- Gabriel Jesus
Amefunga: Mechi 62
Matokeo: Ushindi 57, sare 5
Ukiweka kando medani nne za ubingwa wa Ligi Kuu England, fowadi wa Kibrazili, Gabriel Jesus ana rekodi nyingine tamu kabisa kwenye ligi hiyo.
Mabao 76 aliyofunga kwenye Ligi Kuu England yamepatikana kwenye mechi 62 tofauti, lakini kitu kitamu ni kwenye mechi hizo ambazo Jesus alifunga, hajawahi kupoteza, ameshinda 57 na sare tano. Jumla mechi za Ligi Kuu England ame-cheza 229.