Wakali wa kufumania nyavu 2025
Muktasari:
- Akikipiga kwenye kikosi cha Sporting Lisbon, Gyokeres alitarajiwa kuendeleza moto wa mabao 2025, licha ya kwamba ataingia kwenye ushindani mkali na wakali wengine kama Kylian Mbappe.
LONDON, ENGLAND: STRAIKA, Viktor Gyokeres alikuwa kinara wa mabao 2024, alipohitimisha mwaka huu akifunga mara 52.
Akikipiga kwenye kikosi cha Sporting Lisbon, Gyokeres alitarajiwa kuendeleza moto wa mabao 2025, licha ya kwamba ataingia kwenye ushindani mkali na wakali wengine kama Kylian Mbappe.
Kutokana na hilo, ni staa gani aliyefunga mabao mengi kwenye ligi za Ulaya tangu mwaka huu 2025 uanze?
10) Julian Alvarez (Atletico Madrid) - mabao 17
Mabao mawili aliyofunga dhidi ya Real Betis yamemfanya afikishe 17 kwenye mikikimikiki ya LaLiga msimu huu na ndiyo mabao hayo aliyofunga kwenye michuano yote kwa mwaka huu wa 2025.
9) Robert Lewandowski (Barcelona) - mabao 17
Ana miaka 36 na bado amekuwa tishio kwa makipa katika kuwatuma wakaokote mipira nyavuni. Ame-funga maao 25 katika mechi 33 za LaLiga kwa msimu huu, 17 amefunga ndani ya mwaka huu wa 2025.
8) Harry Kane (Bayern Munich) - mabao 18
Kama kuna kitu Harry Kane anakifanya vizuri basi ni kufunga mabao. Na amekuwa akilifanya hilo kwa uhakika huko Bundesliga akiwa na kikosi cha Bayern Munich, ambako amefunga mabao 18 mwaka huu.
7) Youssef En-Nesryi (Fenerbahce) - mabao 19
Staa wa zamani wa Sevilla, En-Nesryi amekuwa akifanya vizuri chini ya Jose Mourinho huko Uturuki, akionyesha makali ya kufunga mabao, ambapo kwa mwaka huu wa 2025 hadi sasa, amefunga mara 19.
6) Serhou Guirassy (Borussia Dortmund) - mabao 22
Hat-trick dhidi ya Barcelona ilionyesha ukali wa mshambuliaji huyo, aliyefunga mabao 13 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Bundesliga amekuwa moto pia, huku mwaka huu akifunga mabao 22.
5) Vangelis Pavlidis (Benfica) - mabao 22
Alifunga hat-trick pia dhidi ya Barcelona, lakini mabao yake aliyofunga dhidi ya Monaco kwenye mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, yalikuwa muhimu zaidi, huku mwaka huu wa 2025 akitikisa nyavu mara 22.
4) Victor Osimhen (Galatasaray) - mabao 24
Straika wa Napoli, Osimhen alitumia vyema muda wake aliokuwa kwa mkopo huko Uturuki kwa kufun-ga mabao ya kutosha, ambapo kwa mwaka huu wa 2025, ameonyesha yeye ni kiboko kutikisa nyavu mara 24.
3) Ousmane Dembele (PSG) - mabao 25
Dembele alifunga kwenye mechi nane za kwanza za PSG mwaka huu wa 2025, tena akifanya hivyo zaidi ya mara moja, ikiwamo mabao matano dhidi ya Brest na matatu dhidi ya Monaco huku akifikia 25 mwa-ka huu.
2) Viktor Gyokeres (Sporting) - mabao 26
Kinara huyo wa mabao wa mwaka jana, amefunga mara 39 kwenye ligi na kumfanya awindwe na timu kibao ikiwamo Arsenal. Lakini, mkali huyo ni balaa kwa kufunga, akitikisa nyavu mara 26 ndani ya mwa-ka huu wa 2025 pekee kuanzia Januari 1.
1) Kylian Mbappe (Real Madrid) - mabao 29
Mbappe ameonyesha kwanini Real Mdarid ilipambana kupata saini yake kutokana na uwezo wake wa kufunga, akianza maisha kwa kasi hafifu na kuzua maswali mengi kabla ya kuwa moto wa kuotea mbali mwaka huu, akifunga mabao 29.