WAFCON 2026; Mechi nane, mabao 29
Muktasari:
- Idadi hiyo imeifanya fainali ya mwaka huu kuwa na mwanzo wenye mabao mengi zaidi ikilinganishwa na WAFCON tatu zilizopita za mwaka 2024, 2022 na 2018.
TAYARI zimepigwa mechi nane za kwanza kwa kila kundi za fainali ya Kombe la Mataifa ya Afika kwa Wanawake (WAFCON), mashindano ambayo yameanza kwa kasi mwaka huu na kuweka rekodi ya mabao nchini Morocco.
Baada ya kukamilika kwa raundi ya kwanza ya mechi za makundi, jumla ya mabao 29 yamefungwa katika michezo minane, wastani wa kufunga mabao matatu kwa kila mchezo.
Idadi hiyo imeifanya fainali ya mwaka huu kuwa na mwanzo wenye mabao mengi zaidi ikilinganishwa na WAFCON tatu zilizopita za mwaka 2024, 2022 na 2018.
Katika WAFCON 2024 zilizokuwa zinashirikisha timu 12 baada ya mechi sita za kwanza za makundi yalifungwa mabao 16, wakati mwaka 2022 yalifungwa14 katika idadi hiyo hiyo ya michezo. Ukienda nyuma zaidi hadi mwaka 2018, mechi nne za kwanza za makundi zilizalisha mabao nane pekee. Takwimu hizo zinaonyesha wazi kuwa mashindano ya mwaka huu yameanza kwa kasi kubwa ya ushambuliaji kuliko matoleo matatu yaliyopita.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa nahodha wa Zambia, Barbra Banda, ndio kinara wa kupachika mabao kwenye mechi za kwanza, nyota huyo alifunga mabao manne katika ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Misri.Mabao hayo yamemfanya kuwa mfungaji anayeongoza kwa sasa na pia kumfanya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao manne katika mchezo mmoja wa WAFCON ndani ya takribani muongo mmoja.
Mabao hayo yanamuweka kwenye hatua nzuri ya kukaribia Kiatu cha Dhahabu katika baadhi ya matoleo yaliyopita. Akiwa tayari ana mabao manne baada ya mechi moja, anahitaji bao moja tu kufikisha mabao matano ambayo ndiyo yalimpa Ghizlane Chebbak tuzo ya mfungaji bora mwaka 2024 na Thembi Kgatlana mwaka 2018.
Katika WAFCON 2024, nyota wa Morocco, Chebbak, alitwaa Kiatu cha Dhahabu baada ya kufunga mabao matano. Mabao hayo yaliisaidia Morocco kutinga fainali kwa mara ya pili mfululizo na kuthibitisha ubora wake kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi barani Afrika.
Mwaka 2022 kulikuwa na ushindani mkali zaidi kwani Kiatu cha Dhahabu kiligawanywa na kwa Chebbak (Morocco), Rasheedat Ajibade (Nigeria) na Hildah Magaia (Afrika Kusini), kila mmoja akimaliza na mabao matatu.
Mwaka 2018,Thembi Kgatlana wa Afrika Kusini aliibuka mfungaji bora akitupia mabao matano yaliyokuwa na mchango mkubwa wa kutwaa ubingwa wa kwanza wa Afrika.
Banda ana nafasi nzuri ya kuandika historia mpya. Endapo ataendelea na kasi hiyo.