Cameroon yaizaba Mali 2-1 WAFCON
Muktasari:
- Indomitable Lionesses waliendeleza rekodi nzuri dhidi ya Mali kwani katika mechi tano walizokutana nyuma, wameshinda mechi nne na sare moja.
MSHAMBULIAJI Ngah Manga alifunga mabao mawili yaliyoiwezesha Cameroon kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo wa wa Kundi D wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 uliochezwa mjini Casablanca, Morocco.
Indomitable Lionesses waliendeleza rekodi nzuri dhidi ya Mali kwani katika mechi tano walizokutana nyuma, wameshinda mechi nne na sare moja.
Hii ilikuwa ni mechi ya sita kati ya mataifa hayo kwenye historia ya mashindano ya WAFCON, ambapo kwa mara nyingine walionyesha ushindani mkubwa katika mchezo uliokuwa na kasi kubwa kuanzia filimbi ya mwamuzi hadi dakika 90 kutamatika.
Cameroon ilitangulia kupata bao dakika ya 14 kupitia kwa mshambuliaji wa klabu ya Galatasaray S.K. Women ya Uturuki,nNgah Manga, ambaye alidhibiti kwa ustadi pasi ndefu kwa kifua kabla ya kumalizia kwa utulivu karibu na lango na kuipa timu yake uongozi wa mapema.
Mali walijibu dakika ya 30 baada ya kipa Michaely Bihina kumuangusha Aïssata Traoré ndani ya eneo la hatari alipokuwa akijaribu kuudaka mpira. Traoré alipiga penalti na kufunga kwa utulivu, na kufanya mchezo kuwa 1-1.
Kipindi kilichobaki cha kwanza kilikuwa cha ushindani mkubwa, huku kila timu ikitengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini safu za ulinzi zikifanya kazi nzuri kuzuia mabao zaidi.
Kipindi cha pili kiliendelea kwa kasi ileile, huku timu zote zikitafuta bao la ushindi.
Dakika ya 72, Cameroon walipata penalti baada ya mwamuzi kupitia mfumo wa VAR na kuthibitisha faulo. Manga alifunga tena kwa utulivu kutoka eneo la penalti na kukamilisha mabao yake mawili akiipa Cameroon uongozi wa 2-1.
Mali walifanya mashambulizi ya kusaka bao la kusawazisha katika dakika za mwisho, lakini Cameroon walikuwa imara. Nafasi bora zaidi iliangukia kwa mchezaji wa akiba Fatoumata Diarra katika sekunde za mwisho, lakini shuti lake halikuwa na nguvu za kutosha kumshinda Bihina, ambaye aliudaka mpira kirahisi na kuilinda Cameroon hadi mwisho wa mchezo.
Ushindi huo unaongeza sura nyingine nzuri katika rekodi ya Cameroon dhidi ya Mali kwenye mashindano haya.
Cameroon inashiriki WAFCON kwa mara ya 13, ikiwa imecheza kila toleo tangu mwaka 1998 isipokuwa lile la mwisho.
Sasa macho yote yatakuwa kwenye michezo ya pili ya Kundi D itakayochezwa Jumapili, ambapo Cameroon itavaana na Ghana katika mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu, baada ya Black Queens kuanza kwa ushindi dhidi ya Cape Verde. Kwa upande wa Mali, watakuwa wakisaka pointi tatu dhidi ya Cape Verde.