Ghana yaanza kwa ushindi, yaongoza Kundi D WAFCON
Muktasari:
- Hii ni mechi ya kwanza kwa Ghana na imeanza vizuri ikijikusanyia pointi tatu zilizoipeleka kileleni mwa msimamo wa kundi hilo.
Ghana imeanza kwa ushindi fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 baada ya kuichapa Cape Verde mabao 2-0 katika mchezo wa Kundi D uliopigwa katika Uwanja wa Moulay Rachid Morocco.
Hii ni mechi ya kwanza kwa Ghana na imeanza vizuri ikijikusanyia pointi tatu zilizoipeleka kileleni mwa msimamo wa kundi hilo.
Timu hiyo ilianza kupata bao dakika ya sita kupitia kwa mshambuliaji Doris Boaduwaa aliyemalizia vyema shambulizi lililoishtua safu ya ulinzi ya Cape Verde na kuifanya Ghana iongoze mechi hiyo.
Licha ya Cape Verde kujitahidi kujibu mashambulizi, Ghana iliendelea kutawala mchezo kwa kumiliki mpira kwa asilimia 64 huku ikitengeneza nafasi nyingi zaidi.
Takwimu zinaonyesha Ghana ilipiga mashuti 26, sita yakilenga lango, wakati wapinzani wao walipiga mashuti sita na moja ndilo lililolenga lango.
Ghana iliendelea kupeleka presha na kipindi cha pili dakika ya 54 baada ya Eleia Katy Pereira Vieira kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira uliokuwa ukielekea langoni, bao lililoweka mazingira magumu zaidi kwa Cape Verde kurejea mchezoni.
Cape Verde ilimaliza mchezo ikiwa pungufu baada ya Kleydiana Jussara Monteiro Maria Borges kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika za nyongeza, jambo lililohitimisha siku mbaya kwa timu hiyo ambayo ilishindwa kutumia nafasi chache ilizopata mbele ya lango la Ghana.
Ushindi huo umeifanya Ghana kuanza kwa pointi tatu na kuongoza Kundi D, huku Cameroon na Mali zikisubiri kuanza kampeni zao. Kwa Cape Verde, kipigo hicho kinawaacha mkiani mwa kundi bila pointi na wakilazimika kupambana katika mechi zinazofuata ili kufufua matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.