Wachambuzi, malejendi wamvaa kocha Man United
Muktasari:
- Neville amesema kauli hizo ni ujanja wa kocha huyo kutaka kujiweka kando na kile kinachoendelea katika timu yake badala yake alaumu wengine jambo ambalo ni baya sana.
MANCHESTER, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa Manchester United, Gary Neville amekosoa vikali madai ya Ruben Amorim kwamba wachambuzi wanashawishi wachezaji wa timu hiyo na kumtaka asijifiche na kulaumu watu wengine.
Neville amesema kauli hizo ni ujanja wa kocha huyo kutaka kujiweka kando na kile kinachoendelea katika timu yake badala yake alaumu wengine jambo ambalo ni baya sana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ijumaa ya wiki iliyopita, Amorim amesema anaona wachezaji wake wanapotoshwa na wachambuzi ambao wanakosoa sana mfumo wake na kudai kuwa hiyo ndio tatizo jambo ambalo sio kweli kwani yeye anaamini kuna vitu vidogo vidogo ambayo ndio vinaiangusha timu.
Amorim ilikuwa katika presha kubwa baada ya kipigo dhidi ya Brentford, lakini ushindi dhidi ya Sunderland Jumamosi umepunguza kidogo shinikizo la mashabiki kutaka afukuzwe.
“Je, watu hawakumbuki kwamba Alan Hansen alikosoa sana timu yetu kipindi kile tunaingia kama vijana, amesema Man United haitashinda chochote na wachezaji wadogo. Kumbuka huyu alikuwa beki wa kati bora zaidi wakati huo, beki wa kati aliyekamilika, wakati huo aliongea juu yetu kama vile hatukuwa na thamani na hatukuwa tunajua chochote kuhusu soka. Maana yangu ni kwamba hata sisi tulikosolewa. Ukiwa unacheza Manchester United, kukosolewa ni sehemu ya maisha na jambo pekee utakalofanya ili kuepuka hilo ni kuwa bora.”
Baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sunderland, Man United ilipanda hadi nafasi ya nane katika msimamo wa ligi.
Huo ulikuwa ni ni ushindi wao wa tatu tu katika mechi saba tangu kuanza kwa msimu huu na mechi mbili kati ya tatu ilizoshinda ni dhidi ya timu ambazo zimepanda daraja msimu huu.
Neville aliendelea kufunguka kwamba shida kubwa ya Amorim ni kukosa uwajibikaji jambo ambali sio zuri.
“Unapopoteza mechi hutakiwi kulaumu watu wengine wa nje ya timu, inatakiwa uanze ndani na ukionyesha ishara ya kujitoa, hilo ni jambo baya zaidi. Yeye na timu kwa ujumla wanatakiwa kufanya kazi yao vizuri na kushinda mechi za soka. Hilo ndilo jambo litakalowafunga midomo.”