Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vikwazo vitatu vinavyoikabili Arsenal kupata saini ya Isak

Muktasari:

  • Fowadi huyo wa kimataifa wa Sweden ni mmoja wa wachezaji ambao wapo kwenye kiwango cha juu sana cha soka huko Ulaya kwa sasa.

LONDON, ENGLAND: ARSENAL inakabiliwa na vikwazo vitatu katika mpango wa kunasa saini ya straika wa Newcastle United, Alexander Isak.

Fowadi huyo wa kimataifa wa Sweden ni mmoja wa wachezaji ambao wapo kwenye kiwango cha juu sana cha soka huko Ulaya kwa sasa.

Isak, 25, ameanza kuwasha moto baada ya kuanza msimu kwa kasi hafifu na sasa ameshafunga mabao 11 katika mechi 16 alizocheza kwenye Ligi Kuu England. Ubora wake umewavutia Arsenal kutaka huduma yake, lakini sasa kuna vikwazo vingi vinawakabili kabla ya kukamilisha dili hilo.

Kikwazo cha kwanza, fowadi huyo anachotaka kwa sasa ni kubaki St James Park - kama itamaliza ndani ya Top Four.

Taarifa za mtu wa karibu wa mshambuliaji huyo ni kwamba anataka kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini anachoamini atafikia mafanikio hayo akiwa Newcastle United.

Hilo ni pigo kwa Arsenal ambao waliamini tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ingeweza kumshawishi ajiunge kwao.

Kikwazo cha pili ni bei anayouzwa. Ripoti zinafichua kwamba Newcastle haitakuwa tayari kufanya biashara kuhusu mshambuliaji huyo kama dau mezani halifiki Pauni 150 milioni. Newcastle ilikataa kufanya mazungumzo kumuuza Isak kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana kwa sababu iliweka wazi bei ya mchezaji huyo ni Pauni 150 milioni, hivyo Chelsea ambao walionekana kuhitaji huduma  na ofa kiduchu, waliishia njiani.

Kutokana na mkataba wake kubakiza miaka mitatu na nusu, Newcastle hawana presha na kwamba ikifika mwisho wa msimu wanaporesha mkataba huo, wakimwongezea muda zaidi na bei yake itazidi kupanda na si kushuka. Kinachoelezwa ni kwamba mazungumzo ya mkataba mpya yalisitishwa mapema mwaka jana, lakini Newcastle inachokihitaji kwa Isak ni kuendelea kubaki na huduma yake kwa muda mrefu kwenye kikosi chao. Arsenal imekuwa ikifuatilia Isak kwa muda mrefu sana, huku fowadi huyo akifunga mabao 43 katika mechi 69 alizocheza kwenye Ligi Kuu England.

Hata hivyo, shida inaweza kuwa kwenye kupata pesa zinazohitajika kunasa saini ya mchezaji huyo kutokana na masharti yaliyopo kwenye Ligi Kuu England kwa sasa kuhusiana na udhibiti wa usawa wa mapato na matumizi.

Kikwazo cha tatu kinachowakabili Arsenal kwenye matumaini yao ya kumsajili straika Isak ni kwamba si wao tu ndiyo wanaohitaji saini ya mchezaji huyo.

Matajiri wa Ufaransa, Paris Saint-Germain nao wamo kwenye mpango huo, wanaripotiwa kufukuzia saini ya straika huyo, lakini pia kuna klabu mbili vigogo wa Hispania, Barcelona na Real Madrid nazo zinamhitaji mkali huyo.

Na Liverpool kama itashindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya na supastaa wao Mohamed Salah, nao wataingia kwenye vita ya kufukuzia huduma ya Isak ili akawe mbadala wa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Misri huko Anfield.

Kutokana na kuwapo na klabu hizo zenye nguvu kubwa na ushawishi wa kutosha kuingia kwenye vita ya kuhitaji saini ya Isak hilo linaweza kuwatibulia Arsenal kwenye mpango wa kupata huduma yake. Na vuta nikuvute hiyo inaweza kuchochea pia kupanda kwa bei ya Isak.

Mchezaji anayeshikilia rekodi ya dunia kwa sasa ya kusajiliwa kwa pesa nyingi ni Mbrazili, Neymar aliponaswa kwa Pauni 198 milioni wakati anahama kutoka Barcelona kwenda PSG mwaka 2017. Kwa bei iliyowekwa na Newcastle United ya Pauni 150 milioni, inaweza kuongezeka kutokana na uhitaji wa timu wa kutaka saini ya Isak na hivyo kumweka kwenye nafasi nzuri ya kuuzwa pesa nyingi zaidi, inaweza kuvunja rekodi ya Neymar endapo kama ataendelea kucheza kwa kiwango chake cha sasa na zaidi. Kwenye Ligi Kuu England, Isak amecheza mechi 16, akitengeneza nafasi za mashambulizi 28, amefunga mabao 11 na kuasisti mara nne. Amepiga mashuti golini mara 23 na kupiga pasi 306, huku kwenye eneo lake la kuwa mshambuliaji wa kati, amehusika pia kwenye kuzuia mashambulizi ya wapinzani na hivyo kujikuta akicheza faulo mara 16.

Kwa Arsenal kama itakwama kabisa kwa Isak, basi mpango wao ni kuhamia kwa staa wa Wolves, Matheus Cunha, ambaye ni chaguo moja linalofikiriwa na kocha Mikel Arteta katika kuboresha kikosi cha miamba hiyo ya Emirates.