Viktor Gyokeres awavuruga mashabiki Arsenal
Muktasari:
- Gyokeres amekuwa kwenye sakata zito la usajili kwenye kikosi cha Arsenal dirisha hili la majira ya kiangazi, huku dili hilo likidaiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kukamilika ambapo straika huyo wa kimataifa wa Sweden anatarajia kutua London kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya.
LONDON, ENGLAND: KUMEKUCHA. Mashabiki wa Arsenal wametumia kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii kutuma ujumbe kwa mabosi wao kusitisha mpango wa kumchukua straika Viktor Gyokeres na badala yake ikamnase Alexander Isak.
Gyokeres amekuwa kwenye sakata zito la usajili kwenye kikosi cha Arsenal dirisha hili la majira ya kiangazi, huku dili hilo likidaiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kukamilika ambapo straika huyo wa kimataifa wa Sweden anatarajia kutua London kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya.
Lakini, baada ya straika Isak kuibua sakata zito la kuwaambia mabosi wa Newcastle United kwamba anataka kuhama kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamewataka mabosi wao, waachane na Gyokeres na kurudi haraka kwa mkali huyo wa St James’ Park.
Shabiki wa kwanza aliposti kwenye X: “Futeni ishu ya kumpima afya Gyokeres.”
Posti ya shabiki huyo imeonekana kuwavutia wengi, ikipata like 16,000.
Na mashabiki wapinzani wa Arsenal nao walisema kitu, ambapo mmoja aliandika: “Hivi Gyokeres ameshafuzu vipimo vya afya? Kwa sababu baada ya hii taarifa ya Isak, mimi kama ningekuwa Arsenal ningedanganya Gyokeres ni majeruhi.”
Na shabiki mwingine alisema: “Ningetoa ofa ya Pauni 50 milioni pamoja na mchezaji Gyokeres kwa ajili ya Isak. La kama mtasitisha kumfanyia vipimo...”
Gyokeres aliripotiwa kupanga kufanya vipimo vya afya Ijumaa baada ya sakata lake la uhamisho kuchukua muda mrefu kwa kuvutiana na mabosi wa Sporting CP. Dili linalomvuta Emirates mkali huyo linatajwa kuwa na thamani ya Pauni 63.5 milioni, huku straika huyo alifunga mabao 39 kwenye ligi msimu uliopita.
Mshambuliaji mwenzake wa Sweden, Isak alikuwa mmoja wa mastraika bora kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, lakini sasa anadaiwa kutaka kuachana na Newcastle United baada ya Liverpool kujaribu mchakato wa kunasa saini yake kwa ada ya Pauni 120 milioni.
Kitendo cha kuondoshwa kwenye kikosi cha Newcastle kilichofanya ziara ya kwenda Singapore kumenyana na Arsenal kwenye mechi ya kirafiki kimeibua shaka. Na Alhamisi iliyopita, Isak aliiambia klabu yake anataka kuondoka kwenye timu hiyo yenye maskani yake St James’ Park.
Kulikuwa na ishu kubwa kati ya Newcastle na Liverpool juu ya straika huyo, ambapo chama la Anfield liliulizia upatikanaji wa Isak, kabla ya kuvamia mawindo ya Newcastle na kumnyakua Hugo Ekitike.
Lakini, baada ya kusikia Isak anataka kuondoka, Liverpool inapiga hesabu za kurudi tena kwa mshambuliaji ili kupata saini yake, lakini mashabiki wa Arsenal wanataka timu yao nayo iingie kwenye mchakato wa kumnasa straika huyo ambaye tayari ameshaonyesha kiwango bora kwenye Ligi Kuu England.
Liverpool imelipa Pauni 116.5 milioni kunasa saini ya Florian Wirtz mwezi uliopita, lakini Newcastle inamthaminisha Isak kuwa na thamani ya Pauni 150 milioni, pesa ambayo itaweka rekodi ya uhamisho England.