Vigogo EPL wamiminika kuwania saini Garnacho
Muktasari:
- Garnacho ni miongoni mwa wachezaji waliotumika zaidi ndani ya Manchester United katika msimu wa 2024/25 ambapo alicheza mechi 52 katika mashindano yote Ulaya akifunga mabao 11 na kutoa asisti 10.
BAADA ya Chelsea kutajwa hivi karibuni, Tottenham Hotspur na Aston Villa pia zimeingia katika vita ya kuwania saini ya winga wa Manchester United na timu ya taifa ya Argentina, Alejandro Garnacho, 21 katika dirisha la usajili linaloendelea.
Garnacho ni miongoni mwa wachezaji waliotumika zaidi ndani ya Manchester United katika msimu wa 2024/25 ambapo alicheza mechi 52 katika mashindano yote Ulaya akifunga mabao 11 na kutoa asisti 10.
Hata hivyo, kocha wa timu hiyo, Ruben Amorim anadaiwa kuwa haridhishwi na utendaji wake uwanjani na tayari amemuweka katika orodha ya wachezaji ambao hawapo katika mipango yake kwa msimu ujao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti mbalimbali za England, Man United inahitaji takribani Pauni 40 milioni ili kumuuza Garnacho.
Mchezaji huyo bado ana mkataba mrefu wa muda mrefu na Man United ambao unatarajiwa kumalizika 2028, na kuna kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi baada ya kipindi hicho.
Chelsea chini ya Enzo Maresca inahitaji huduma ya mchezaji huyo kwa sababu kocha anaamini kwamba anaendana na mifumo yake.
Kwa upande wa Tottenham, kocha Thomas Frank moja kati ya eneo ambalo anataka kulifanyia maboresho dirisha hili ni lile la winga ya kushoto ambapo anahitaji mchezaji anayeweza kufanya uamuzi wa haraka na kutoa asisti, sifa ambazo Garnacho anazo.
Mbali na kiwango chake ndani ya Manchester United, pia Garnacho anazidi kuimarika katika timu ya taifa ya Argentina ambako tayari ameshacheza mechi sita za kimataifa na alijumuishwa kwenye kikosi cha Copa America 2024.
Benjamin Sesko
MABOSI wa Manchester United wanaamini mshambuliaji wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Slovenia, Benjamin Sesko, 22 anatamani zaidi kujiunga nao kuliko timu nyingine. Sesko ambaye msimu uliopita alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 21, ana mkataba unaomalizika 2029 lakini kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka kwa Euro 78 milioni katika dirisha hili.
Ollie Watkins
ASTON Villa imejiandaa kupokea ofa kutoka Manchester United kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa England, Ollie Watkins, 29, ikiwa itashindwa kumnasa Benjamin Sesko wa RB Leipzig. Watkins alimaliza msimu uliopita akiwa mfungaji bora wa Villa na mabao 16 akitoa asisti nane katika michezo 38 EPL. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Harvey Elliott
RB Leipzig imeonyesha nia ya kumsajili kiungo wa Liverpool, Harvey Elliott, 22, ambaye inahitajika kati ya Pauni 30 hadi 40 milioni ili kuipata huduma yake. Elliott bado ana mkataba wa kuitumikia Liverpool hadi 2027 na anatamani sana kuondoka kwa sbabau hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Arne Slot. Msimu uliopita alicheza mechi 28 za michuano yote.
Harry Maguire
INAELEZWA Manchester United imekataa ofa tano kutoka kwa klabu za England na Italia kwa ajili ya beki mkongwe Harry Maguire. Beki huyo ambaye msimu uliopita alicheza mechi 29, amekuwa akihusishwa kuondoka Man United kwa muda mrefu, lakini ofa ambazo zimewasilishwa na timu hizo hazijafikia kiasi ambacho Mashetani Wekundu wanakihitaji.Mkataba wake unamalizika 2026.
Lloyd Kelly
JUVENTUS ipo tayari kumuuza beki Lloyd Kelly, ambaye ilimsajili kama mchezaji huru kutoka Newcastle United katika dirisha lililopita la majira ya baridi. Mchezaji huyo ambaye alicheza mechi nne katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu mwaka huu, kiwango chake kinadaiwa hakiridhishi benchi la ufundi la Juventus. Mbali ya kuwa tayari kumuuza pia imepanga kumsajili beki wa Arsenal Jakub Kiwior, 25, kama mbadala wake.
Dominic Calvert-Lewin
SUNDERLAND inataka kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Everton, Dominic Calvert-Lewin, 28, ambaye kwa sasa yupo huru baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu uliopita. Lewin ambaye msimu uliopita alisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, alifunga mabao sita katika mechi 21 za EPL. Mbali ya Sunderland, Lewin pia amepokea ofa ya West Ham.
Jacob Ramsey
WEST Ham United inataka kumsajili kiungo wa Aston Villa, Jacob Ramsey, 24, ambaye msimu uliopita aliandamwa na majeraha. Ramsey bado ana mkataba wa kuitumikia Villa hadi 2027, lakini nafasi yake kikosini inaonekana kuwa ndogo hali inayosababisha atamani kuondoka. Msimu uliopita alicheza mechi 46.