Uzito rungu la Man City
Muktasari:
- Februari 2023, Man City ilifunguliwa kesi na Chama cha Soka England (FA) kutokana na kipengele cha usawa wa mapato na matumizi kilichopo kwenye kanuni maarufu kama FFP.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City ilitumia takriban Pauni 1.2 bilioni kusajili wachezaji wapya katika misimu tisa wakati ilipokuwa ikikabiliwa na mfululizo mkubwa wa matumizi ya fedha tofauti na mapato, suala ambalo hatimaye hukumu yake inaweza kuwa mbaya zaidi katika ulimwengu wa soka.
Februari 2023, Man City ilifunguliwa kesi na Chama cha Soka England (FA) kutokana na kipengele cha usawa wa mapato na matumizi kilichopo kwenye kanuni maarufu kama FFP.
Itakumbukwa mwaka 2006, Juventus ilikumbana na rungu zito kutokana na skendo maarufu ya Calciopoli iliyohusisha upangaji wa matokeo na kuwahonga marefa, jambo lililoilazimisha kushushwa hadi Daraja la Pili Italia msimu wa 2006/2007.
Ni katika kali kama hiyo kwenye ulimwengu wa soka inayoweza kutumika dhidi ya Man City iliyokutwa na hatia katika makosa 114 kati ya 115 ya matumizi mabaya ya fedha katika uendeshaji wa shughuli zake hasa usajili wa wachezaji, na kinachosubiriwa ni adhabu inayoweza kuwa na matokeo matatu mazito; kupokwa pointi nyingi na kushushwa daraja, kulimwa faini kubwa na kupokonywa ubingwa ilioupata katika kipindi cha kuanzia msimu wa 2009/10 hadi 2017/2018 na au kufungiwa kusajili wachezaji kwa miaka mingi sambamba na faini.
Hata hivyo, wakati timu hiyo ikitarajiwa kupokea adhabu huku ikidaiwa kuwa katika hatua za mwisho za kukata rufaa, timu kadhaa za Ligi Kuu England zinapanga kuifungulia mashtaka zikitaka fidia kutokana na kukoseshwa haki ya mafanikio katika kipindi ambacho City ilikuwa ikimwaga fedha kusajili mastaa bila kuzingatia mizania ya mapato na matumizi.
Tayari Manchester United sambamba na wachezaji wake wengi wakiwamo wa zamani wameelezea wanazitaka medali za ubingwa walizovyalishwa nyota wa Man City katika kipindi ambacho ilibeba ubingwa mfululizo wa mashindano ya England ukiwa ubingwa wa ligi. Timu nyingine zilizoikalia kooni City ni Chelsea, Arsenal na Liverpool.
WAMECHANGIA
Kwa mujibu wa ripoti kutoka The Athletic katika misimu ya kuanzia 2009/10 hadi 2017/18, Man City ilisajili wachezaji 76 kwa jumla, huku usajili ghali zaidi ukiwa na thamani ya Pauni milioni 55.
Wakati baadhi ya wachezaji hao walitua na kuwa magwiji wa klabu wengine walitoweka haraka kama walivyowasili kutokana na kushindwa kuingia katika mifumo ya makocha na mazingira ya klabu, ambapo uhamisho mkubwa ulikuwa wa Muargentina Carlos Tevez wenye thamani ya Pauni 25.5 milioni ulioashiria kuanza kwa enzi mpya 2009/10.
Tevez ambaye alikuwa ametumia misimu miwili iliyotangulia kwa mkopo Manchester United alicheza mechi 42 katika msimu wake wa kwanza City akifunga mabao 29 na kutoa asisti saba akisaidia City kumaliza nafasi ya tano kutoka ya 10 msimu uliotangulia na kufuzu kucheza Europa League.
Kuanzia msimu uliofuata, walianza kuweka msingi wa kikosi kilichokuja kushinda ubingwa kupitia usajili wa mastaa Yaya Toure na David Silva kwa ada ya Pauni milioni 24 kila mmoja.
Toure alifunga bao la ushindi dhidi ya United katika nusu fainali ya FA Cup mwaka 2011 kabla ya kufanya hivyo tena dhidi ya Stoke kwenye Uwanja wa Wembley na kuipa klabu hiyo taji lake kubwa la kwanza baada ya miaka 35.
Kwa pamoja, wawili hao walishinda mataji matatu ya Ligi Kuu England, Carabao Cup tatu, FA Cup moja na Community Shield moja.
Kisha, mwaka 2011 likatua jina lililobadilisha kila kitu; Sergio Aguero ambalo City iliilipa Atletico Madrid karibu Pauni 38 milioni kusajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 na kumfanya kuwa usajili wa gharama kubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo wakati huo.
Alipowasili alisema: “Sisi ni timu ambayo siku zijazo itakuwa ikipambana kila mwaka kushinda mataji makubwa.”
Na Muargentina huyo hakudanganya alikuwa mfungaji bora wa muda wote wa City, lakini hata bila yote yaliyofuata angekuwa tayari ameweka historia kutokana na bao lake la dakika ya 93.20 lililoipa City ubingwa wa msimu wa 2011/12.
Lakini si kila dirisha la usajili lilileta staa Muargentina wa kuvunja rekodi kwa City ili kuimarisha hadhi yao. Biashara ya usajili kwa msimu wa 2012/13 ilikuwa na mvuto mdogo zaidi.
Javi Garcia alikuwa usajili mkubwa zaidi akitokea Benfica kwa ada ya karibu Pauni 16 milioni, lakini bahati mbaya walilazimika kushuhudia United wakiwapiku na kutwaa ubingwa wa ligi, wakimaliza wakiwa na tofauti ya pointi 11, huku Kocha Roberto Mancini akiondoka. Walirejea 2013 wakati kocha mpya Manuel Pellegrini alipowasaidia kutwaa mataji mawili.
Fernandinho mwanzoni alionekana kuwa mchezaji wa miaka 28 aliyekuwa ghali kutoka Shakhtar Donetsk kusajiliwa na City aliyetua kwa ada ya Pauni milioni 30.
Lakini baadaye alithibitisha thamani yake, akawa kiungo aliyesaidia kuunganisha enzi ya Pellegrini na ile ya Pep Guardiola.
Dirisha lililofuata liliacha wakiwa wametumia Pauni 62.42 milioni zaidi ya walizopata kutokana na wachezaji waliowaachia. Eliaquim Mangala alikuwa juu katika orodha ya usajili wa fedha nyingi ikiwa ni ada ya Pauni 38.75 milioni na beki huyo Mfaransa alitumia misimu miwili kwenye Ligi Kuu England akiwa na matumaini ya kuwa mshirika wa muda mrefu wa Vincent Kompany.
Badala yake, alianza maisha ya kusafiri kwa mikopo katika klabu mbalimbali Ulaya, kisha wakaja mastaa wakubwa; City walivunja rekodi ya usajili kwa kumsajili kiungo wa zamani wa Chelsea, Kevin De Bruyne kwa Pauni 55 milioni kutokea Wolfsburg wakamrudisha England.
Pamoja naye alikuwepo staa wa zamani wa England, Raheem Sterling, aliyefanya uhamisho wa kushtukiza kutoka Liverpool kwa Pauni 44 milioni, akiwa mmoja wa wachezaji Waingereza waliowahi kusajiliwa kwa gharama kubwa zaidi wakati huo.
Na mara Guardiola alipowasili, hakupoteza muda kuingiza kikosini mastaa ambao wangeweza kuunda timu ya muongo uliofuata, na usajili wa kwanza akiwa City ulikuwa Ilkay Gundogan, aliyesajiliwa kutoka Borussia Dortmund kwa karibu Pauni 21 milioni.
Alipitia matatizo makubwa ya majeraha mwanzoni, lakini hatimaye akawa nahodha, mshindi wa mataji mara kwa mara na mmoja wa viungo waliokuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo.
John Stones, aliyewasili kutoka Everton kwa karibu Pauni 47.5 milioni akawa mmoja wa mabeki ghali zaidi duniani wakati huo, huku winga Leroy Sane naye akifuata kutoka Schalke kwa ada ya Pauni 37 milioni aliyefanya vizuri katika msimu wake wa kwanza na hata akashinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Kulipwa England katika msimu ambao City walitwaa ubingwa 2017/18.
Lakini Guardiola na City hawakuwa tayari kuishia hapo. Waliendelea na ununuzi mkubwa katika soko la usajili, wakinasa wachezaji kama Kyle Walker (Pauni 45 milioni), Bernardo Silva (Pauni 43 milioni) na Ederson (Pauni 35 milioni).
City pia walifungua pochi kumsajili beki wa kushoto wa Monaco, Benjamin Mendy (Pauni 49.5 milioni) na Danilo wa Real Madrid (Pauni 25.8 milioni), kabla ya Aymeric Laporte (Pauni 55.9 milioni) kuwasili Januari 2018. Na kutokana na hilo, matokeo yakaanza kuonekana, tena yakawa makubwa.
Kikosi cha Guardiola kilimaliza msimu kikiwa na POINTI 100, ikiwa timu ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu England kufikisha idadi hiyo na kumaliza msimu ikiwa na tofauti ya pointi 19 dhidi ya timu iliyoshika nafasi ya pili.
MASTAA KUONDOKA?
Adhabu yoyote kubwa inaweza kusababisha baadhi ya mastaa wakubwa wa klabu hiyo kuondoka, akiwemo mshambuliaji wa Norway, Erling Haaland, ambaye amebakiza miaka minane kwenye mkataba wake wa miaka 10 wenye thamani ya Pauni 500,000 kwa wiki na City ingawa inaaminika kuwa una vipengele vya kuvunjwa, hasa ikiwa City watashushwa daraja.
City walitumia zaidi ya Pauni 450 milioni katika soko la usajili msimu huu, huku wachezaji wawili wakisajiliwa kwa zaidi ya Pauni 100 milioni.
Fernandez alijiunga akitokea Chelsea kwa ada ya rekodi ya Pauni 125 milioni mwishoni mwa dirisha la usajili, wakati Elliot Anderson alisajiliwa kutoka Nottingham Forest kwa Pauni 116 milioni. Kiungo Ayyoub Bouaddi pia alihama kutoka Lille kwa Pauni 85 milioni.
Mshambuliaji wa Everton, Iliman Ndiaye, na winga wa Palmeiras, Allan, walikuwa miongoni mwa mastaa wengine waliokamilisha uhamisho katika dirisha lililoweka rekodi.
RODRI AWATETEA
Rodri, nyota wa Barcelona na Hispania aliyetokea Manchester City msimu huu amesisitiza kwamba ‘walistahili’ mafanikio licha ya kupatikana na hatia ya FFP
Mchezaji huyo amesema hakuna anayeweza kuwanyang’anya mafanikio waliyopata wachezaji wa Man City na bado anaamini klabu yake ya zamani haikuwa na hatia.
Rodri alimaliza kipindi chake cha mafanikio makubwa katika Uwanja wa Etihad wakati wa majira ya kiangazi na hakuepuka swali hilo alipokuwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya dhidi ya England.
“Tulikumbana na jambo kama hili mwaka 2020, tulikuwa na mchakato kama huo wa kisheria,” alisema kiungo huyo wa Barcelona.
“Mashtaka yalikuwa tofauti lakini mchakato ulikuwa kama huu.”