Mechi nane za kutazama Qatar
Muktasari:
- Miongoni mwa mechi za kuvutia ni ile ya kundi E, Italia dhidi ya Jamaica na Ivory Coast dhidi ya Uzbekistan. Italia inaingia ikiwa bingwa wa Ulaya U-17 wa mwaka huu baada ya kuifunga Ubelgiji kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1.
MECHI nyingine nane za hatua ya makundi ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17, Qatar 2026, zinatarajiwa kuchezwa leo Novemba 20, 2026 huku mataifa 16 yakisaka matokeo katika mashindano hayo yanayoshirikisha timu 48.
Miongoni mwa mechi za kuvutia ni ile ya kundi E, Italia dhidi ya Jamaica na Ivory Coast dhidi ya Uzbekistan. Italia inaingia ikiwa bingwa wa Ulaya U-17 wa mwaka huu baada ya kuifunga Ubelgiji kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1. Jamaica nayo ilifuzu kwa kushinda mechi zote tatu za kufuzu Concacaf na kufunga mabao 18, huku nahodha Jahmarie Nolan akifunga manne na kutoa asisti mbili.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Ivory Coast inataka kubadili rekodi yake baada ya kupoteza mechi zote tatu za makundi mwaka jana. Hata hivyo, ina kumbukumbu nzuri ya mwaka 1987 ilipomaliza nafasi ya tatu. Uzbekistan imefuzu baada ya kufika nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Asia U-17, ikiwa na nyota kama Asilbek Aliev na Muhammad Khakimov.
Kundi F, litakuwa na Senegal dhidi ya Croatia na Cuba dhidi ya Tajikistan. Senegal, mabingwa wa Afrika U-17 mwaka huu, inashiriki kwa mara ya nne baada ya kufika 16 bora mwaka 2019 na 2023, kabla ya kutolewa hatua ya 32 bora mwaka 2025.
Cuba, kwa upande mwingine, inarejea kwenye fainali hizo baada ya miaka 35 tangu iliposhiriki mara ya mwisho mwaka 1991.
Mshambuliaji Yankarlos Iglesias ni miongoni mwa wachezaji wake wa kuangaliwa baada ya kuchangia mabao mawili na asisti moja kwenye kampeni ya kufuzu.
Kundi G litashuhudia Mali ikiumana na New Zealand, huku Ubelgiji ikiikabili Vietnam.
Mali, iliyowahi kucheza fainali mwaka 2015 na kushika nafasi ya tatu na ya nne miaka tofauti, inaingia ikiwa na matarajio ya kufanya vizuri zaidi baada ya kutolewa hatua ya 16 bora mwaka jana.
New Zealand imewahi kufika 16 bora mwaka 2009, 2011 na 2015. Ubelgiji nayo inaingia baada ya kuwa mshindi wa pili wa mashindano ya Ulaya U-17 mwaka huu, ikipoteza fainali kwa Italia kwa penalti.
Katika kundi H, Hispania itakutana na China, huku Fiji ikiikabili Morocco. Hispania imefika fainali za mashindano hayo mara nne, mwaka 1991, 2003, 2007 na 2017, bila kutwaa ubingwa.
China nayo inakuja ikiwa mshindi wa pili wa Kombe la Mataifa ya Asia U-17 mwaka huu baada ya kupoteza fainali dhidi ya Japan.
Beki Junior Zamorano na kiungo Zhou Yunuo ni miongoni mwa wachezaji wa kuangaliwa katika timu hizo.
Morocco inaingia dhidi ya Fiji ikiwa na uzoefu wa kufika robo fainali katika matoleo mawili yaliyopita, 2023 na 2025.
Mshambuliaji Ziyad Baha ni jina la kuangaliwa baada ya kufunga mabao manne mwaka jana, yakiwemo mawili katika ushindi wa 16-0 dhidi ya New Caledonia. Fiji inashiriki kwa mara ya pili mfululizo na itategemea zaidi kiungo Maikah Dau, aliyekuwa nahodha wake mwaka jana.