Uwanja wa Old Trafford unavyoikataa Man United
Muktasari:
- Lakini, tangu Ferguson aondoke Mei 2013 mambo yamebadilika kwa kiwango kikubwa.
MANCHESTER, ENGLAND: UWANJA wa Old Trafford unaojulikana pia kama ‘Theatre of Dreams’ kwa muda mrefu ulikuwa ngome ya kutisha chini ya utawala wa kocha Sir Alex Ferguson.
Kuanzia 1986 hadi 2013, Ferguson aliijengea Manchester United heshima kubwa na kufanya uwanja huo kuwa sehemu ambayo timu nyingi za Ligi Kuu England na Ulaya ziogope kwenda kuchezea hapo.
Lakini, tangu Ferguson aondoke Mei 2013 mambo yamebadilika kwa kiwango kikubwa. Old Trafford imebaki kuwa jina na timu nyingi hazionekani kuwa na hofu ya kucheza hapo. Timu kubwa na ndogo zimekuwa zikipata ushindi, kuandika historia na kuvunja rekodi ambazo zilidumu kwa miongo kadhaa. Hapa chini tunakuwekea rekodi ambazo zimewahi kuvunjwa tangu Ferguson aondoke katika timu hiyo.
8. KIPIGO KIZITO LIVERPOOL
Oktoba 24, 2021 Man United ilipokea kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Liverpool. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Liverpool kupata ushindi mkubwa kama huo bila ya Man United kupata hata bao moja katika dimba hilo tangu 1986.
Mohamed Salah alifunga hat-trick akiwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kufanya hivyo kwenye uwanja huu katika historia ya Ligi Kuu England. Kipigo hicho kilikuwa aibu kubwa kwa Man United kwa sababu kilitokea mbele ya mashabiki 73,000, ambapo baadhi waliondoka mapema kabla ya dakika ya 60. Awali, Ferguson hakuwahi kushuhudia kipigo kikubwa namna dhidi ya Liverpool nyumbani.
7. KIPIGO CHA KARNE KUTOKA SPURS
Jose Mourinho, aliyewahi kuwa kocha wa Man United alirudi Old Trafford na kuiongoza Spurs kutoa kipigo kikubwa zaidi dhidi ya Man United nyumbani tangu 1930. Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Anthony Martial kuonyeshwa kadi nyekundu, Tottenham ilifunga mabao 6-1 kupitia Son Heung-min na Harry Kane.
Hii ilikuwa mara ya pili kwanza Man United kuruhusu mabao sita nyumbani kwani iliwahi kufanya hivyo mbele ya majirani zao Man City kipindi cha Sir Alex Ferguson ambapo mechi ilimalizika kwa 6-1.
6. BURNELY KUANDIKA HISTORIA YA MIAKA 58
Baada ya kuichapa Man United kwa mabao 2-0, Januari 22, 2020, Burnley iliandika historia ya kupata ushindi wa kwanza katika dimba la Old Trafford tangu 1962. Mabao ya Chris Wood na Jay Rodriguez yaliwafanya mashabiki wa Burnley kushangilia ushindi wa kihistoria. Kwa Mashabiki wa United waliishia kuandamana na kutaka Ed Woodward na familia ya Glazers waachane na timu yao baada ya mchezo.
5. USHINDI WA KWANZA KWA PALACE
Agosti 24, 2019 Crystal Palace iliweka rekodi ya mara ya kwanza tangu 1992 kushinda mechi Old Trafford baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya wenyeji wa uwanja huo. Bao la dakika za jioni la Patrick van Aanholt lilipeleka Palace kwenye vitabu vya historia. Hata hivyo, Palace ilithibitisha kuwa ushindi huo hakuwa ajali kwa kurudi katika uwanja huo 2020 kisha kushinda kwa mabao 3-1.
4. BRIGHTON MARA YA KWANZA OLD TRAFFORD
Mwaka 2022, Brighton ilishinda mechi ya Ligi Kuu Englanda kwa mabao 2-1 Old Trafford. Huo ulikuwa ni ushindi wa kwanza kabisa katika historia yao. Pascal Grob alifunga mara mbili na kufanya Man United kuanza vibaya msimu huo. Mwaka uliofuata, 2023, Brighton ilirudia kushinda tena kwa mabao 3-1.
3. MAN CITY KUTAWALA OLD TRAFFORD
Kuanzia 2019 hadi 2022, Man City ilishinda mechi nne kati ya sita ilizocheza Old Trafford katika michuano tofauti, kitu ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya jiji hilo. Ushindi wa 2-0 (2019), 3-1 (2020), 2-0 (2021), 2-0(2021).
Wakati wa Sir Ferguson, Man United mara nyingi ndiyo ilikuwa inatawala dabi hiyo.
2. MABAO MACHACHE ZAIDI NYUMBANI
Msimu wa 2015/16 chini ya kocha Louis van Gaal, Man United ilifunga mabao 19 pekee nyumbani katika msimu mzima wa ligi hiyo. Hii ilikuwa idadi ndogo zaidi ya mabao yaliyofungwa Old Trafford kwa msimu mmoja tangu 1973. Timu kama Norwich City, Southampton na West Bromwich Albion pia ziliondoka Old Trafford na ushindi.
1. LEICESTER CITY YAVUNJA MWIKO
Mei, 2021 Leicester ilipata ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kushinda mchezo kwenye uwanja huo tangu 1998. Ushindi huo uliisaidia Leicester City kufuzu michuano ya Europa League na pia ulivunja rekodi ya Man United ya kutopoteza nyumbani michezo 14 mfululizo.