Prime
Jibu la Kajala kwa Harmonize baada ya kusema hamuheshimu
KAULI ya mwanamuziki Rajab Abdul Kahali, maarufu Harmonize, kudai kuwa aliyekuwa mpenzi wake, Kajala Masanja, hamheshimu na humfanyia dharau kutokana na tofauti yao ya umri imezua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika moja ya maonyesho yake ya hivi karibuni, Harmonize alisikika akiwa jukwaani akisema Kajala ni mtu mwenye maringo, anayependa kubembelezwa na hampi heshima anayostahili kwa sababu anamwona ni mdogo kwa umri.
Kauli hiyo imeamsha upya mjadala kuhusu mahusiano yao, huku baadhi ya watu wakidai wawili hao wameachana, wakati wengine wakiamini huenda ni mgogoro wa kawaida na bado wanaweza kumalizana.
Kutokana na mjadala huo, Mwanaspoti ilimtafuta Kajala ili kupata upande wake kuzungumza hilo.
Mwanaspoti: Harmonize amesema humheshimu, unamdharau na kwamba tofauti yenu ya umri ndiyo chanzo cha hali hiyo. Unasemaje kuhusu kauli hizo?
Kajala: "Mmmm... niache kwanza, tutaongea."
Mwanaspoti: Hutaki kuzungumzia kabisa alichokisema?
Kajala: "Sitaki kuzungumzia alichokisema. Kwanza sijasikia chochote." (Anacheka).
Mwanaspoti: Sawa, unaweza kusema hujasikia, lakini video imesambaa karibu kila sehemu mitandaoni. Hujawahi kuiona?
Kajala: "Hapana, sijaiona."
Mwanaspoti: Kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu uhusiano wenu. Wapo wanaosema mmeachana, wengine wakisema bado mpo pamoja. Una lipi la kuwaambia?
Kajala: "Sina chochote cha kuzungumzia kuhusu penzi letu kwa sasa. Rhobi, hivi unajua tuna kipindi cha A List kinachoonyeshwa DSTV? Embu waambie mashabiki zangu wakitazame basi... khaa!"
Mwanaspoti: Nitawaambia. Ila na hili la Harmonize pia mashabiki wako wanahitaji kulisikia kutoka kwako, kwa sababu wana maswali mengi.
Kajala: "Waambie nawapenda mashabiki zangu."
Baada ya majibu hayo mafupi, Kajala hakutaka kuongeza neno lolote kuhusu Harmonize wala hali ya mahusiano yao.
Kauli ya Harmonize ilivyoibua gumzo
Video ya Harmonize akizungumza jukwaani imeendelea kusambazwa kwa kasi kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii. Mbali na kusema Kajala anapenda kubembelezwa, msanii huyo alidai pia kuwa wakati mwingine hakupata heshima aliyotarajia ndani ya uhusiano wao.
Kauli hizo zimegawa maoni ya mashabiki. Wapo wanaoamini Harmonize alikuwa akieleza hisia zake kutokana na aliyopitia kwenye uhusiano huo, huku wengine wakiona masuala ya kimapenzi yanapaswa kubaki faraghani.
Penzi lililowahi kutikisa mitandao
Tangu walipoanza kuonekana pamoja hadharani, Kajala na Harmonize walikuwa miongoni mwa wapenzi waliovuta hisia za mashabiki wengi wa burudani nchini. Mahusiano yao yalikuwa gumzo mara kwa mara, yakigubikwa na vipindi vya furaha, migogoro na tetesi za kuachana na kurudiana.
Kila mmoja wao alipowahi kuonekana bila mwenzake au kutoa kauli zenye utata, mitandao ya kijamii ilijaa mijadala kuhusu hatma ya penzi lao. Hata sasa, baada ya kauli ya Harmonize, mjadala huo umeibuka tena.
Kajala aendelea kulinda ukimya
Tofauti na Harmonize ambaye ameamua kueleza hisia zake hadharani, Kajala ameonyesha wazi kuwa kwa sasa hayupo tayari kuzungumzia suala hilo.
Kwa sasa, jambo lililo wazi ni kwamba Harmonize amesema upande wake, huku Kajala akichagua kubaki kimya na kuwatumia mashabiki wake salamu fupi ya upendo, bila kuingia katika mjadala wa mahusiano yao.