Arsenal yabanwa kwa Bruno Guimaraes!
Muktasari:
- Kwa mujibu wa mwandishi wa Sky Sports, Keith Downie, Guimaraes tayari ameuambia uongozi wa klabu hiyo kuwa anatamani kujiunga na Arsenal katika dirisha hili la usajili.
LONDON, ENGLAND: KLABU ya Newcastle United imeanza kuchoshwa na namna Arsenal inavyofuatilia kiungo wake na nahodha, Bruno Guimaraes, huku ikisisitiza haitamuuza kwa chini ya pauni milioni 80 (zaidi ya Sh bilioni 280).
Kwa mujibu wa mwandishi wa Sky Sports, Keith Downie, Guimaraes tayari ameuambia uongozi wa klabu hiyo kuwa anatamani kujiunga na Arsenal katika dirisha hili la usajili.
Hata hivyo, hadi sasa Arsenal haijawasiliana rasmi na Newcastle kujadili uhamisho huo. Badala yake, imekuwa ikitumia mawakala na watu wa kati kuchunguza uwezekano wa dili hilo, jambo ambalo limewakasirisha viongozi wa Newcastle.
Inaelezwa Newcastle imefikia hatua ya kuiuliza Arsenal kama kweli ina nia ya kumsajili nyota huyo wa Brazil kutokana na kutopokea ofa yoyote rasmi.
“Mpaka sasa Arsenal haijawasiliana nasi. Kila kitu kinaendelea kupitia mawakala na hali hiyo inamvuruga mchezaji, ndiyo maana ameonyesha nia ya kutafuta changamoto mpya,” alisema Downie.
Newcastle inataka kubaki na nahodha wake, lakini inaamini thamani yake ni zaidi ya pauni milioni 80, ikiwa ni pauni milioni 20 chini ya alizouzwa Sandro Tonali kwenda Tottenham mapema mwezi huu kwa pauni milioni 100.
Downie alisema Guimaraes anatamani kucheza katika timu yenye nafasi kubwa ya kushinda mataji, lakini Arsenal italazimika kuweka mezani ofa kubwa kabla Newcastle haijachukulia uzito nia yao.
“Wanasema Guimaraes hauzwi, lakini mchezaji anapoonyesha wazi anataka kuondoka, inakuwa vigumu kumzuia. Hata hivyo Arsenal lazima itoe ofa rasmi, si kupitia watu wa kati,” aliongeza.
Katika dirisha hili la usajili, Newcastle tayari imeingiza fedha nyingi baada ya kumuuza Anthony Gordon kwenda Barcelona kwa pauni milioni 69.3 na baadaye Sandro Tonali kwenda Tottenham kwa pauni milioni 100. Pia imetumia pauni milioni 83.5 kuwasajili Bazoumana Toure, Sean Steur na Ewen Jaouen.
Kwa upande wa Arsenal, bado haijakamilisha usajili wowote mkubwa. Morgan Rogers, ambaye alikuwa kwenye rada zao, amejiunga na Chelsea kutoka Aston Villa, huku jitihada za kumsajili Guimaraes zikiwa bado hazijafikia hatua ya ofa rasmi.
Guimaraes, ambaye anakaribia kutimiza miaka 29, ameichezea Newcastle mechi 195 katika mashindano yote na kufunga mabao 31 tangu aliposajiliwa mwaka 2022 kwa pauni milioni 40.
Kiungo huyo wa Brazil anaonekana kuwa chaguo muhimu kwa Arsenal kutokana na uongozi wake, uzoefu mkubwa na uwezo wa kucheza majukumu mbalimbali katikati ya uwanja, huku mabingwa hao wa Ligi Kuu England wakitaka kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya kutetea taji na kutawala zaidi soka la England.